The Chant of Savant

Saturday 10 July 2021

Tathmini ya Siku 100 za Rais Samia Madarakani


Japo wengi wameishaandika tathmini zao juu ya maadhimisho ya siku 100 tangu rais Samia Suluhu Hassan abebeshwe zigo zito baada ya kufariki kwa yule aliyekaririwa akimuita ‘Bonge la Kaka’ Hayati Dkt John Pombe Magufuli aliyekuwa rais wa awamu ya tano. Mengi yamesemwa hasa kwa uzuri. Na bado yatasemwa kulingana na namna rais anavyochapa kazi.

            Kwa vile mengi yameishaandikwa, sitayarudia zaidi ya kumtia shime ashikilie hapo hapo ili mambo yaende kama yalivyotarajiwa. Nikaingalia uzoefu wa makamu wa rais waliochukua nyadhifa baada ya vifo vya marais wao, ndani ya siku mia wengi walishaonyesha wasivyoyahimili madaraka jambo ambalo ni tofauti kwa rais Samia hasa ikizingatiwa kuwa mtu aliyevaa viatu vyake, hakuwa kiongozi wa kawaida. Hivyo, utendaji wake si haba, kama alivyosema mzee Ali Hassan Mwinyi, kama ni muziki unasema once more. Nchi jirani za Malawi, 2012 na Zambia, 2009 zinaweza kukupa picha ya namna makamu wa rais walipoapishwa na namna walivyoanza kwa kulaumiwa tena ndani ya siku mia. Joyce Banda, alilaumiwa kwa kuanza kujilimbikizia mali na kushindwa kutaja mali zake hata kutopambana na ufisadi huku baadhi ya watu wake wakijifanyia watakavyo. Kitu kingine alicholaumiwa kwacho ni ukosefu wa usalama. Majambazi na waovu wengine siku zote hupenda kutumia kubadili utawala kama fursa ya kutenda jinai zao. Nako Zambia Rupiah Banda alistumiwa kwa mfumko wa bei ambao ndani ya siku 100 za uongozi wake ulikuwa 20.5% ikilinganishwa na asilimia tano nukta tisa kabla ya kuingia madarakani. Pia Banda wa Zambia, sawa na mwenzake wa Malawi, alituhumiwa kulegea kwenye kupambanana ufisadi.

            Alipoapishwa kukalia kiti cha urais, wengi walitia shaka tokana na mambo makubwa mawili yaani jinsi yake na sifa za yule aliyemrithi. Hata hivyo, kwa siku hizi 100 rais ameweza kuwaondoa wasi wasi waliokuwa na shaka naye. Kwanza, ameonyesha kujiamini katika kila anachofanya. Rejea alivyoweza kuwaondosha baadhi ya watendaji waliokuwa wameteuliwa na mtangulizi wake ili kuunda timu yake anayoiamini. Mbali na kujiamini, rais ameonyesha umakini wa hali ya juu katika kujadili na kutolea majibu baadhi ya matatizo au maswali anayoulizwa na vyombo vya habari. Cha mno, rais ameweza kuendeleza jitihada za mtangulizi wake za kuwaunganisha watanzania kupitia kutenga fursa ya kukutana na baadhi ya makundi ya wananchi ili kuweza kuongea nao na kuwasikiliza.

            Pia rais, ndani ya siku 100, ameonyesha kiasi kikubwa cha ukweli. Mbali na kuja na kauli mbiu mpya–––ambayo, hata hivyo, si tofauti sana na ya mtangulizi wake–––rais ameonyesha kutoyumba hasa kwenye mambo muhimu ya kitaifa kama vile ujenzi wa miundombinu wezeshi na ya kimkakati. Mfano, juzi tumesikia kuwa hivi karibuni serikali itasaini mikataba ya kuongeza ndege tano zaidi kwenye idadi ya zile ambazo tumeishanunua. Pia ujenzi wa reli ya Standard Gauge unaendelea kama kawaida ukiachia mbali miradi mingine mikubwa kama vile wa daraja la Tanzanite Dar es Salaam, daraja la Busisi, ujenzi wa bwawa la Nyerere, ujenzi wa meli na usambazaji wa umeme vijijini. Wengi walidhani kuwa kifo cha Magufuli kingeathiri miradi hii, ambayo kimsingi, ndiyo iliipaisha Tanzania kiuchumi na kimkakati. Na miradi hii haikuwa jicho la mtangulizi wake bali hata nchi nzima.

            Ukiachia mbali vitu, amani na mshikamano wa kitaifa ambavyo ndiyo tunu ya taifa vimeendelea kama kawaida. Hata hivyo, kuna kipindi ndani ya siku hizi 100, majambazi walijaribu kumbeep rais kwa kuanza kufanya ujambazi hadi kutekwa hata kw abasi. Rais hakukaa kimya wala kuona aibu kulisemea hili. Alilionya jeshi la polisi kuhakikisha kadhia hii au tuseme kutaka kuzenguana na rais kumalizwa mara moja. Na kweli, tangu atoe angalizo hili, mambo yamekuwa shwari. Eneo jingine ambako rais analaumiwa ni pale aliposema wazi kuwa anataka kusimamisha nchi kiuchumi ndiposa aruhusu mikutano ya kisiasa. Alisema kwa “nguvu ya kiuchumi hununua nguvu za kisiasa." Hata hivyo, alisema vyama vinaruhusiwa kufanya mikutano ya ndani ya kisiasa. Hili kidogo lina ukakasi kwa vyama vya upinzani na watetezi wa haki za binadamu. Sambamba na hili, ni ile hali ya rais kutotoa ahadi ya kuandika katiba mpya. Wengi wamemlaumu kwa hili bila kujua kuwa katiba mpya si muarobaini wa matatizo yetu. Kwani ingekuwa hivyo, nchi kama Afrika ya Kusini na Kenya zenye katiba mpya na nzuri sana katika bara la Afrika zisingekuwa na matatizo hata kidogo. Ukiangalia ukabila na ubaguzi wa rangi unaoendelea kwenye nchi husika, utagundua kuwa katiba mpya siyo muarobaini. Nadhani matatizo mengi yanayokumba nchi tajwa hapo juu ni ya kiuchumi. Hivyo, nguvu waliyowekeza kwenye kuandika katiba mpya zingeelekezwa kwenye kujenga uchumi kwa ajili ya raia wote, mambo huenda yangekuwa mazuri kuliko sasa.

            Eneo jingine ambalo rais amefanya vizuri ni lile la uongozi ambapo ameonyesha kuwa anataka kujenga uongozi shirikishi. Katika kufanya hivyo, ameteua wakuu wa mikoa na wilaya toka karibu katika kada zote isipokuwa wazee, walemavu na wakulima. Tungeshauri kukumbuka makundi haya ambayo ameyaacha nje kwenye uteuzi wake. Hata hivyo, kuna habari njema kuwa uteuzi wake umeongeza idadi ya kina mama jambo ambalo linaweza kutuelekeza kwenye kupunguza au kuondoa ukosefu wa ulinganifu katika nafasi za uongozi kijinsia.

            Huwezi kuongelea siku 100 za rais SSH bila kugusia uchumi. Kwa wanaojua hali ilivyo–––kwa mujibu wa taarifa za rais mwenyewe––––nchi ina akiba ya kutosha miezi sita. Pia mfumko wa bei uko kwenye digitali moja ukiachia mbali sarafau yetu kuendelea kuimarika huku uwekezaji ukiongezeka. Hii maana yake ni kwamba uzalishaji umeendelea kupanda hasa baada ya kufanya marekebisho hapa na pale. Sambamba na hili, kuna ombwe kuhusiana na ujenzi wa bandari ya Bagamoyo ambayo hadi sasa taifa halijaelezwa kilichofanya isitiswe na utawala uliopita lakini sasa ionekane big deal. Je nini faida zake kwa taifa? Mbali na hili, kuna kuanza kuachiwa kwa watuhumiwa wa kesi za ufisadi mkubwa nchini. Taifa halijaambiwa mantiki ya kuingia majadiliano na watu walioumiza taifa letu huku wengine wakiachiwa hivi karibuni baada ya mahakama kuwaamuru kulipa fedha kidogo kulinganisha na ile waliyoiba.

            Tumalize kwa kusema kuwa mafanikio ya rais Samia ndani ya siku mia ni makubwa kuliko mapungufu. Muhimu, tunamsihi aendelee kubadili pale panapofaa kama tulivyogusia hapo juu na mengine yanayohitaji kufanya hivyo. Hongera rais SSH kwa kumaliza siku mia kwa mafaniko.

Chanzo: Raia Mwema leo.

 

No comments: