Japo wakenya wakisema kuna mambo wanazidi nchi nyingine huonekana kama wanajisifia sawa na watanzania. Mfano, wakenya huiita nchi yao economic hub of East and Central Africa sawa na watanzania wanavyojiita kisiwa cha amani barani Afrika. Kuna mambo wakenya wana haja ya kujisifia sawa na watanzania na wananchi wengine wa nchi za kiafrika zilizotengenezwa na mkoloni jambo ambalo linaonyesha namna tunavyoshangilia ukoloni kiasi cha kuushiriki kwa namna moja au nyingine.
Pamoja na mijisifa mingine isiyo na msingi, kwa sasa Kenya inangia kwenye kundi teule barani la nchi za Afrika ya Kusini, Botswana na Ghana kama nchi zinazoweza kujisifu kuwa zina katiba zilizostaarabika. Kwani, katiba za nchi hizi zimefanya kila mhimili wa dola kujitegemea na kutoingiliwa wala kuingilia mihimili mingine kama inavyotaka dhana ya utawala bora na wa sheria. Chini ya dhana hii, juzi dunia, kwa mara ya kwanza, ilishuhudia ushindi wa rais ukifutiliwa na kubatilishiwa mbali na mahakama. Kitendo hiki, licha ya kuiletea Kenya sifa kedekede, kimeiweka mbele hata kuliko nchi vigogo vinavyojigamba kuwa mabingwa na walimu wa demokrasia kwa Afrika kama vile Marekani ambayo ina migogoro ya matokeo ya uchaguzi sawa na nchi za kiafrika.
Pia uamuzi huu umekuwa suto karibu kwa nchi zote za kiafrika ukiondoa zile zilizoonyeshwa hapo juu. Ni suto sana kwa Afrika Mashariki ambayo licha ya kuwa na serikali mbili tu za kidemokrasia za Kenya na Tanzania, ina wingi wa viongozi ving’ang’anizi wa madaraa chini ya visingizio mbali mbali.
Leo safu hii itaangalia masomo yanayopatikana kwenye uamuzi wa mahakama kuu ya Kenya wa kufutilia mbali ushindi wa rais. Kwanza, haijawahi kutokea popote duniani. Je Kenya imefanya hivi kutokana na kuwa na watu wa ajabu? Hasha. Ni kutokana na kuwa na katiba bora yenye kutokana na utashi na mawazo ya wananchi iliyoanza kutumika mwaka 2010. Katiba ya Kenya inatoa haki kwa raia yoyote kupinga matokeo yoyote katika nafasi za kuchaguliwa hata kuteuliwa anapohisi haki haikutendeka. Wakati Katiba ya Kenya ikifanya hivyo, ya Tanzania hairuhusu hata kuhoji matokeo hasa ya urais. Inamuweka rais juu ya sheria jambo ambalo licha ya kuwa moja ya masalia ya ukoloni, ni aina fulani ya ukoloni ulioendelezwa na watawala waliopokea uhuru na waliowafuata kwa hofu ya kuondolewa madarakani hata kushitakiwa walipovurunda.
Pili, tokana na kuwa na Katiba inayotoa uhuru na haki kwa wananchi wengi, hata taasisi za Kenya kama vile Mahakama na nyingine zinao uhuru na wajibu kwa wananchi wote bila kujali mamlaka yao. Hivyo, mahakama ya Kenya ni huru; na uamuzi wake hauwezi kuingiliwa na mhimili mwingine kama ilivyo kwenye nchi nyingine ambako mahakama hutumika kama mhuri au rubberstamp wa utawala.
Si mahakama tu. Hata bunge la Kenya lina haki na uhuru kuliko mabunge mengi ya Afrika ambayo hutumika kama nyumba ndogo za utawala katika kulinda na kuendeleza uovu. Mifano midogo ni nchini Rwanda na Uganda ambapo mabunge yalipitisha sheria za kuruhusu watawala wao kubadilisha katiba ili kubakia madarakani kinyume cha matakwa ya wananchi.
Tukija Tanzania, bunge letu bado si huru tokana na kuwa na wabunge wengi wa chama tawala; jambo ambalo hulifanya lipitishe mambo ya hovyo bila kuogopa kushughulikiwa kisheria. Ukiachia hili, ukosefu wa sheria inayolipa madaraka hata likiwa chini ya chama kimoja kama mhimili wa dola yanaonekana namna chama tawala kinavyolitumia litakavyo bunge. Mfano wa hivi karibuni ulijitokeza hivi karibuni nchini Afrika Kusini ambapo katiba huru hulipa bunge uhuru. Baada ya vyama vya upinzani kutoridhishwa na udhu wa rais wa nchi hiyo mwenye wingi wa kashfa za rushwa na ukosefu wa maadili hata binafsi Jacob Zuma, walikwenda mahakamani na bunge likaamuru rais apigiwe kura ya kutokuwa naye imani. Kama si kuwa na wabunge wengi wa chama chake–ambacho kimechakaa tangu aondoke rais wa kwanza wa nchi hiyo shujaa Nelson Mandela kama CCM baada ya Nyerere– walimuokoa. Ingekuwa Tanzania nani alitegemea upinzani upeleke hoja bungeni halafu spika aipitishe? Ni mara moja ilipotokea bunge likapitisha hoja ya kutaka kuishughulikia serikali mwaka 2008 ambapo–tokana na siasa za makundi ndani ya chama tawala na ushiriki wa rais mwenyewe kwenye kashfa–alimtoa kafara waziri wake mkuu.
Somo jingine linalotolewa na ubatilishwaji wa matokeo ya urais nchini Kenya ni kwamba Tanzania inahitaji kufikiri upya juu ya kuendelea kuua rasimu ya katiba mpya ya wanachi iliyolenga kuondoa mabaki ya ukoloni Tanzania ambayo imekuwa ikiendeshwa na katiba viraka ya zamani isiyo endana wala kukidhi matakwa ya watanzania. Katiba ya sasa ni ya watawala na si ya wananchi tofauti na katiba ya Kenya ambayo ni ya wananchi na wanaweza kuitumia dhidi ya watawala hata akiwamo rais bila kikwazo wala woga.
Tumalizie kwa kuwataka watanzania na hata watawala kuanzisha mchakato wa kudai kurejeshwa kwa mchakato wa katiba mpya kama kweli si wanafiki wanataka kuikomboa na kuiendeleza nchi kama wengi wanavyosema. Tunataka matendo na si maneno. Tunataka katiba mpya sasa.
Chanzo: Tanzania Daima J'pili kesho.
No comments:
Post a Comment