Heko Rais Magufuli

Sunday, 24 September 2017

Somo toka shambulizi dhidi ya Lissu


            Kwa wenye busara kila tukio ni darasa. Tukio la kinyama na kishenzi dhidi ya rais wa Chama cha Wanasheria Tanzania (TLS) na mbunge wa Singida Mashariki Mheshimiwa Tundu Lissu, kadhalika, nalo lina somo kwa Tanzania kama taifa na jamii ya watu. Katika makala ya leo, safu hii itadurusu masomo tunayoweza kupata tokana na kitendo hiki cha kipuuzi na kipumbavu.
            Kwanza, hata kama ni kwa kusuasua na kuchelewa, tunapongeza azma na tamko la serikali la hivi karibuni kuwa itamtibia Lissu popote pale duniani kama yatatafsiriwa kwa vitendo. Hata hivyo, umma unahoji, kwanini serikali imechukua muda mrefu kufikia hatua hii muhimu kana kwamba Lissu si mtanzania na kiongozi.  Japo inaweza kuwa si kweli au kweli, wapo wanaoona kama kuwa kuna upendeleo katika kuhudumia viongozi wetu. Wanadhani; kama Lissu angekuwa mbunge wa upande mwingine, huenda serikali isingechukua muda mrefu kufikia msimamo huu mpya. Hata hivyo, tunaipongeza; na kuishauri, ijifunze kutokana na udhaifu huu. Maana, leo ni kwa Lissu. Kesho hatujui litamtokea nani. Tunasema haya kutokana na uzoefu kuonyesha kuwa kuna viongozi wengi ambao wameishatibiwa nje tena kwa haraka na wakiwa hawako kwenye hali ya kutisha kama aliyokuwa nayo Lissu kabla ya kukimbizwa Nairobi anakoendelea na matibabu.
            Pili, tukio hili limechafua sifa ya Tanzania ya kuwa taifa la amani, sifa ambayo tumeijenga kwa gharama kubwa na kwa muda mrefu lakini sasa inaondolewa na wapuuzi na wahalifu wachache.  Tumechafuka mbele ya mataifa. Kitendo hiki cha kinyama kimelaaniwa dunia nzima kiasi cha jumuia ya kimataifa kuanza kuiangalia Tanzania kwa macho tofauti na ilivyokuwa. Gharama ya unyama huu kwa taifa si ndogo. Kwani, wenzetu sasa wanatuona kama taifa lisilo na amani wala usalama; jambo ambalo lina athari zake kijamiim, kisiasa na kiuchumi. Sijui kama kuna mtu nwenye fedha zake na akili zake atataka kuwekeza kwenye taifa ambalo watu wake na viongozi wake hawako salama.
            Tatu, tukiachia mbali mateso na mahangaiko anayopitia Lissu na familia yake,  kitendo hiki kimehujumu jimbo lake na taifa hasa ikizingatiwa kuwa Lissu ni mwakilishi wa jimbo na kiongozi mkubwa wa kisiasa na kisheria nchini.
            Nne, tukio hili limeonyesha udhaifu wa polisi wetu. Rejea ukweli kuwa Lissu alitoa ripoti si mara moja wala mbili kuwa alikuwa akifuatiliwa na watu ambao walikuwa wakitishia uhai na usalama wake. Kuonyesha ukweli wa madai ya Lissu, polisi waliyapuuzia hadi lilipotukia shambulizi. Hali hii inaondoa imani ya umma kwa jeshi lao la polisi jambo ambalo si jema. Kwa wenye kufanya maamuzi ya haraka, wanaona kama linashiriki au kubariki jinai hii.
            Tano, ukiliangalia shambulizi dhidi ya Lissu kiuchumi, unagundua kuwa hawa wauaji wamelisababishia taifa hasara kijamii, kisiasa hata kiuchumi. Mfano, tujiulize, fedha ambayo imeishatumika kumtibia Lissu ingetumika kujenga vyumba vya madarasa au kununua dawa kwenye zahanati zetu zisizo na madawa ingejenga au kunuua dawa kiasi gani?
            Sita, ukiangalia kadhia hii kwa Lissu na familia yake, ni muda na fedha kiasi gani wameishatumia ukiachia mbali kukwamisha maisha na shughuli zao za kawaida. Hapa hatujagusia mateso ya kisaikolojia familia inapitia bila kusahau maumivu na mateso anayokabiliana nayo mgonjwa. Lissu ni binadamu lakini si wa kawaida. Mchango wake kwa taifa na familia yake ni mkubwa tu. Kama baba, ni kiasi gani watoto na mkewe wanateseka ukiachia mbali ndugu na jamaa wanaomtegemea? Kama mbunge, ni huduma kiasi gani jimbo lake linakosa hasa kipindi hiki cha bunge? Kama wakili, ni watu wangapi wanakosa huduma yake? Kama mkereketwa, taifa linapata hasara kiasi gani kwa kukosa ushauri na mawazo yake kama mbunge na mtaalamu wa sheria? Kimsingi, hasara ni nyingi na kubwa kuliko tunavyoweza kufikiria.
            Saba, kama taifa, kitendo cha kinyama alichofanyiwa Lissu kinapaswa kutuzindua toka kwenye usingizi na ulevi wa amani tulivyokuwa navyo kwa muda mrefu. Kwani, hadi sasa, hatujui nani walifanya unyama huu na kwanini. Hivyo, basi, kama taifa, tunapaswa kuwasaka hawa wauaji na kuwashughulikia kwa mujibu wa sheria ili kurejesha imani mbele ya mataifa na watu wetu. Kwa hali ilivyo, na kutokana na mambo yanayofanywa na serikali ya rais John Magufuli ambayo, bila shaka, ina maadui wengi, hasa wale ambao ulaji wao umeingiliwa, kuna uwezekano kitendo hiki kikafanywa na maadui wa taifa ili kuichonganisha serikali na watu wake ukiachia mbali kuichafua kimataifa. Hivyo, nyavu za kutafuta wahalifu hawa zinapaswa kuwa pana sana. Ukiachia mbali maadui wa serikali, pia wapo watu wanaopenda kujipendekeza wanaoweza kufanya kitendo hiki kwa vile wanamuona Lissu kama adui wa serikali. Rejea kilichotokea hivi karibuni ambapo gazeti fulani lilifungiwa kwa miaka miwili kutokana na kutumia maneno ya rais kuelezea kilichotokea. Je waliochukua hatua hii waliangalia upande wa pili na athari za hatua zao?
            Tumalizie kwa kusema tu; shambulizi dhidi ya Lissu ni somo tosha kwa jamii, nchi na watu wenye kufikiri sawasawa hasa kama tutaangalia upande wa pili wa madhara kuliko malengo ya wauaji hawa. Hatutaki kunyosha vidole. Ila serikali isikwepe kuwajibika kutokana na ukweli kuwa jeshi la polisi lilizembea kwenye wajibu wake mkubwa wa kulinda watanzania na mali zao. Tunamtakia Lissu apone haraka; na taifa lijifunze tokana na kilichomsibu.
Chanzo: Tanzania Daima J'pili leo. 

No comments: