Taarifa za kushambuliwa kwa risasi na kujeruhiwa kamanda Tunduni Lissu zimesikitisha kijiwe. Baada ya kuzinyaka, kila mmoja alionyesha kusononeka huku tukilaani ujinga, upumbavu na unyama huu.
Mijjinga anaingia akiwa anasonya na kutikisa kichwa kwa hasira, ngoa na uchungu. Tokana na ukweli kuwa tulikuwa tumeishapata breaking news toka radio mbao, tulijua wazi kilichokuwa kimechukiza na kumsikitisha. Baada ya kuamkua anasema “hivi nani ataishi milele tumuone lau mjanja kuliko wauaji na washamba wanaoanza kuhalalisha utekaji na uaji kayani? Ama kweli kiburi ni fimbo ya mpumbavu. Unamwaga damu ya mtu asiye na hatia halafu utegemee mafanikio? Kawadanganya nani wapumbavu na wauaji nyie msio na akili wala maono?”
Kabla ya kuendelea Msomi Mkatatamaa anamfariji kwa kumpigapiga mgongoni. Anasema “brother hili tukio la kushambuliwa kwa mwanakijiwe mwenzetu Tunduni Lissu hata kama huwa hashiriki kijiwe limetuhuzunisha na kutuchukiza hakuna mfano. Hawa wanahizaya waliojificha nyuma ya kinachoitwa wahalifu wasiojulika ni woga na washamba wasiojua maana ya kuvumiliana. Wanadhani wanaweza kutunyamazisha. Wanaweza kumuua Lissu lakini si mawazo yake. Akifa Lissu mmoja wanaibuka kumi. Hivyo, dhamira yao ovu haitafanikiwa.”
“Usemayo ni ya kweli. Kwani alivofishwa Ntikila si alikuja huyu Tundu? Waweza ua Tundu lakini hatoliziba hili tundu linilosababishwa waja wanene hata kuweka maisha yao hatarini ati. Kwani hao walotaka kumua wataishi milele wakati kila kit ki wazi kuwa kul nafsi zalikatul maut yaani kula nasi itaonya mauti?” Mpemba anajibu kwa hasira huku wanakijiwe wakishangaa anavyotafuna kimanga kama wamanga wenyewe. Laiti kingekuwa kimombo huenda angekuwa mbali na hapa kijiweni.
Kapende anakula mic “sikutegemea kuwa tungefika hapa na kuonekana kama kaya katili na ya hovyo kama zile zinazotawaliwa na maimla katili na mauaji. Hapa lazima kuwa na mkono wa mtu. Je SMG walotumia hawa wahalifu ilipatikana wapi? Hapa ndata lazima watoe maelezo inakuwajekuwaje wahalifu wanatesa mchana kweupe bila kuwanyang’anya silaha wakati rahis alishaagiza wawanyang’anye hizo silaha?”
Kabla ya kuendelea Mgoshi Machungi anamnyang’anya mic “hii shambuio inashangaza sana.
Je seikai iichukua hatua gani pae Lissu aipotoa taiifa kuwa anafuatwa na wahalfu wanaotishia usaaama wake zaidi ya kunyamaza? Je hapa kwei itazuia wachovu kusema mambo tena yasiyopendeza? Je hawa ndata waikuwa wanafanya kazi gani wakati tinajua kuwa wamekuwa wakimfuata mjengoni na kumkamata au ni kwa vile si wa chama chao?”
“Chungi veve sema kweli kweli. Kwanini data napata guvu ya kamata yeye jengoni lakini hapana linda yeye kama hapana tatizo? Hii tisa sana” anachangia Kanji.
Msomi Mkatatamaa aliyekuwa akisiliza na kutikisa kichwa kila mara anaamua kutia guu “Kanji umesaidia kujibu swali kubwa yaani nini wajibu wa lisirikali kwa usalama wa wapingaji. Linachoweza kukufanyia si jingine bali kukusweka ndani kwa kulalamikalalamika. Tujulize maswali mengine. Je waliomshambulia Liisu si wale waliomtishia kwa bunduki Mapepe Ninaye alipochunguza hujuma ya Bashit dhidi ya Klaudz? Je hawa wahalifu walipata wapi SMG na jeuri ya kufanya uhalifu mchana kweupe tena kwenye makao makuu ya kaya? Je kwenye nyumba za wahishiwa hakuna walinzi? I can’t understand this game really. Je wafe wangapi ndipo lisirikali listuke na kutimiza wajibu wake au kwa vile Liisu ni mpingaji? Wameshindwa kupambana na majambazi na mafisi yanaoiba mawe yetu kila uchao wanahangaika na wapingaji wanaowapa vipande vyao? Hawa wahalifu wanapaswa kusakwa, kama alivyosema rahis, wakamatwe na kujibu mashtaka haya ya uuaji na upumbavu.”
Sofia Lion aka Kanungaembe anakula mic “kusema ukweli haya mambo yanatisha. Ni ukatili, upumbavu na unyama vya hali ya juu. Nadhani kama kaya tunapaswa kuangalia historia yetu na kuzingatia umuhimu wa amani. Sidhani kama hawa wanaotaka kunyamazisha au kutoa roho za wenzao wana nafasi katika kaya hii. Sidhani kama hawa wanaotumia njia za giza ni wenzetu au wanataka kutuchonganisha? Maana haiwezekani mja aeleze maoni yake auawe. Hawa wana nia mbaya na kaya yetu. Hivyo, nashauri mamlaka ziwashughulikie haraka kabla mambo hayajavuka mipaka.”
Mheshimiwa Bwege aliyekuwa kimya muda wote anaamua kukamuua mic “ nimewasikilizeni sana kwa muda mrefu. Hivyo nisemacho si kipya bali kutia msisitizo. Kwanza, nakubaliana huu ni ubwege wa mwaka kufikiri kuua nafsi kutaondoa tatizo. Pili, nakubaliana kabisa kuwa hapa lazima uwepo mkono wa mtu. Swali muhimu ni: kwanini ndata walipotaarifiwa hawakuchukua hatua wakati wanasifika kwa kumsweka Tunduni ndani bila makosa mara kwa mara? Lazima tuelezwe tujue. Maana hii kaya ni yetu sote bila kujali nani ni nani ilmradi uwe raia halali wa kaya hiii iliyozoeleka kuitwa kisiwa cha amani ambacho sasa kinageuka kisiwa cha mauaji na unyamazishaji. Hatuwezi woe kuwa mabwege kama hao wanaotaka kuua wenzao. Lazima tuseme hapana. Hivyo ndiyo sivyo. Mtatupeleka pababaya mshindwe kututoa huko. Kubomoa ni rahisi kuliko kujenga. Ni bwege pekee adhaniaye kubomoa ni sehemu ya kujenga.”
Kijiwe kikiwa kinanoga si likapita shangingi jeupe. Sie kwa hasira tulidhani ni la mabashite watekaji na wauaji. Tukiwa tumeliweka kati si akatoka mshikaji wetu ambaye jina sitaji!
Chanzo Tanzania Daima J'tano kesho.
No comments:
Post a Comment