Tasnia ya habari juzi ilipata pigo. Ni pale tarehe 8 Julai ilipoondokewa na mwandishi nguli Attilio Tagalile ambaye alitumikia tasnia hii kwa takriban miaka 50 kati ya 70 ya uhai wake. Binafsi, naandika tanzia hii kama rafiki wa karibu wa marehemu. Licha ya kuwa kwenye tasnia moja, nilimfahamu Hayati Tagalile kupitia kwa ndugu yangu Hayati Reggie Mhango (RIP) waliyekuwa wakifanya kazi wote Daily News. Tulikuja kufahamiana kwa karibu sana wakati tukisoma wote sheria pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Baada ya hapo, tulifahamiana siyo sisi tu bali wake na watoto zetu wakikutana kufahamiana na kuendelea kuishi kama familia rafiki.
Kwa wanaomjua Hayati Tagalile kama mwandishi wa habari nguli hasa mbobezi katika habari za michezo akiwa mchambuzi, watakubaliana nami kuwa alikuwa nguli haswa. Pia, alikuwa mwalimu wa uandishi akitoa semina mbali mbali baada ya kustaafu. Ukiachia mbali kufundisha kwa njia ya semina na warsha, alikuwa mwandishi wa vitabu aliyechapisha vitabu vitatu huku viwili alikufa akiwa mbioni kuvichapisha. Kwa wanaomjua Hayati Tagalile, alifisika kwa uwazi, ukweli na ubukuzi wake. Alisoma sana, saa nyingine kuliko hata kuandika.
Sasa Tagalile hatunaye tena. Je nini cha mno, mbali na urafiki na ukaribu kilichonisukuma kuandika tanzia hii? Kwanza, marehemu alikuwa mwandishi mzuri wa tanzia moja kati ya nyingi ikiwa ni ya Hayati Augustine Mahiga. Mbali na hiyo, alikuwa kielelezo safi cha waandishi na wachambuzi wa habari. Kusema ule ukweli, mwandishi wa habari, pamoja na kutumikia taifa kwa kirefu, halipwi vizuri kama maafisa wengine. Anachoambulia ni tanzia baada ya kufariki. Anayebishia hili anipe orodha ya waandishi maarufu ambao ni matajiri.
Kwa vile magazeti huandikwa na waandishi wa habari kama Hayati Tagalile, kwa tulio hai, hii ni fursa ya kufarijiana na kuendelea kutumikia wito huu wa kuhudumia taifa. Waandishi wa habari wana hali mbaya hasa wakati huu wa gonjwa la corona. Wanapaswa watafute habari hata kwa kuweka maisha yao na familia zao hatarini ili kutumikia wito huu. Pia, waandishi wa habari wana changamoto nyingi kulingana na aina ya serikali na viongozi walioko madarakani. Hili nisingependa nilijadili sana. Kwa wale waliopitia mshike mshike hasa kipindi ambapo vyombo binafsi, licha ya kukabiliwa na kesi, kufutwa na kunyimwa matanganzo na mtangazaji mkuu ambaye ni serikali wanajua. Kwa sisi ambao tumo kwenye tasnia ya elimu, si haba kwa wale wa viwango vya vyuo.
Kwa tuliomfahamu Hayati Tagalile kwa karibu, alikuwa mkarimu si wa mali tu hata hali. Ukifanya kosa au akigundua una upungufu katika fani, atakueleza hata kama kufanya hivyo kutakufanya ujisikie vibaya au kumlaumu. Hivyo, hakuwa mbinafsi wa maarifa mengi aliyokuwa amejilimbikizia tokana na muda mrefu wa kutumikia tasnia hii. Kwa upande wa mali, Hayati Tagalile alijua shida hasa ikizingatiwa alitoka mbali kufikia alipofikia. Ukiwa na shida atakusaidia hadi uone aibu. Kama binadamu yeyote, ukimwendea una shida na bahati mbaya akawa hawezi kuitatua, atakwambia, nenda kwa shemeji yako Mama Hans, huenda anaweza kukupa jibu. Naye Mama Hans, sawa na mumewe, ni mama mkarimu na mwelewa.
Kifo hakiepukiki ila kinauma hasa namna kinavyotuchukua. Hayati Tagalile hakuugua muda mrefu. Nadhani hata yeye hakutarajiwa angekufa ghafla kama ilivyotokea. Alikuwa tough. Mpiga judo na karate, muangalifu wa anachokula, anavyofikiri na anavyoishi kwa ujumla. Sie tunaomfahamu tumestuka na kupigika, sijui mkewe Maria, watoto wake Hans, Doreen na Yvonne wamepokeaje pigo hili. Sijui mjukuu wake Noah ambaye huwa napenda kumwita mgomvi wake anajisikiaje. Hakika, kul nafsi zalikatul maut bi maana kila nafsi itaonja mauti, tunapaswa kuwafariji waliobaki.
Baada ya kupata habari za kifo cha Tagalile, niliwasiliana na marafiki zangu tuliomjua kwa pamoja wengi wakiwa makamanda wa jeshi la polisi ambao tulisoma nao sheria. Kila mmoja ilimchukua muda kuamini huku wengine wakishindwa hata kujibu. Mie binafsi, mwezi huu umekuwa mugumu kwangu. Kwani wiki moja kabla, nilimpoteza rafiki yangu John Njema Ndamu (Chairman of Poor People) huko Githakwa, Tetu, Nyeri, Kenya ambaye naye alifariki ghafla. Kutokana na kutojulikana nchini, sikutuma tanzia yake gazetini. Badala yake niliituma kwa familia yake wakaichapisha na kuitawanya kwa waombolezaji. Sikujua nitaandika nyingine ndani ya muda mfupi.
Itoshe kusema kuwa sina nguvu ya kuendelea kuandika. Ninachoweza kusema ni kuwaombea Faraja wana familia yake, ndugu, jamaa na marafiki na wana tasnia ya habari.
LALA PEMA KAKA, NDUGU NA RAFIKI YANGU ATTILIO TAGALILE
HAMBA KAHLE MFOWETHU, MZALWANE
AAAMINA.
Chanzo: Raia Mwema Leo.
No comments:
Post a Comment