The Chant of Savant

Wednesday 20 September 2017

Wilaya ya Ilala isiwaonee ombaomba


            Hivi karibuni rafiki yangu alinitumia kipande kilichorekodiwa cha tangazo la wilaya ya Ilala likiwataka wananchi kutotoa fedha kwa ombaomba wala ombaomba kuomba; na watakaokiuka watachukuliwa hatua za kisheria. Tangazo hili, kwanza lilinishangaza; na pili lilinisikitisha kutokana na sababu zifuatazo:
            Mosi, kwanza, hakuna sheria kama hiyo. Nadhani mtoa tangazo ima hajui sheria au anajifanya kutojua sheria hasa anaposema kuwa suala hili litashughulikiwa chini ya sheria ndogo ndogo ambazo hazina nguvu zinaposimama dhidi ya sheria mama yaani katiba ambayo haisemi kuomba kihalali ni kosa.
            Pili, ni ile hali ya baadhi ya watawala wetu kukurupuka na kushupalia mambo madogo wakati makubwa wakiyaacha au kuwashinda. Hivi kweli ombaomba ni tatizo sawa na mafisadi au wahalifu ambao kwa sasa wamepewa cheo cha watu wasiojulikana? Hivi ombaomba ni tatizo kubwa kuliko uchafu, uzembe, ukahaba na ulevi na kadhia nyingine kwa wilaya ya Ilala?
            Tatu, kwanini wilaya ya Ilala imeona ombaomba kama tatizo kubwa kuliko mengine mengi inayokabiliana nayo kama vile uingiaji wa wahamiaji haramu uliotamalaki nchini hadi wengine kufikia kuendesha biashara bila leseni wala vibali ya kufanya kazi wala kuishi nchini?
            Nne, je wilaya ya Ilala ina habari kuwa taifa lao nalo ni ombaomba? Rejea wakati wa utawala uliopita ambapo rais mstaafu Jakaya Kikwete alilalamikiwa sana na kusifiwa kwa kuzunguka dunia akiomba misaada huku serikali yake ikizembea kiasi cha kuacha madini na raslimali nyingine nyingi zenye thamani kubwa kuliko pesa ya kubomu vikiibiwa kila uchao. Rejea kutoroshwa kwa wanyama hai tena mchana kweupe ukiachia mbali madini yetu yenye thamani ya mabilioni. Hapa hatujaongelea viwanda bubu ambavyo vingi vinamilkiwa na wageni au wahamiaji haramu kama alivyowahi kubaini mkuu wa wilaya ya jirani ya Temeke hivi karibuni.
            Tano, hivi wilaya ya Ilala haijui sababu ya kuwa na raia ombaomba nchini? Tumegusia baadhi ya maovu kama vile ufisadi, wizi wa fedha za umma, uzembe, ubinafsi na ulevi wa madaraka. Nadhani ni mlevi wa madaraka anaweza kuona ombaomba kama tatizo kubwa kuliko ufisadi tokana na ukweli kuwa wengi wa ombaomba wetu wamezalishwa na mipango mibovu ya serikali zetu ukiachia mbali ufisadi uliozalisha watendaji wa umma wanaotumikia wezi wa nje na ndani kwa kuwauma watu wetu na raslimali zao. Rejea namna ambayo rais John Magufuli anavyohangaishwa na ufisadi kiasi cha kuogopa hata kusafiri nje. Rejea kufichuka kwa wizi mkubwa wa madini ya dhahabu kwa njia ya makinikia ukiachia mbali wizi wa almas na tanzanite.
            Sita, je wilaya ya Ilala inaendeshwa kwa sera zipi wakati serikali yake inaongoza nchi ombaomba kimataifa? Au ni yale ya nyani haoni nonihino lake au ile ya mwenye shibe hamjui mwenye njaa?
            Saba, ukiachia nchi kuwa ombaomba wakati ina raslimali lukuki, kuomba si kosa kisheria wala kimaadili. Kuomba kunakoharamishwa ni kama vile kuomba rushwa iwe ya fedha au ngono au upendeleo. Je hii jinai ya kuomba rushwa nchi ikoje? Kuomba ni haki ya binadamu hasa anapokuwa na tatizo ambalo hawezi kulitatua. Ndiyo maana watu hufurika makanisani na misikitini kuomba kila siku. Ukiachia mbali kuomba kuwa si kosa kisheria sawa na mengine tuliyoeleza, hata nchi tajiri na zilizoendelea bado zina ombaomba na haziwabughudhi kwa kujua kuwa kuomba si kosa; na baadhi ya ombaomba wanazalishwa na sera mbaya za serikali au nchi.
            Nane, je nini kifanyike?
            Nashauri wilaya ya Ilala na wengine wenye mawazo kama haya, kwanza wajikite kwenye kuokoa, kusimamia na kulinda raslima za umma ili kupunguza umaskini ambao ndiyo mzazi wa ombaomba wanaokimbia maisha magumu vijijini tokana na kutokuwa na elimu, ujuzi wala mitandao ya kuwawezesha kupata kazi na kuishi maisha mazuri. Sijui kama kuna mtu mwenye akili timamu anaweza kupenda kuomba au kukuonea fahari.  Kama nchi haioni aibu kuombaomba, itakuwaje wananchi wake tena wasio na raslimali sawa nan chi?
            Pili, nashauri wilaya ya Ilala itafute njia za kukuza uchumi kwa kupambana na vipingamizi kama vile wahamiaji haramu, ufisadi, wizi wa fedha za umma, ufujaji wa raslimali na mali za umma.
            Tatu, simamieni ukusanyaji wa mapato ili muwe na kipato cha kutosha kiasi cha kuanzisha miradi ya kupunguza vijana wasio na kazi na wengine wenye uhitaji kwenye eneo lenu badala ya kutoa amri za ajabu ajabu msijue zitawageuka.
            Mwisho, kabla ya kufikiria achia mbali kutangaza kuwafukuza ombaomba, mfikiri mara mbili. Je ombaomba wanatokana na nini? Je nyinyi si sehemu ya tatizo? Je mwaweza kuwa sehemu ya suluhisho? Je kuzuia wananchi kutoa fedha yao kwa wanaowaonea huruma mnadhani kuna nguvu kisheria kama mnavyotishia? Hata nchi yenyewe inapewe misaada na yeyote anayeionea huruma bila kutenda kosa lolote. Sasa kama nchi yenye kujaliwa kila aina ya raslimali ikazivuja ukiachia mbali kuwa na vyanzo vingine inaomba, itakuwaje mwananchi wa kawaida? Fikiri mara mbili.
Chanzo: Tanzania Daima J'tano leo.

No comments: