The Chant of Savant

Sunday 10 September 2017

Mlevi ataka Katiba Mpya kama Kenya


            Baada ya mwana wa mfalme U-freedom Kinyataa kunyang’anywa ulaji wa dezo unaosemekana kupatikana kiharamu kwa njia ya uchakachuaji ambao sasa umegeuka fasheni Afrika, ilibidi nisukuti. Tokana na kusukuti huku, leo sitaki longolongo wala mizungusho bali kusema kwa kinywa kipana tena kwa herufi kubwa kuwa kaya yetu inahitaji katiba mpya ili kufanya mambo kisasa na si kizamani kama ilivyo na ilivyozoeleka. Hebu msomaji tuseme pamoja kwa herufi kubwa “TUNATAKA KATIBA MPYA ILI TUFANYE MAMBO MAPYA”
            Naona yule anagwaya akidhani yatamkuta yanayowakuta akina Tunduni Liisu. Ogopa Mungu si miunguwatu. Wanaweza kufunga mwili wako lakini  si mdomo wako wala mawazo yako. Kwani kaya hii ni yao au mama zao? Hebu tusema pamoja “TUNATAKA KATIBA MPYA SASA VINGINEVYO HAPAKALIKI HAPA.”
            Japo inaweza kuonekana kuwa najipa ujiko na kujifagilia, ni kwamba mawazo yangu yamechangia kufikia hapa ninapoongelea. Naona yule anatikisa kichwa na kusonya. Kama unadhani hizi ni kamba au longolongo asome gazeti la Kenya linaloheshimika la Daily Nondo utakuta nondo na vimondo vyangu. Kwa wasiojua hawa jamaa wanavyopendana kiasi cha kutotaka wageni waingilie mambo yao, kupata fursa ya kutupa mawe mle si kawaida. Lazima kichwa kiwe kinajibu na kuchemka kweli kweli. Nadhani mimi ni mlevi pekee toka Bongo aliyepata fursa ya kutupa mawe mle si mara moja wala mbili. Naona yule anazidi kubeua midomo na kutikisa kichwa. Maskini hajui kuwa nabii hakubaliki nyumbani yaani kwa kilatini Nemo profita in patria sua. Hayo tuyaache.
            Kuna maswali ya kujiuliza. Je ilikuwaje mwana wa mfalme akanyang’anywa tonge mdomoni wakati alikuwa na kila zana za kuchakachua?  Si baada ya kustukia mchezo wa uchakachuaji, mpinzani wake Jadwong Madwong amaye by extension ni rafiki yangu na dingi, akaenda kwa Pilato. Kwa vile Katiba ya kule inaruhusu kila mlevi kwenda kwa Pilato anapohisi hajatendewa haki si Pilato akampa alichotaka kwa kumpiga chini mwana wa mfalme. Just imagine. Unadhani ingekuwa Bongolala na katiba yetu viraka jamaa angetoboa kama wasemavyo huko? Wala kisingeumana.
            Kwa vile nimependa chesi hii, nawaalika walevi wote wapenda demokrasia bila ghasia na maendeleo vya kweli waje tupange namna ya kuwabana wanene wetu warejeshe Katiba yetu mpya ya jaji Jose Waryuba iliyouawa na majambazi na mafisadi ili wasinyee debe kama akina Singasinga na Rugetumbuliwa bila kumsahau jamaa yangu Manjilinji. Au vipi walevi? Semeni kwa pamoja ‘Tumechoka na longolongo, ubabaishaji na mauaji ya Katiba mpya ya kaya.” Sema tena “Tunataka Katiba mpya na si uongo mpya.”
            Ninapoandika hapa, dingi atakuwa akitabasamu kwa swahiba yake kupata fursa nyingine ya kujaribu urahisi huku ndugu yangu Eddie aliyeshabikia upande wa pili akiugulia kwa machungu ya hukumu hii takatifu.
            Tukirejea umuhimu na majaliwa ya Katiba mpya, lazima niseme bila kumung’unya kuwa huwezi kuendeleza kaya bila kuwa na haki na uhuru kwa wanakaya kama ilivyo sasa. Hivyo basi, wote wanoota ndoto za nchana kuwa kaya inaweza kuendelea kwa maigizo wanapoteza muda. Maana, Katiba mpya ndiyo muarobaini wa ufisadi, uvivu na ubabaishaji ambavyo dingi amejaribu kutumbua akaishia kuchoka kabla hata hajamaliza ngwe moja. Hata hivyo, amejitahidi. Sema angekuw anashaurika, hakuna jambo la maana angewatendea walevi kama kufufua nchakato wa Katiba mpya ili itumike kuleta usawa, haki na uwajibikaji kayani kama ilivyotokea kwa majirani zetu wa the country of man eat man hivi karibuni.
            Huwezi kuendeleza kaya wakati kuna matabaka ya walevi ambapo wapo wasioguswa na wanaotolewa kafara kwa sababu wanaeleza mawazo yao ambayo ni haki yao kikatiba. Huwezi kuendeleza kaya kwa katiba viraka na makengeza kiutendaji ambapo baadhi ya wahalifu wanakingiwa kifua tokana na ukaribu wao kwa wakubwa au ukubwa wa vyeo walivyoshika au kushikwa na maswahiba au waramba viatu wao kama ilivyo.
            Leo sichongi sana. Nakwenda kujiandaa kulianzisha la kudai upya katiba mpya. Kusema ukweli natamani Maraga angekuwa Bongo lau tumpe ofa na kumpongeza. Kwa wale wanaoatamia katiba yetu mpya wakae wakijua kuwa wanakalia kaa la moto. Kumbe naota! Hata hivyo, tuseme "TUNATAKA KATIBA MPYA."
Chanzo: Nipashe J'mosi, jana.

No comments: