The Chant of Savant

Tuesday 5 September 2017

Kijiwe champongeza pilato mkuu wa Kenya

       Image result for photos of david maraga    Baada ya mahakama kuu ya Kenya kumpiga kalamu rais Uhuru Kenyatta, Kijiwe kimempongeza jaji mkuu wa kaya hiyo Davie Maraga aliyesimama kidete kulinda maslahi ya umma.
            Msomi Mkatatamaa aliyekuwako kule kama mwangalizi wa kijiwe wa uchakachuaji ule anaingia akiwa na furaha ya kufa mtu. Anaamkua na kuagiza kahawa na kusema “si niliwambia kuwa Uhuuto utapigwa chini kwenye mahakama ya haki! Mmesikia rafiki yangu na mwanafunzi wangu Davie Maraga alivyofanya kweli kuonyesha alivyoelewa somo langu la jurisprudential supremacy and sancrosanctity of the constitution?”
            Mzee Maneno anamchomekea “hiyo sankaramantiki ni mnyama gani Msomi mbona unaniacha Solemba ndugu yangu?” Kijiwe hakina mbavu namna anavyoharibu maneno ya kitasha tokana na kutopiga buku babu huyu wa kiramizi.
            Kapende anaamua kumpoka mic mzee Maneno “nadhani Msomi anamaanisha ukuu na utukufu wa sheria ambao, bila shaka, ndio uliwawezesha majaji kutoogopa cheo cha mtu wala njuluku zake na kuamua kutenda haki kwa kusema wazi kuwa kulikuwa na uchakachuaji kwenye uchakachuaji uliopita wa Kenya. Natamani hii ingekuwa hapa kwenye kaya yetu. Nichukue fursa hii kuwapongeza majaji hawa hasa kiongozi wao jaji mkuu Davie Maraga ambaye ni shemeji yangu.”
            Mpemba anakwanyua mic “yakhe waliozea vya kunyonga; vya kuchinja hawaviwezi ati! Kweli mie nilishangaa sana kusikia eti hawa jirani walikuwa wamenchagua mwana wa mtesi wao anosifia kwa unyakuzi wa mashamba na ulimbikizaji wa mali huku akiwaacha hai lakini hoi. Nshangaa na kusikitika sana. Heri majaji wametenda haq. Wallahi nasema, nasi twataka haki kama hii. Ingekuwa yawezekana, kwa vile kaya yetu haina jaji mkuu, ningemualika jaji Maraga aje huku lau tupate katiba mpya ati.”
            “Sasa wewe unatafuta matatizo. Hukusikia wapingaji walivyopiga kelele hadi makoo yakakauka ukiachia wengine kutiwa misukosuko? Hata hivyo, kama Kenya iliondokana na imla kama Dan arap Mwai, nasi kuna siku tutauzika uimla kama walivyofanya bila hata kurusha ngumi. Naamini dunia inabadilika kila uchao ingawa wanene wetu hawataki kuliona na kulikubali hili” anachomekea Mijjinga huku akifunua ukurasa wa tabu kubwa analosoma kuhusu utawala wa kidemokrasia na haki” anachomekea Mipawa.
            Mgoshi Machungi aliyekuwa kimya anaamua kula mic “jamani, kwanza tieeze wazi. Mimi niifuahi kusikia habai hizi toka Kenya. Mpaka sasa sieewi ogic wakenya wanayotumia kuchagua mwana wa mfame kama aivosema ami wakati aiwazuumu ardhi na mai kiasi cha kuacha famiia yake ikiwa ya mabiionea! Tikiejea hapa kayani, naona wakati umefika wa kudai katiba mpya bia kupepesa jicho waa kumung’unya maneno. Maana ukiangaia uchakachuaji wetu unaofanyika kia mwaka, unatamani tingekuwa na katiba mpya angaau tufanye mambo mapya kama waivofanya Kenya.”
            Mheshimiwa Bwege anaamua kutia guu mapema. Anakula mic “huwa nashangaa wanaotaka mambo yetu yawe kama Kenya. Wenzenu, tokana na kuminywa sana na ubepari tangu kupata uhuru walitia akili. Wako tayari kulianzisha wakati wowote wanapohisi mambo sivyo ndivyo tofauti nasi tunaotaka kila kitu kiletwe kwenye sahani. Watawala si watu wa kujadiliana. Ni kama nyuki. Bila moto asali haitoki mzingani. Lau nyuki asali ni yao. Mfano rahisi ni kwamba maziwa huwa ni yako kabla hujampa paka. Je unafanya nini kumnyang’anya paka maziwa? Lazima uwe tayari kuparuriwa na iwe zake ama zako au vipi.”
            Da Sofia Lion aka Kanungaembe anakula mic “hapa kaka umenikuna kweli kweli.”
            Kabla ya kuendelea Mchunguliaji anamchomekea da Sofia” amekukuna wapi na vipi; mbona sijakupata vizuri dada?”
            Mheshimwa Bwege hangoji Sofia ajitetee. Maana ameguswa yeye; na isitoshe ameguswa yeye. Anajibu ‘nimemkuna hapo hapo na hivyo hivyo unavyotaka au vipi? Kwani mawazo yangu hayajakukuna hata wewe ndugu yangu!” Mchunguliaji anaamua yaishe kwe mkwara. Anasema ‘tuheshimiane mheshimwa Bwege. Naye mheshimiwa Bwege anajibu “tuheshimiane basi.”
            Kanji naye kapata upenyo. Anakwida mic “vatu iko sema witu wingi bila angalia sababu na singi yake. Leo nasifia Kenia. Hii vatu ya Kenia iko na katiba safi sana. Sasa hii nataka mambo ive kama Kenia na katiba laka kweli nafikiri zuri dugu yanguni? Kama nataka kvenda binguni na pepo lazima ikufe.” Kijiwe hakina mbavu namna Kanji anavyobukanya uswa ingawa wengi huwa wanajifanya hawaujui wakati wanaujua fika kuliko hata waswa wenyewe.
             Baada ya kusikiliza hoja za wote, Msomi anaamua kutia guu uwanjani lau afunge mjadala kabla kijiwe hakijavurugwa na mambo ya mtaani. Anasema “ni kweli tunahitaji katiba mpya. Ila hatuwezi kuipata kwenye sahani ya dhahabu. Kama alivyosema vizuri Kanji, hatuwezi kwenda peponi, kama ipo, bila kufa. Nakubaliana na mheshimiwa Bwege kuwa bila moto asali haitoki. Hivyo, nashauri tujipange. Muhimu kuliko yote, nampongeza mwanafunzi wangu jaji Maraga kwa ujasiri na heshima yake kwa kaya yake. Wiki ijayo lazima nitie timu kijijini Bonyamatuta kumpa tafu huyu Mura Kikiohoya.
            Kijiwe kikiwa ndiyo kinachanganya si ikapigwa kelele ya mwizi! Acha kila mmoja atoke mkuku kwenda kushuhudia kibaka anavyochomwa moto wakati mibaka ikienziwa.
Chanzo: Tanzania Daima J'tano kesho.

No comments: