The Chant of Savant

Saturday 23 September 2017

Mlevi kupambana na watu wasiojulikana

            Baada ya watu wasiojulikana–au tuseme wahalifu wanaojulikana- wakajjficha nyuma ya kutojulikana tokana na ushamba na ujinga–wamekuwa tishio kayani. Kwanza, sidhani kama kuna watu wasiojulikana wanaoweza kuishi kwenye kaya inayojulikana tena yenye kujisifia kwa kuwa na vyombo vya usalama vyenye kuaminika kiasi cha wakubwa kuwahakikishia walevi kuwa wasiwe na wasiwasi juu ya usalama wao kana kwamba hawa wanaoshambuliwa si raia wa kaya hii. Kaya yoyte ikifikia mahali kama hapa ambapo wahalifu wachache, tena wasiojulikana kuiteka, uje kuna tatizo kubwa tu. Sijui usalama wa kaya kama unaweza kutolewa kafara hivi. Je ni kwa faida ya nani na ili iwe nini kama siyo aina nyingine ya ulevi tena mbaya kuliko wa kanywaji? Hawa watu wasiojulikana wanajulikana. Mheshimwa Tunduni Lissu anawajua; n ahata wahishimiwa wabunge waliofuatiliwa nao wanawajua tu.  Hivyo, wanajulikana; na kila kitu kinajulikana hata wale wanaowatuma wanajulikana. Kama hawajulikani basi wao wanajijua.
            Juzi walevi walinisonga na mawazo wakitaka kujua geshi la nini kama wahuni wachache wanaotumia fursa zao vibaya kwa kuwaumiza hata kuwaua wenzao? Je ndata nao ni wa nini kama wanashindwa na wahalifu na washamba wachache tena wasiojulikana? Basi hata dingi hana sababu ya kuwapo akilipiwa kila kitu wakati kila kitu kimekaa ndivyo sivyo kuhusiana na usalama wa walevi. Walevi wanataka usalama wa uhakika; na kuwaumbua hawa wahalifu wanaojifanya hawajulikani.
            Hawa watu wanajulikana; si mazombi, wala popobawa wala maruhanni. Ni wahalifu, ni washamba, ni wauaji, na yote katika yote, ni washenzi wanaopaswa kutokomezwa kama ndui. Hivyo, wasiendelee kujificha kwenye kutojulikana wakati wanajulikanaau kuvimbisha bichwa kuwa wataendelea kutojulikana. Kwani zimepita tawala ngapi kaya hii? Mbona wakati wa mzee Mchonga hatukuwasikia wala waliofuatia hadi juzi tu?  Kwa vile mimi nimesomea usalama, nitahakikisha nawafichua na kuwaumbua ili wale wanaodhani hawajulikani wajue wanajulikana. Mlevi lazima niwasake na kuwafanyia kitu mbaya tena nchana kweupe. Kitu ya kwanza, nitawasaka mama zao kwanza. Pili, nitahakikisha nawaumizia watu wao kama wanavyoumiza wapendwa wa wengine ili wajue na kuona inavyouma. Haiwezekani tukakubali kaya yetu igeuke kaya ya maimla, wasanii na wababaishaji wanaochukia wenzao kwa vile wanajua uovu na ushenzi wao. Tunduni hivi kosa lake nini zaidi ya kuzoza ukweli? Nani anaweza kuua ukweli akafanikiwa. Unaweza kuchelewesha ukweli kujulikana; lakini huwezi kuua ukweli. Ukweli ni kama mada, hauawi wala kuumbwa. Ukweli ni ukweli na utabaki kuwa ukweli iwe ni kwa shari au kwa heri.
            Inashangaza kusema kuwa kuna wahalifu wasiojulikana wakati waliomuonyesha cha moto Nape Mapepe wanajulikana; sema ndata waliogopa kuwakamata kutokana na kutojua nani aliwatuma kutaka kutenda unyama ule.  Walisahau kuwa wale waliomwonyesha cha moto Mapepe wanaunganishwa na yule aliyekuwa akitaka kushuhgulikia jinai yake na yule aliyempuga haraka haraka ili asiweze kumuumbua mshenzi mwenzake. Sasa mimi nasema. Hawa wajalaana wanajulikana na sababu ya kutenda jinai bila kukamatwa zinajulikana. Mbona watu wasiojulikana waliosumbua walevi wa Rufiji walijulikana na kufutiliwa mbali?  Hivi unataka kuniambia hawa jamaa wangekuwa wanatishia maisha ya wenye kaya wangeendelea kutojulikana kweli?
            Hivi waliowateka akina Dk Steve Ulimboka, Absalom Kibanda, Romania Mkatoliki, na wakampoteza Ben Saanane eti bado hawajulikani kweli? Hivi waliomwagia shaba Tunduni hawajulikani kweli? Hivi waliolipua ofisi za wakili anamofanyia kazi wakili wa Tunduni kweli hawajulikani? Kweli waliompoteza Ben Saanane hawajulikani kweli?  Hawa watu wasiojulikana wana lisirikali ndani ya lisirikali au ni siri kali ya lisirikali?  Yaani ndata wetu na uzoefu wao wamezidiwa ujanja na watu tena wachache wasiojulikana au kuna namna kama si nkono wa ntu?
             Kwanini hawa wasiojulikana wanapambana na wale wanaoonekana kuwa mwiba kwa wenye ulaji wanaoonza kuugeuza urithi? Hivi kweli waliovamia Klauds hawafahamiki an wanaowakingia kifua kwa vile wanatumiana hawajulikani kweli? Basi majini. Basi semeni majini na si watu wasiojulikana wakati wanajulikana. Naona yule anatikisa kichwa. Kama unadhani kawaulize akina Tunduni na wahishimiwa wengine waliowahi kufuatiliwa na ndinga hilo la watu wasiojulikana. Mbona wahishimiwa akiwamo Tunduni walishataarifu ndata kila kitu wasichukue hatua tokana na kuwajua wahusika kuwa hawajulikani na wakijulikana lazima uwaite wasiojulikana wakati wanajulikana.
            Nimalizie kwa kuronga; hawa watu wasiojulikana wanajulikana. Kama hawajulikani kwa walevi, kwa Mungu wanajulikana. Pia, kama umma wa walevi tukiamua wajulikane watajulikana tu. Hivyo, tusitishwe na kivuli cha kutojulikana, wanajulikana na watajulikana japo wapo wanaotaka wasijulikane; ila wajue watajulikana kama wanavyojulikana ingawa twaambwa hawajulikani wakati wanajulikana.
Chanzo: Nipashe J'mosi leo.

No comments: