How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Sunday, 17 September 2017

Watu wasiojulikana: Barua ya wazi kwa rais Magufuli

Image result for photos of unkown people
            Ndugu rais John Joseph Pombe Magufuli,      
            Naamini u mzima wa afya na unaendelea na majukumu yako ya ujenzi wa taifa kama raia na rais wa Tanzania. Leo, kwa mara nyingine nimeamua kukuandikia waraka mwingine. Si mara yangu ya kwanza wala ya mwisho kufanya hivyo. Leo naomba kwa taadhima nijielekeze kwenye jinamizi lililokumba taifa letu linalosababishwa na wale wanaojulikana kama watu wasiojulikana. Watu wasiojulikana wameliteka taifa kiasi cha kuanza kuwa na sifa mbaya kimataifa. Swali la kwanza, ningependa kujua, nini msimamo wako kuhusiana na kadhia hii ambayo inaonekana kuwachanganya wananchi tokana na kukosekana tamko rasmi la serikali ukiachia mbali kueleza ni mikakati gani inafanywa kuliangamiza kundi hili la washenzi na wauaji wasiojuliana kabla halijaliangamiza taifa kwa kuamsha chuki na hasira zinazoweza kusababisha vurugu kutokana na hisia kuwa kuna ubaguzi, upendeleo na uonevu?
            Ndugu rais, nadhani, kama raia na rais wa nchi, hii mambo ambayo yameishatendwa na wahalifu hawa yako mezani kwako kama siyo kwenye mitandao na vyombo vyako vya dola. Ajabu ya maajabu, hawa wanaoitwa watu wasiojulikana, kuna baadhi ya watu wanawajua lakini hakuna vyombo vya dola vimefanya jitihada za kutaka kwuajua na kuwaweka wazi baada ya kuwafungia korokoroni.  Kuna wahanga ambao wameishatoa taarifa polisi kuhusiana na watu hawa kuwafuatilia lakini hakuna hatua zilizochukuliwa. Wa kwanza kutoa taarifa hizi ni baadhi ya wabunge waliohisi kuna gari lenye watu wasiojulikana waliokuwa wakiwafuata.  Hapa sijaiongelea watu ambao wameishaumizwa kwa kutekwa na kupatikana baada ya kuteswa. Kinachoshangaza na kustua ni ukweli kuwa  kama wabunge wanafuatiliwa na kutishiwa maisha yao na hakuna anayejali, je hao raia wa kawaida walalahoi  na kajamba nani yakiwakuta hali itakuwaje? Je kwanini tunaruhusu hofu ianze kutawala nchi yetu? Ni kwa nini na kwa faida ya nani?
            Ndugu rais, waheshimiwa wabunge waliotoa taarifa kuhusiana na watu wasiojulikana kuwafuatilia walitoa namba za gari lao na hata rangi ya gari. Ajabu ya maajabu, si polisi wala nani alikuwa tayari kuongelea angalau hata kulaani watu hawa wasiojulikana ambao uharifu wao unajulika nchi nzima. Sijui ukimya huu unaisaidiaje serikali? Sijui hata mantiki ya jeshi lenye kila zana, hadi sasa, kushindwa kuwakamata watu tena wachache wasiojulikana. Je ni kweli hawa watu hawajulikani? Kama nchi yenye vyombo vya usalama inaweza kuwa na watu wasiojulikana, hili hakikisho la usalama wetu kama wananchi ni la nini?
            Ndugu rais, kama kiongozi wa nchi, naandika kukutaarifu na kukuomba uchukue hata ili hawa wasiojulikana wasijevuruga nchi na kuufanya uongozi wako uonekane umeshindwa kulinda usalama wa taifa ukiachia mbali kushindwa na genge la wahalifu tena wanaojifanya hawajulikani wakati wanajulikana.
            Pili, umekuwa ukihubiri amani, na upendo nchini ukihimiza utendaji haki bila ubaguzi. Juzi juzi mheshimwa mbunge Tundu Lissu wa CHADEMA alivamiwa na hawa wanaojifanya kutojulikana na kummiminia risasi mchana kweupe. Ajabu ya maajabu, hadi leo, polisi bado wanasuasua. Hatuoni mikakati ya kuwasaka na kuwakamata hawa watu wasiojulikana. Hili llimewashanga na kuwatia shaka na uchungu wengi kuona mwenzao na kiongozi wao anamiminiwa risasi na hakuna anayejali.
            Ndugu rais, wengi tunajiuliza tena kwa mshangao na uchungu: Huku kuwatumikia watanzania bila kujali tofauti zao kuko wapi iwapo inapokuja kwenye kuwakamata akina Lissu, Halima Mdee na Godbless Lema wote wabunge wa upinzani, hatuoni polisi kusuasua. Ajabu ya maajabu na kituko ni kwamba polisi wana muda wa kuwamata watajwa kwa vitu visivyokuwa na kichwa wala miguu lakini wanashindwa kuwasaka watu wasiojulikana. Je hapa kunani? Wapo wanaohoji kama kweli Lissu angekuwa mbunge wa chama tawala, hawa watu wasiojulikana wangefumbiwa macho au kushughulikiwa taratibu kama ilivyo? Wengi wananahoji, huo usawa mbele ya sheria na kupata hifadhi kutoka katika jamii viko wapi au ni maneno ya jukwaani?
            Ndugu rais, yalipotokea mashambulizi na mauaji kule Kibiti, polisi walichakarika kweli kweli na hatimaye kuyakomesha. Je inakuwaje watu wasiojulikana wanaendelea kuchezea nchi kana kwamba wana serikali yao ndani ya serikali wakati watanzania wanajua kuna serikali mbili tu ya Magufuli na ya Zanzibar?
            Ndugu rais, sitaki niseme mengi. Ninachojua ni kwamba mataifa yaliyoishia kwenye machafuko yalianzia huku tuliko. Haiwezekani watu wasiojulikana, iwe ni kwa kutumwa, kujituma au kujipendekeza waendelee kuonea watu wasio na hatia umma unyamaze. Lazima umma utataka kuwajua na kuwatia adabu kama mamlaka zitaonyesha kushindwa kufanya hivi.  Nisingependa taia letu lifike kule kana kwamba lina ombwe la uongozi. Hawa wahuni na mabwana zao wanapaswa kusakwa na kuteketezwa haraka kabla hawajakuchafulia jina. Tuondoe taifa letu mikononi mwa wahalifu wanaojificha nyuma ya kutojulikana. Tuepusha ukatili na mauaji vinavyoanza kuathiri sifa nzuri ya taifa letu ukiachia mbali kutishia mustakabali na usalama wa taifa.  Watanzania wanangoja tamko, uongozi wako na suluhu juu ya kadhia hii itokanayo na ukatili, ushamba na upumbavu wa wote walioko nyuma ya ujambazi huu.
Kila la heri.
Nkwazi Mhango
Chanzo: Tanzania Daima J'pili leo.

No comments: