The Chant of Savant

Sunday 10 September 2017

Barua ya wazi kwa maaskofu Kilaini na Nzigilwa

Image result for photos of kilaini na nzigilwa
          Wahashamu maaskofu Methodius Kilaini na Eusebius Nzigilwa,
            Kwanza, nawaamkua shikamooni; na kukwapa pole kwa majukumu yetu ya kiroho na kidunia. Pia nawapa pole kwa yaliyowakuta. Maana si madogo. Ni pale mlipotuhumiwa, kabla ya kukiri, kuchotewa fedha zilizotokana na kashfa ya wizi wa fedha za umma wa watanzania maskini ijulikanayo kama Escrow mlizopewa na mtuhumiwa na muasisi mkuu wa kashfa hii, James Rugemalira ambaye sasa yuko korokoroni akituhumiwa kwa makosa ya kulihujumu taifa na kuuibia umma. Hivyo, sitaweza kuingi undani wa suala zima tokana na sababu za kisheria na ukweli kuwa mnalijua vizuri hata kuliko mimi kama wanufaika ambao sasa wanajitenga na mshitili wao.
            Hivi karibuni, nilisoma tangazo lenu la tarehe 7 Septemba, 2017 kuutaarifu umma kuwa mmeamua kurejesha zile fedha kwa serikali baada ya kujiridhisha kuwa hazikupatikana kihalali. Je mmetubia dhambi hii itokanayo na uroho ambayo ni kinyume cha mafundisho ya Yesu Kristo? Je mmetumia vigezo gani hasa ikizingatiwa kuwa atoaye sadaka kanisani au matoleo, kama manavyoita, huwa haulizwi namna alivyochuma fedha atoazo? Maana ingekuwa hivyo, bila shaka mngelimuuliza Rugemalira alivytengeneza hiyo fedha kabla ya kuzichukua na kuishia kwenye kashfa ambao itawagharimu vilivyo kama mkondo wa sheria utafuata ikizingatiwa nyinyi ni viongozi na watumishi wa umma waliopokea fedha chafu zitokanazo na wizi wa fedha za umma. Je huu si ushahidi tosha kuwa hii fedha haikuwa ya kanisa bali yenu kutokana na kitendo mlichofanya mkidhani kitawasafisha kikaishia kuwafichua na kuwachafua zaidi?  Katika tangazo tajwa hapo juu, mnakiri kupokea fedha ambazo hamkutaja ni kiasi gani ingawa inafahamika ni shiling milioni 40 na ushei, hapo Februari 2014 kupitia kwenye akaunti zenu za benki.  Hii maana yake ni kwamba fedha tajwa ilikuwa benki kwa takriban miaka mitatu ikitengeneza faida. Je mmerejesha na interests zilizolipwa na benki tokana na kuwa na kiasi hiki kikubwa? Je tukiacha ubabaishaji na kujitetea, kweli kwenye nafsi zenu hamkujua kuwa fedha hii ilikuwa kubwa; na uwezekano wa mhusika kuipata visivyo halali ulikuwa mkubwa ikizingatiwa kuwa kashfa yake haikuanza jana wala juzi? Je mnategemea kufanikisha nini katika hatua hii ambayo kisheria ni ushahidi wa wazi unaoweza kutumika dhidi yenu? Je kwanini mlingoja mpaka Rugemalira akamatwe? Je angeendelea kunyamaziwa mngechukua hatua mlizochukua au ni baada ya kugundua kuwa mambo sasa si mchezo wala mazoea kama ilivyokuwa imezoeleka nchini ambapo mafisadi wakubwa walizoea kulindwa na kuengwaengwa huku wakiwakoga wale waliowaibia? Kuna haja ya kutubu na kujisuta sana huku mkisema ukweli ili mueleweke na ikibidi kusamehewa au kuhukumiwa kulingana na wenye fedha watakavyoamua.
            Wapendwa, naomba niendelee kuwadodosa lau ukweli ujulikane ili uwaweke huru.  Katika tangazo lenu mlidai kuwa fedha husika ilikuwa ni matoleo.Je kama kweli yalikuwa ni matoleo, kwanini yaliingizwa kwenye akaunti zenu na si kwenye akaunti za makanisa yenu? Hapa nani anasema ukweli; na utaratibu wa kupokea matoleo ni upi kwa mujibu wa kanuni za kanisa? Je kwanini mmeamua kurejesha fedha serikalini na si kwa yule aliyewapa au familia yake wakati mkijua serikali aihusiki kwenye kashfa hii? Je mlipata ushauri wa kisheria ua wa kidini katika kufikia hatua hii hatari. Kwani, kiushahidi wa mazingira, hamna tofauti na wanufaika wengine waliohongwa tokana na nafasi zao katika utumishi wa umma ambao nanyi, kama watumishi wa kiroho, mnahusika? Je kitendo chenu cha kupokea fedha chafu kwenye akaunti binafsi kinatoa funzo na picha gani kwa jamii yetu? Je mnadhani mlichofanya ni suluhu ya sakati hili linalopaswa kuisha kisheria?
            Wapendwa, japo sitaki niseme mengi wala kuhukumu ili nisihukumiwe, tangazo lenu limeficha mengi zaidi ya liliyoweka wazi. Kwa mfano, kwanini hamkueleza utaratibu unaojulikana kikanisa wa muumini kutoa matoleo kwa kanisa ili umma upime kama kilichofanyika ni sawa au si sawa? Je kwanini mmechukua muda mrefu kufikia uamuzi mliofikia? Lazima kuwe na sababu zaidi ya mhusika kuwa korokoroni. Je mlifanya jitihada za kumrejeshea aliyewapa hiyo fedha kabla ya kufikia kuzipeleka serikali au mnafanya hivyo, ili serikali na umma usiwashughulikie?
            Nimalizie kwa kusema kuwa kitendo chenu kinaacha maswali mengi kuliko majibu. Sidhani kama serikali itaona sincerity kwenye kitendo hiki zaidi ya kuwa mbinu ya kutaka kuepukana na matokeo ya kashfa hii ambayo ni kufikishwa mbele ya vyombo vya dola ili haki itendeke. Maana, hali tuliyo nayo nchini kwenye ufisadi inatisha na kukatisha tamaa ingawa rais anajitahidi kupunguza madhara na ukubwa wa tatizo ambalo watangulizi wake walililea na kulifumbia macho. Si viongozi wa serikali wala wa kiroho japo si wote, imewaozesha na kuwaharibu kiasi cha kusahau hadhi, heshima na wajibu wao kwa umma. Ushauri wangu wa bure kwenu ni kwamba kirini kukwa mlipotoka na muombe msamaha mambo yaishe ili liwe somo kwa wengine wanaodhani kuwa wanaweza kutumia nyadhifa zao kula na mafisadi.
Chanzo: Tanzania Daima J'pili leo.

No comments: