The Chant of Savant

Sunday 26 May 2013

Baraza la mawaziri litunge mitihani

Ajabu eti J4 Kawa-mbwa bado anang’ang’ania huku Njaa Kaya akijifanya haoni ushuhuba wao unavyoharibu kaya! Wanafiki watupu na wachumia tumbo walio tayari kuteketeza kaya kwa maslahi yao uchwara.
Baada ya tangazo hili la machukizo kutolewa, walevi tulikutana haraka haraka kujadili nini kifanyike. Katika kuskuti tumegundua yafuatayo ambayo tungependa wahusika watekeleze mara moja.
Mosi, kuanzia sasa baraza la mawaziri au serikali lipewe jukumu la kutunga, kusimamia, kusahihisha na kupanga matokeo. Kwanini baraza liwe na uwezo wa kufuta tu? Huku siyo kuzoea vya kunyonga siyo?
Pili, tunapendekeza walimu wote wawe wabunge ili waweze kulisaidia baraza la mawaziri mawazo na namna ya kutunga, kusimamia na kusahihisha mitihani. Kama mawaziri wamechukua mamlaka ya wengine kwanini yao nayo yasichukuliwe? Ukiwa tayari kula uwe tayari kuliwa ati.
Tatu, mawaziri wote wasio walimu watimliwe na mahali pake wachukue walimu. Pia katika kufanya hivi wahusika wahakikishe wote walioghushi wanatupwa nje ili wasije kufundisha watoto kughushi.  Nadhani mheshimiwa Willy Lukuvi aliyetangaza uamuzi wa serikali hapa ametupata. Pia mawaziri kama Emmy Nchimbi, Merry Nagu, Makorongo Muhanga na wote wanaotuhumiwa kwa kashfa ya kughushi lazima wapigwe chini ili uwe mfano kwa vijana wetu.   
Nne, tunapendekeza wauza unga na matajiri wote walioupata utajiri kwa njia za jinai kama vile ujambazi, rushwa, ufisadi na utapeli wakamatwe na kufilisiwa ili hili liwe motisha kwa vijana kuwa elimu ndiyo ufunguo wa maisha. Maana kwa sasa kama elimu ni ufunguo wa maisha basi ni ufunguo wa kuyafunga na si kuyafungua. Badala yake utajiri wa haraka utokanao na jinai kama zilivyotajwa hapo juu ndiyo ufunguo wa maisha.
Tano, ili kuepuka kukumbwa na kashfa nyingine hadi kutengeneza nyingine ya kufuta matokeo, mishahara ya walimu iwe sawa na ya wabunge. Hili litasaidia kutoa motisha kwa wasomi wengi tena waliobobea kuomba na kufanya kazi ya ualimu. Walimu ambao hawatateuliwa mawaziri au kuwa wabunge basi nao wapewe mishiko ya makalio almaarufu sitting allowance.
Sita, tunapendekeza watoto wote wa vizito wa sirikali na watumishi wote wa juu wa ofisi za umma wasiruhusiwe kusoma kwenye academies wala international schools. Hili litasaidia wazazi wao kuweka kipaumbele kwenye elimu badala ya kuiua kwa vile vitegemezi vyao haviathiriki.
Saba, tunapendekeza scholarships zote zitolewe kwa watoto wa walevi ili nao waweze kujikwamua toka kwenye uchovu wa kifedha na kielimu.
Nane, walevi wanapendekeza kuwa shule zote za kata zifutwe na majengo yake yageuzwe baa ili kuwapa nafasi walevi kukutana vizuri na kuunda sera muhimu kwa ajili ya ukombozi wa kaya. Hii ni kutokana na ukweli kuwa walevi wa siasa wameshindwa. Hivyo, walevi wa ulabu wanapaswa wapewe nafasi ya kuonyesha jinsi walivyo na vipaji vya ajabu vya uongozi.
Tisa, walevi wanashauri sirikali ifute uamuzi wake wa kufuta matokeo. Badala ya kuhangaika kutengeneza kashfa nyingine, itumike kanuni ya inverted reactions and elimination whereas the undesirable opposite is eliminated to justify its  desirable  opposite. Chini ya dhana hii, tume iliyoundwa ilipaswa kubadili matokeo yanayogombaniwa. Kwa vile walioshindwa ni 60%, tume ilipaswa kupendekeza ifanyike inversion kwa kutangaza kuwa 60% washindi na wale waliokuwa wametangazwa kuwa walishinda ambao ni asilimia 30 na ushei watangazwe wameshindwa. Pia chini ya dhana hii wanafunzi na wazazi wanaweza kufuta sirikali kazi kabla ya kukubali uamuzi wake wa kufuta kazi za wanafunzi. Simpo. Hii itaokoa pesa ambayo ingeharibika kwenye kuunda tume na kurudia kutunga, kusimamia na kusahihisha mitihani itakayotungwa kwa lengo la kuepuka aibu na kashfa nyingine.
Pia, ili kuondoa kufeli hovyo hovyo, uchakachuaji unaweza kuhalalishwa. Kama wale waliofikia uamuzi wa kuunda tume hata kufuta matokeo walipatikana kwa njia ya uchakachuaji, kwanini na wanafunzi wasifundishwe hii sayansi ya uchakachuaji ili kuepusha kashfa nyingine baadaye?
Kumi, walevi wanapendekeza mamlaka zinunue kompyuta vitabu na vifaa vya kisasa badala ya mashangingi ya waheshimiwa. Zana hizi zitawezesha wanafunzi kuvutiwa na kujisomea ukiachia mbali kuwawezesha kusoma kwa utulivu sawa na washimiwa wavyoweza kupata utulivu hadi kutukana Mjengoni kama matunda ya maisha bora. Nadhani watu kama Pita Seukamba wanapaswa kurejeshwa shuleni ili wajifunze kuyaangilia mambo muhimu ya kufanya kama waheshimiwa.
Nadhani kama tumeweza kufuta matokeo ya taifa zima, tutumie ithibati na uthubutu huu kufuta watu kama Sheukamba, Jobless Nduguy, Anna Makidamakida, Livingjiwe Lusinde na wengine wengi ambao wameshindwa vibaya kwenye uwakilishi wa umma.
Kumi na moja, waajiriwe walevi kufundisha mashuleni ili kuwezesha ujuzi wao wa kupambana na ufisadi na kuushinda kwa kujinywea na kujiburudisha uwasaidie wanafunzi kuepuka kufeli.
Mwisho, itakuwaje kama sheria itataka wakuu wote kuanzia wabunge hadi dingi mwenyewe waonyeshe matokeo (madudu) yao na jinsi walivyofika hapo walipo wakizidi kufanya madudu? Jibu, ni kupima utendaji wa kila mtu bila kujali udogo wala ukubwa na akionekana hajafikia malengo anafutwa kazi. Namna hii tutaendelea ndani ya kipindi cha wiki moja.
Kwa leo nakunja jamvi nikiwaomba walevi wote wawe wa ulabu au siasa kutafakari kabla ya kuingia kwenye mtego wa nyani haoni nonihino lake. Ili kuzuia wakubwa kuendelea kufanya mambo ya kitoto basi tuwaruhusuni watoto wafanye mambo ya kikubwa ili kunusuru kaya katika kashfa na aibu hii. Ni mawazo tu.
Kula la heri wakati ukinywa bia aina ya Kinana au Ndovu au vipi?
Salamu kwa walevi wote wa maeneo ya Shule ya Uhuru Roundabout na wale wa Mtibwa. Special Salaams to J4 Kawa-dog. Guy, what are you waiting while you've proved to be a damn stinking let down?
Chanzo: Nipashe Jumamosi 25, 2013.

No comments: