The Chant of Savant

Tuesday 26 September 2017

Kijiwe chamuunga mkono Dk Kanywaji Magu

Image result for photos of mererani
            Baada ya Kijiwe kurejea toka Nairoberry kumuona Tunduni Lissu ambaye kwa sasa, si haba na alhamdullillahi, anaendelea vizuri, kilifarijika kusikia kuwa lisirikali limeamka usingizini na kuamua kuweka uzio kwenye machimbo ya bongonite kule Mererani.  Pia kijiwe kilifarijika kusikia kuwa lisirikali lina mpango wa kuntibia Tunduni; hata kama ni kwa kusuasua na kuchelewa baada ya kupima upepo wa walalahoi na kugundua wanampenda na kumuona kama shujaa wao baada ya Chris Mtikisa (RIP).
            Mpemba anaingia akiwa na bashasha tofauti na wiki zilizopita alipokuwa akiingia akiwa amenuna na kukasirika tokana na mwanakijwe mwenzetu kumiminiwa mvua ya shaba. Anaamkua na kuoda kahawa yake na kulianzisha “yakhe mwasemaje kuhusiana na hii amri ya kujenga uzio kuzungushia machimbo ya bongonite kule Nrerani?”
            Kabla ya kuendelea Kanji anamkosoa na kusema “veve Pemba kwanini naharibu Swahili kama hindi? Kule naitwa Rerani siyo Nrerani.” Kijiwe hakina mbavu kwa namna anayemkosoa mwenzake anavyokosea tena zaidi.
            Mbwamwitu anaamkua kumkosoa Kanji “duh! Hii kweli kali. Sasa Kanji unachokosoa nini kama nawe unarudia makosa tena zaidi? Nadhani kule kwaitwa Mererani na Rerani. Hiyo Rerani nadhani iko Bobei lakini si Daganyika dugu yangu.”
            Mpemba akiwa anatabasamu anarejea “hakuna alokosea baina yangu na Kanji hasa ikizingatiwa kuwa kila ntu ana lafudhi ya kwao. Mie ndhani sasa tujadili hili la kulinda utajiri na raslimali za taifa badala ya raslimali za lugha na matanshi yake. Basi mie nshauri tudurusu hii amri alotoa rahis ya kuzungushia wigo maeneo yenye madini yetu.”
            Msomi aliyekuwa akisoma jarida moja kubwa la kigeni anaamua kula mic mapema ili kuokoa mjadala usirejeshwe kwenye utani. Anakwea mic “Mpemba una hoja hapa. Ni kitendo cha maana kuzugushia wigo kwenye eneo la Mererani. Hata hivyo, nina angalizo. Je hili ni jibu? Mbona bandari imezungushiwa wigo na mipaka imejaa mageti lakini mali zetu zinapitishwa na taifa linakula hasara? Nadhani badala ya kujengwa wigo kwenye machimbo ambalo ni jambo safi, tungeanza kujenga wigo kwenye vichwa na mioyo ya watumishi wanaoajiriwa kwenye maeneo nyeti kama haya.”
            Kabla ya kuendelea Kapende anamchomekea “duh! Msomi kweli wewe si wa kawaida! Wachovu wengi waliposikia wigo walisherehekea kiasi cha kupofuka wasijue kuna mianya mingine mawe yanaweza kuibiwa.”
            Kabla ya kuendelea Msomi anampoka mic na kuendelea kudema “ni kweli usemayo. Kawaida wengi huwa na kupelekwa na matukio kiasi cha kushindwa kuyaongoza. Sina ugomvi na ujenzi wa wigo ingawa utatumia fedha nyingi ambayo kama tungekuwa na mifumo ya kupambana na wanaotuibia huenda zingetumika vinginevyo kama vile kuweka mitambo isiyochezewa ya kielektroniki au kuongeza magereza ya kuwafunga wanaotuibia. Nadhani tungetunga sheria kali dhidi ya wezi wa namna hii na kuunda mfumo usiochezewa, ingekuwa bora kuliko nyigo hizi.”
            Mijjinga napoka mic na kuronga ‘usemayo Msomi ni ukweli mtupu tena ya maana. Hata mimi nadhani, tungewekeza kwenye usalama kwa kuwaangalia watendaji wetu wa kwenye maeneo ya madini, viwanja vya ndege na mipakani. Tutatejenga ukuta kuzuia wezi. Je tumeimarisha ulinzi kwenye mipaka yetu kupambana na utoroshaji wa madini na uingiaji na utokaji wa hovyo wa wakimbizi wa kiuchumi?”
            Kabla ya kuendelea, Mgoshi Machungi anakula mic “Mijjinga nakubaiana nawe sawa na Msomi. Hatiwezi kutegemea kuta kia sehemu. Hemu fikiia. Kama twiga waisafiishwa mchana tena kupitia airport na si uchochoo wa mpaka, huu wigo kwei utawazuia wanaotiibia mawe yetu? Kwanini tisitunge sheia ya kuwanyonga watakaopatikana na kuiba mawe yetu ii wanaopanga kufanya hivyo waogope au wajue kinachowangoja?”
Da Sofia Lion aka Kanungembe anakula mic “kaka Mgoshi umenikuna kweli kweli.” Kabla ya kuendelea Mchunguliaji anamchomekea Sofi “dada utani huu mbaya. Eti amekukuna? Amekukuna wapi na vipi ili tujue?”
            Sofia naye hamkawizi anajibu “unataka ujue ili iweje. Ili akukuna nawe siyo kaka yangu?”
            Kabla ya kuendelea Mchunguliaji anachomekea haraka “Da Sofi tuheshimiane tafadhali.”
            Sofia anajibu “kweli dawa ya moto moto. Hivyo ndiyo ninavyokuheshimu kulingana na namna ulivyotumia hilo neno lako na kulielewa visivyo.”
Kabla ya kuendelea Mipawa anaamua kuokoa jahazi. Anazoza “jaman utani tuache kwenye mada serious kama hii hata kama tunahitaji kutaniana basi tuvumiliane au siyo jamanini? Ingekuwa bora kumpa fursa dada Sofia naye aelezee anachodhani kifanyike kuboresha ulinzi wa mawe yetu au siyo?”
            Sofia anakamua mic “kaka umenena. Huyu kazoea vya kunyonga vya kuchinja haviwezi na isitoshe mkuki kwa nguruwe. Hayo tuyaache. Mie nadhani sirikali iongeze bidii katika kudhibiti utajiri na vipato vya wafanyakazi wake. Tumeishapiga kelele tukitaka irejeshwe sheria ya maadili ambapo kila mwanakaya anapaswa kujaza fomu ya mapato yake kila mwaka. Baada ya hapo lazima turejesha mfumo wa kupelelezana na kuripotiana. Nadhani hili ni muarobaini kuliko wigo wa mabilioni. Je hao wanageshi tunaowaweka siyo waja wenye udhaifu wa vishawishi au tunajeshisha kaya?”
            Kabla ya kujiwe kuendelea si tawi la mti likakatika tukatawanyika bila kumaliza mada!
Chanzo: Tanzania Daima J'tano leo.

No comments: