Liberal Peace Conflict, Gender, and Peacebuilding
Thursday 23 May 2013
Machafuko Mtwara na utabiri wangu katika SAA YA UKOMBOZI
Ingawa kitabu changu cha SAA YA UKOMBOZI hakijawa hit, nafarijika kuona yale niliyotabiri yakitokea wakati nikiwa bado hai tena kijana. Katika kitabu hiki nilitabiri watu wa taifa la MIZENGWE kujikomboa kutokana na utawala kidhabi wa nchi hiyo. Wanakijiji wa KITHAKWA wakiongozwa na mzee maarufu aitwaye NJEMA NDAMU waliweza kuwatimua watawala na mapolisi wao walipofika kijijini pale wakiandamana na mzungu mwekezaji MR. SUCKER. Baada ya kugunduliwa vito vya thamani kwenye kijiji cha GITHAKWA, serikali iliamua kuuza eneo lao kwa mwekezaji huku ikija na amri ya kuwataka wanakijiji wahame ili kupisha 'maendeleo'. Mzee Njema msomi wa zamani aliyenyimwa kazi kutokana na kuipinga serikali ya Mizengwe alisimama kidete na kuwahamasisha wananchi kujikomboa kwa kupinga DHULUMA waliyokuwa wakitendewa.
Kwa kushirikiana na vyombo vya habari na wanaharakati wa haki za binadamu, wanakijiji wa Githakwa waliweka historia kwa kuwa wa kwanza kuangusha serikali kutokea kijijini na kupitia sanduku la kura. Rais mzururaji wa Mizengwe aliyekuwa ughaibuni akitanua alirejea na kukuta hali imeishachafuka kiasi cha kutapatapa na hatimaye chama chake kupigwa teke kwenye uchaguzi uliofuata. Baada ya kutimuliwa kwa njia ya kura rais huyo na familia yake na marafiki na waramba viatu wake walifungwa na wengine kunyongwa baada ya kupatikana na hatia ya kuhujumu taifa.
Sasa Mtwara kumekucha na maji yanaendelea kuzidi unga. Ni wakati muafaka kuwatia moyo wananchi kusiama kidete na kujiletea ukombozi wa kweli kupitia kuishupalia serikali inayoendekeza kulinda maslahi binafsi ya wakubwa zake na wawekezaji. Akina Sucker wapo wengi. Ni jukumu adhimu na takatifu la wananchi kuhakikisha wanabwaga kongwa na kushika hatamu ya nchi na raslimali zao. Haiwezekani serikali kuendelea kututenza kama hatuna haki wala akili. Ni habari mbaya na aibu ya aina yake kuona Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na polisi wakitumika kupora, kutesa, kupiga na kuua wananchi waliopaswa kuwalinda. Je tunalipeleka wapi taifa hili? Kikwete ona aibu kuna siku utakuwa nje ya ofisi na haya yatakufuata. Nadhani wanaharakati tuanze taratibu za kumfikisha Kikwete, Eamuel Nchimbi, Davis Mwamunyange na Said Mwema The Hague mbele ya ICC.Ni bahati mbaya kuwa akina Kikwete na genge lake bado wanaishi kwenye ukale wa kutojua kuwa haki za binadamu sasa siyo suala la kitaifa wala kikanda bali la kimataifa. Wakawaulize UhuRuto pale Kenya.
Je wafe wangapi ndipo watawala wetu watoke kwenye business as usual ya kulinda miradi yao ya kifisadi? HEKO WANANCHI WA MTWARA NA MSIRUDI NYUMA.
Jeshi letu la wananchi na la polisi wanapaswa kujitenga na kutumiwa kama nepi kulinda na kuficha uovu wa watawala mafisi na vipofu wasioona zaidi ya urefu wa pua zao. Ni wakati muafaka wa kuamasha hisia za ukombozi wa umma kuielekea na kuileta SAA YA UKOMBOZI. SAA YA UKOMBOZI NI SASA.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment