Tokana na kaya yetu kuwa ya amani hata kama ni ya imani, nashauri wanene wetu wasibadili katiba kiasi cha kuruhusu wafyatuliwe kila mara bila kujali nyadhifa zao. Mambo ya kubadili katiba ni ya kikoloni. Maana, huwapa mafyatu fursa ya kufyatuka na kufyatua wanene hovyo hovyo kiasi cha wanene kujikuta pakanga bila sababu. Natoa sababu zifuatazo kuwa chondechonde tusifanye makosa tukabadili katiba kwani, kufanya hivyo:
Mosi, tutawatoa mafyatu usingizini kiasi cha kuwafyatua wakaamua kufyatua. Ni kuwaongezea mafyatu madaraka makubwa wakati wao ni wadogo.
Pili, tutawaongezea wanene presha kiasi cha kuwalazimisha kula kwa uangalifu badala ya kula kwa miguu na mikono tena bila kunawa wala kutosheka mbali na hata wengine kutapika humo waliamo. Nani anataka kadhia hii ya kujitakia? Si muliwashuhudia Gen Ziro wa kule wakikinukisha kwa kudai kuwa ni haki yao kikatiba?
Tatu, ni hatari maana, kufanya hivyo, ni kuwafyatua mafyatu ambao, kwa ufyatu wao watawafyatua wanene kila mara kiasi cha kuwatia woga hata adabu jambo ambalo si safi kwa amani.
Nne, ni hatari kuwapa madaraka makubwa wadogo ili wawafyatue wakubwa. Kama mkifanya hivyo, mtapunguza hata kuondoa hadhi ya unene. Unene ni kwa wanene na udogo ni kwa wadogo.
Tano, tujue. Wanene huchaguliwa na Mungu. Unapoanza kugawa madaraka yao kwa wadogo wawafyatue huoni ni kinyume na mapenzi ya Mungu aliyewateua ingawa huwa hapigi kura?
Sita, kutoa madaraka kwa mafyatu ni kuwapa ukubwa wadogo wakati mafyatu siyo wakubwa wala wenye kujua mambo makubwa kama kutafuna kaya na kutumia madaraka tena waliyopewa na Mungu. Kwanini kuwaghasi wasioghasiwa, kuwasumbua wasiosumbuliwa hata kuwafyatua wasiofyatuliwa?
Saba, kubadili katiba ni jambo la hatari sana kwa kaya. Maana huwapunguzia wenye madaraka madaraka na kuwapa wadogo madaraka wakati hawayahitaji wala hawakuchaguliwa na Mungu.
Nane, kubadili katiba siyo kuleta uhuru zaidi bali udhuru. Kwanza, nani aliwaambia kuwa tunataka uhuru mwingine wakati uhuru wenyewe tuliupata miaka mingi iliyopita? Kubadili katiba na kutoa uhuru huu wa kifyatu ni ukoloni wa kizungu ambapo kila fyatu anajiona yeye ni yeye na anaweza kuwatisha hata kuwafukuza wanene kama walivyofaya hawa mafyatu wa kaya jirani.
Je sasa nini kifanyike? Nashauri yafuatayo:
Mosi, tusibadili katiba bali tuifanyie marekebisho na kutamka wazi kuwa sisi hatutaki fujo.
Pili, tuanzishe utaratibu wetu wa chata kimoja ili kuepuka usumbufu kwa wanene hata wadogo. Maana, tukiwa na chata kimoja, mambo ya kutekana na kupotezana yatatoweka. Hapatakuwa na haja ya kushikana uchawi wala kuwauliza wanene kwanini wanakula na kunenepa. Hivi kweli mnataka wale halafu wakonde?
Mwisho, napendekeza tufute hata hii katiba ili tuendeshwe kwa maono ya waona maono.
Lo! Kumbe niko bongolalaland!