Pamoja na kujaliwa uwezo mkubwa wa kufikiri, pia binadamu amejaliwa uwezo mkubwa wa kusahau ukiachia mbali tamaa na wakati mwingine ubinafsi na upogo. Leo tutaongelea wabunge ambao wanalalamika kuwa mishahara na marupurupu wanayopata havitoshi. Madai haya ya ajabu kidogo yaliibuliwa hivi karibuni hivi karibuni na mbunge wa Mbogwe (CCM) Nicodemus Maganga aliyekaririwa akisema “nikiwa bado sijaingia humu nilikuwa nafikiri kuna posho za kutosha. Nimeangalia mabunge mengi ya Afrika ya Kusini pamoja na Kenya pamoja na mabunge mengine wanalipa kwa dola.” Kuonyesha kuwa madai na mawazo haya ya ajabu yalikuwa yanawakilisha au kushabikiwa na wabunge wengi kama siyo wote, badala ya kuzomewa au hata kustua wenzake, alipotoa hoja hii alishangiliwa sana na wabunge wenzake kuonyesha kuunga mkono mawazo yake pamoja na uhovyo wake.
Tukianza na kulipa kwa dola, je nasi tulipe kwa dola wakati tuna sarafu yetu ya shilingi ambayo ni alama na hazina ya taifa? Je kweli huyu ni mzalendo au mchumia tumbo ambaye yuko tayari kuitoa sadaka sarafu na alama ya taifa lake ili kujaza tumbo ambalo–––siku zote–––halina kumbukumbu wala shukrani. Je huyu ana jipya la kuchangia kwenye mhimili wa dola wa bunge na wananchi anaodai kuwawakilisha? Je nasi tulipe kama hayo mabunge anayodai ameyaona bila kuangalia uwezo wetu hasa wananchi wetu walipa kodi? Je mbunge wa namna hii–––na wengine kama yeye–––kweli hawakilishi tumbo lake badala ya wananchi ambao inaonekana hawafahamu vizuri kuwa ni maskini wanaokamuliwa kodi kulipia matanuzi yake? Je haya aliyosema Mbunge wa Mbogwe ni mawazo na msimamo wa wana Mbogwe ambao ni maskini sawa na watanzania wengine? Je huyu Mbunge anawafaa au analifaa tumbo lake? Je Mbunge wa namna hii anahitajika katika kipindi hiki cha kupambana na matumizi mabaya ili kuleta maendeleo kwa watanzania?
Kama unavyojua, wabunge ni watanzania. Walikotoka kunajulikana. Wapo waliokuwa walimu, wanuka jasho na wahangaikaji wengine kama wengine.
Tunapolaani ubinafsi, roho mbaya na uroho, hatuko peke yetu. Kwani baada ya Maganga kupayuka kama alivyofanya, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Daniel Chongolo alilaani katendo hiki akisema kuwa“aende kwa hao wanaolipa dola. Kwanini anafanya kazi hapa?” Mbali na kusema haya, Chogolo alijiapiza kuwa mbunge wa namna hii hataendelea kuwa mbunge. Tunaomba asisahau nadhiri hii kwa watanzania.
Ni ajabu wengi wa watu tena ambao walikuwa wamefulia na kupauka leo wamesahau waliowapa kura na madaraka kiasi cha kuamua kutumika tamaa na tumbo lake. Huyu––––kama katiba yetu ingeruhusu–––ilipaswa ashinikizwe aachie ngazi wenye uwezo wachukue na kutumika na kutumikia matumbo yao badala ya wananchi. Kama sikosei Maganga alikuwa mfanyabiashara wa kawaida kabla ya kuukwaa uheshimiwa. Hivyo, sina shaka kuwa biashara yake haikutosha ndiyo maana akaingia kwenye siasa ili kuchuma. Je bado nchi yetu inahitaji wabunge kama hawa kweli?
Kama Katibu Mkuu wa CCM alivyoonyesha na kuonyesha uchungu wake tunataka hata wana CCM wamkane mtu huyu ambaye ameonyesha sura zake halisi. Huyu na yule aliyetaka watanzania wakamuliwe kwenye simu zao ili kupata kodi ya ‘uzalendo’ sitegemei kama watarejea kwenye uchaguzi ujao. Hapa lazima niseme wazi wazi na Mwenyekiti wa CCM na Katibu wa CCM kuwa wahakikishe sura kama hizi zinapotea ili kuepuka kuendelea kuchafua chama na kukipata matope.
Kimsingi, wabunge wa aina hii siyo kuwa wanataka kuwaibia wananchi na kuwatumia kwa faida zao binafsi bali wanawachokoza, kuwatukana, kuwadharau watanzania wanaotaka wawanyonye. Kwa mtu anayejua namna wabunge wetu wanavyolipwa ‘pesa ndefu’ kuliko madaktari, maprofesa na wengine wenye elimu zao haba, watakubaliana nasi kuwa watu hawa hawana kumbukukumbu, shukrani wala hawaoni mbele ukiachia mbali kuwa wanawakilisha matumbo yao. Wakati wao wakitunzwa kama wafalme, watanzania wanaendelea kuhenyeka. Na hili wala haliwahangaishi. Wanataka zaidi. Nirudie ili kuweka msisitizo. Je hawa wanawakilisha wananchi kweli wakati hawajui kuwa hali zao ni mbaya tangu tupate uhuru? Je hawa wanaishi nchi gani? Tutakopa mangapi na toka wapi? Hakika, hawa ni wa kuogopwa kuliko hata corona, ukimwi na ukoma. Kesho watataka walipwe kama wabunge wa marekani au uingereza au falme za kiarabu. Je namna hii tutafika? Inakuwaje mwindaji wa sungura anataka kula saw ana mwindaji wa tembo? Wengine hawakuwa na hata pikipiki sasa wanatembelea mashangingi
Wengine hata hawachangii bungeni.
Leo hatusemi mengi. Tunamshauri Maganga kujitafakari upya. Ima awaombe msamaha watanzania, afute madai haya ya ajabu na hovyo na atubie au aachie ngazi aende huko ziliko dola kama alivyosema Katibu Mkuu wa CCM ambaye tunampongeza kwa busara, ujasiri na ushauri wake mwanana kwa Maganga na wengine wanaofanana naye. Ni ushauri wa bure. Pia hata Mwenyekiti wa Chama rais SSH aangalie namna ya kumwajibisha mbunge huyu wa chama chake ambaye anaonekana kutokuja hata misingi na sera za chama chenyewe ambavyo vimejikita kwenye kuwatetea wanyonge. Kwa wananachi wa Mbogwe, mbunge mliyemwamini haaminiki wala hajui na wala hayuko tayari kutetea maslahi yenu bali tumbo lake. Mtoseni haraka ili mpata mbunge anayefanana nanyi. Ni ushauri wa bure tu. Kwa waheshimiwa wabunge waliopotoka na kumshangilia, jitengeni naye kwa kukiri kuwa alikosea na alichotaka hakiwakilishi mawazo yenu wala ya watanzania.
Chanzo: Raia Mwema leo.
No comments:
Post a Comment