How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Tuesday, 27 July 2021

Barua ya Wazi kwa Rais Samia na Waziri Nchemba

Wapendwa waheshimwa,

Salamu, nianze na mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuzingatia hadhi. Kwanza, kwa hesima na taadhima, nakusalimu wa Jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Pili, nakupongeza kwa kuendelea kuliongoza taifa letu baada ya kupoteza bonge la kaka, Hayati Dk John Pombe Magufuli ambaye wengi wameanza kumsahau na wengine kumsaliti. Tatu, naandika rasmi kukuomba ufanye kweli na maamuzi magumu na haraka bila kupepesa kwa kujitua mzigo ambao–––huko mbele ya safari­­­   utakukwamisha–––kama utaamua kuuvumilia kwa hasara yako baadaye. Mzigo huu si mwingine bali waziri wako wa sasa wa fedha Mwigulu Nchemba. Kwanza, niseme wazi, binafsi simjui huyu bwana. Pili, sina chuki naye. Tatu, sina maslahi yeyote na nitakayosema na juu ya ushauri wa kuomba umwachishe ngazi mara moja. Na nne, nayaandika haya kwa roho safi kabisa.

            Mama Rais, ndani ya muda mfupi, huu ni ujumbe wa pili mtawalia kwa waziri wako ambaye nilimshauri asikupotezee muda wala kukutwisha mzigo wa uzembe wake bali aachie ngazi kabla hujalazimika kumuamuru afanye hivyo.  Juzi juzi alibuni tozo za hovyo almaarufu tozo la miamala ya simu. Kusema ule ukweli, jambo hili limekuwa la kwanza kuonyesha hasira za umma dhidi ya utawala wako bila sababu yoyote ya msingi kama waziri angekuwa muadilifu, mbunifu, mweledi na realistic (sina Kiswahili chake). Kwani, mbunge mmoja mbinafsi alipopendekeza kodi ya uzalendo wakati yeye hanao na umma ukaikataa wazi wazi, ilimtosha waziri kuachana na upuuzi huu.

            Pili, gazeti hili, wiki jana, lilianika ubinafsi, uchafu na ufisadi wa Nchemba kuhusiana na kumtumia mkewe Neema na washirika zake wengine ambao gazeti liliweka wazi majina yao kumilki kampuni ya kubahatisha jambo ambalo lilimsukuma–––tokana maslahi binafsi na sababu za kifisadi–––kupunguzia makampuni kama lake asilimia tano ya kodi ambazo anataka kuzilipa kwa kuwakomoa maskini wengi wa taifa hili kwa faidi ya mafisadi wachache. Naomba ufuatilie expose hii ili ubaini ukweli zaidi na kuwa na kila sababu ya kuchukua hatua za kumfukuza mhusika haraka na kumfikisha mahakamani. Wakati tukingoja hili, kwanini asiweke kando kupisha uchunguzi kuhusiana na kadhia hii mbichi na inayomuonyesha waziri kama asiye na uzalendo wowote wala udhu wa kuaminiwa fedha za umma.

            Mwisho, mama Rais, najua una mengi yanayokufikia mengine yakiwa umbea na fitina. Ila hili la tuhuma dhidi ya waziri wako lina kila ushahidi wa kumfunga mtu. Sijui kama utaliona tofauti na kujitia doa kwa ajili watu wengine. Ili ufaidike nini? Naomba kama utaona gazeti linapiga chuku au kukomoa, ujikumbushe maneno ya makamu wako aliposema kuwa hatakuwa na subira na panya watakaotuhumiwa kutafuna fedha za umma. Sina wasi wasi hata panya buku hutawavumilia hata kama wako karibu nawe namna gani.

            Kwa waziri Nchemba,

Bwana Lameck, naomba usinielewe vibaya wala kuona kama natia kichumvi. Kwa mtu yeyote anayekubaliana na ukweli na msomi­­­­–––kama kweli wewe ni msomi­­­–––lazima aukubali ukweli haraka kuliko vihiyo wanaotegema miujiza na waganga wasijue hawana msaada. Japo binafsi sikujui wala hunijua, najua wewe ni daktari wa falsafa japo sina uhakika wa namna ulivyopata shahada yako kwani sijawahi kuona andiko lako. Langu ni juu ya namna Tanzania ilivyoweza kuutumia Ujamaa kuua ukabila na namna inavyoweza kutumika kama mfano na nyenzo ya kusaidia nchi zinazokabiliwa na kadhia ya ukabila na vita. Hivyo, ninapohoji kuhusiana na andiko lako, jua siyo kihiyo au msomi uchwara bali nguli mwenye kuandika zaidi ya vitabu 20 vingi vikiwa vya kiada na sura nyingi tu kwenye vitabu vya kiada pia. Hivyo, kama msomi mwenzako––––kama kweli wewe ni msomi mwenzangu–––nashauri ufanye uamuzi wa kisomi. Achia ngazi mara moja hasa ikizingatiwa kuwa tuhuma mbili zinakutupa nje ya ulingo bila utetezi wowote ni kubwa na chafu mno–––vinginevyo itokee miujiza–––japo zama za miujizi zilishapita miaka mingi iliyopita.

            Mbali na tuhuma zinazokukabili, jikumbushe namna Hayati Magufuli alivyowahi kukutumbua ukatubia akakurudisha kwa vile alikuwa ni mtu anayependa watu wanaotubu. Hata hivyo, kwa uoza unaokukabili, ningekushauri na kumshauri Rais wala usipoteze wala asipoteze muda kukupa fursa ya kutubia. Makosa ya kuhujumu uchumi hayana kitubio ukiacha na hili la kuja na tozo la hovyo ambalo nalo linatokana na tuhuma za ufisadi–––hivyo nalo ni la kifisadi. Kwa kilatini yanaitwa sacriligo yaani yasiyo tubiwa wala kusameheka. Pia, uombe Mungu utumuliwe bila kuchunguzwa na kufikishwa mahakamani kama wengine ambao sasa wako wanasaga meno kwa kutumia madaraka vibaya.

            Namshauri Rais aamuru TAKUKURU wachunguze kadhia hii na kukufikisha mbele ya vyombo vya haki ili haki ionekane inatendeka bila kupendelea wala chuki. Iweje wengine waliotuhumiwa wafukuzwe kazi tena toka kwenye ngazi za chini wewe uachiwe? Wakati wa kulindana haupo hasa ikizingatiwa kuwa mheshimwa Rais ana miaka minne tu kuingia kwenye uchaguzi apimwe utendaji wake si kwa sifa bali kura. Niliwahi kumwandikia mheshimwa Rais kujifunza toka kwa Makamu wa Rais wan chi jirani za Malawi na Zambia waliorithi madaraka baada ya mabosi wao kufia madarakani wakashindwa kuchaguliwa tokana na kutumia vipindi vya urithi vibaya muuaji mkubwa akiwa kufumbia macho mafisadi waliokuwa karibu nao. Mama Rais, rejea historia za hao kama kweli unautaka Urais baada ya kumaliza kipindi cha urithi.

            Mwisho, kama nilivyoanza, namaliza kwa kumshauri waziri Mwiguli ajipime na kupima maji na kufanya maamuzi magumu kabla ya Rais hajafanya hivyo. Hii, licha ya kumpa heshima na fursa ya kujitetea, itampa Rais fursa ya kurekebisha makosa kabla hayajamgharimu. Ni ushauri wa bure ila wa thamani.

            Kwa mama Rais, huna haja ya kuumiza kichwa wakati taifa linao nguli wengi bungeni na nje ya bunge wanaoweza kuhudumu vizuri kwenye wizara ya fedha. Isitoshe, ukimtimua Mwigulu, utataoa ujumbe kwa waliobaki na watakaomrithi kuwa wasipotimiza wajibu wao wataonja alichoonja. Pia nashauri waziri huyu asisimamishwe kazi wala kufukuzwa bila kuchunguzwa na kufikishwa mahakamani ili liwe somo kwake na wengine wenye mawazo na tabia kama zake. Kimsingi, hichi ndicho kilichokupandisha chati wewe na mtangulizi wako tokana na utumbuaji usio na simile wala kungoja ngoja. Kazi kwenu. Nawatakia maamuzi magumu mema na ya haraka ili kuzuia madhira yasiwe makubwa kwa wapendwa watu wetu hasa walipa kodi ambao pesa yao inapigwa. Zama za Tanzania kuwa shamba la bibi ziliisha mwaka 2015.

Chanzo: Raia Mwema


No comments: