Heko Rais Magufuli

Saturday, 16 September 2017

Pole Tundu mwana wa Lissu


            Leo naandika kwa hasira na uchungu hakuna mfano. Hivyo, yoyote anayesoma waraka huu uliovuviwa rohomtakahaki na mpingamaouvu kilevi, asidhani ni hasira au mawazo ya kilevi hata kama umeandikwa na mlevi akimtetea mlevi mwenzake wa kanywaji aina ya Justice alikopenda kupiga mzee Mchonga. Waraka huu ni karipio dhidi ya walevi wa majanga mengine kama madaraka, uhalifu, woga na upumbavu kama mtakavyoona. Hii ni baada ya mlevi mwenzangu Tunduni Liisu kumiminiwa shaba kama mia hivi, lakini akatoka mzima wa afya ukiachia mbali majeruhi. Waliotaka kumnyotoa roho wameshindwa na washindwe sana na kunyong’onyea kwa majina ya mizimu ya mababu zetu.
            Hakuna kitu kimetuudhi na kutustua walevi kama tukio hili la kijinga, kipumbavu na kishamba. Hawa wanahizaya wanaonekana hamnazo. Wanadhani wakimnyotoa roho Liisu watakomesha ulevi wake wa kanywaji aina ya justice? Unaweza kumnyotoa roho mlevi hata kupiga marufuku ulabu lakini huwezi kuua ulevi. Sijui kwanini washenzi hawa walitumia makalio kufikiri badala ya vichwa. Kama wanadhani kunyotoa roho ya Liisu ni suluhu, basi wajue ni mwanzo wa tatizo na sehemu ya tatizo. Kwani, akidondoka Liisu mmoja, mia wanachipuka tena kwa ukali zaidi. Kwanini hawataki kujifunza kutokana na kunyotolewa roho Chris Mtikisa? Si alikufa kwa ajali ya barabarani tata wakadhani walevi wa haki watanyamaza. What a mistake! Si Liisu aliibuka ghafla bin vu na kuchukua usukani wa kukemea na kukosoa maovu. Dawa ya kuepuka na kelele na maudhi ya walevi kama Liisu ni kuachana na kutenda uovu unaowapa jeuri ya kuwazozea wanaoteanda uovu.  Hivi tunakwenda wapi jamani? Mzee Mchonga akifufuka leo anaweza kujinyotoa roho hasa ikizingatiwa kuwa kaya yake inaelekea kwenye kila watasha husema to the dogs. Who wants to be a witness of such sacrilege?
            Leo naandika kwa hasira sana hadi naanza kuchukia baadhi ya mijitu tena inayojidai iko kulinda usalama wa walevi. Leo nitauliza kilevi tu. Hivi ndata walikuwa wapi hadi Liisu anamiminiwa shaba mchana kweupe kama hakuna namna au wanazembea kwenye usukani ikizingatiwa kuwa walishapewa rangi na namba ya ndinga waliyotumia wanahizaya kumshambulia Liisu? Je inakuwaje mlevi analalamikia usalama wake jamaa wanalaza damu au ni wale wale waliomteka yule mfokaji aitweye Romania ya Katoliki? Wanahizaya hawa wamechoka na amani siyo? Je wanadhani watafanikiwa kunyamazisha walevi? Wanadhani hii kaya ni ya mama zao siyo? Sasa kitaeleweka. Nafanya mpango kuwahamasisha walevi tuandamane na michupa yetu kutaka kijulikane kwa kukinukisha kutaka lisirikali litoe maelezo kwanini halikumpa ulinzi Liisu wala kuchukua hatua au ni kwa vile ni mpingaji?
            Mnashindwa kupambana na majizi na majambazi yanayosafirisha mali za kaya kana kwamba inaendeshwa na machizi mnapoteza muda kuwaadamana walevi? Kama kweli waliofanya kitendo hiki ni wazalendo, basi wasingepoteza muda kufanya huu unyama, ulimpyoto na unywanywa zaidi ya kwenda kuwasaka wanaobaka kaya yetu tena mchana kweupe. Maana inashangaza wahalifu kujiamini na SMG na kufanya ualifu mchana kweupe mji mkuu. Je hizo nyumba za wanene wahishiwa na mitaa yake haina CCTV kamera au hadi niwaazime zangu? Je waliomshambulia Liisu kweli hawajulikani; na lengo la unyama wao? Wanaodhani kuwa kuua ni jibu wanapaswa watubie na kuelimishwa kuwa hilo si jibu bali tatizo hasa ikizingatiwa kuwa hakuna ngurumbili atakayeishi milele hata aue wenzake vipi. Wako wapi akina Ceausescu, Gadaffi, Hamurabi, Hitler, Pinochet, Saddam, Stalin, na mimla wengine waliotekeza mamilioni wasijue nao siku zao zikifika watarejesha namba?
            Kwa vile walevi tuna akili, kama ndata wataendelea kucheza makidamakida na wahalifu hawa, nasi tuaamua kama mbaya mbaya tutaamua kuwatafuta kwa tujuavyo na kuwachoma moto kama vibaka. Huwa nashangaa kwanini walevi tunapata wepesi wa kuwachoma moto vibaka wakati tukiwanyamazie mibaka kam iliyotajwa juzi kwenye wizi wa mawe! Sasa ngoja nilonge sasa. Badala ya kuwaandama vibaka, basi tuwasake hawa wanaotaka kunyotoa roho walevi tokana na mawazo yao na kuwachoma moto tena baada ya kuwafanya kitu mbaya.
            Pia Liisu akipona nitamshauri akienda kwenye njengo apeleke hoja ya kubadili ndata. Haiwezekani waendelee kulipwa njuluku za kodi zetu waendelee kuacha tuuawe na wakora. Pia lazima lisirikali lionywe. Haliwezi kupandisha bei ya kanywaji na kupata njuluku na kununua kila zana za usalama lakini zikaishia kutumika kuwakandamiza walevi na kuacha wengine wanyotolewe roho na wahalifu wapumbavu na woga. Kama wangekuwa njemba kweli si wangekwenda kuzipiga na Liisu badala ya kumshambulia kwa shaba. Shame on them and whoever sent them! Mungu anawaona hata kama kuna wanaowafumbia macho.
            Namaliza kwa kuwalaani wanahizaya wote waliomshambulia Liisu iwe moja kwa moja au vinginevyo. Nawalaani wote wanaowateka wenzao ambao sasa wameanza kuwaua. Nalaani wote wanaozembea kwenye wajibu wao. Nalaani wote wanaomchukia mlevi kwa mawazo yake na si uovu. Nalaani nda…we! Kwa kutochukua hatua hata walipopewa taarifa ya kuwepo kwa maandalizi ya uovu huu. Walaaniwe wote ikiwezekana wafe taratibu ili wateseke. Aaaminaaaaaaaaa.
Chanzo: Nipashe J'mosi leo.

No comments: