Na Ansbert Ngurumo
RAIS Barack Obama, anaingia nchini Tanzania kesho mchana.
Sihitaji kueleza nini kinaendelea hapa nchini kuhusu maandalizi ya
mapokezi ya kiongozi huyo.
Yamesemwa mengi na kuandikwa mengi. Haya yanayoendelea mbele ya macho
yetu na watawala wetu yanatosha kuitwa matusi dhidi ya utu wetu.
Iwe tulimwalika au alipanga mwenyewe kuja, kinachoendelea ni matusi
zaidi ya yale yanayowahangaisha polisi wetu na kuwafanya wawakamate
wanasiasa wa upinzani kuwa wanawatusi watawala.
Ndugu yangu mmoja ameniambia kuwa alipokuwa kijana wa shule moja ya
sekondari mkoani Tabora, alipata fursa ya kuwa miongoni mwa vijana
wachache waliochaguliwa kumpokea Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere, alipotembelea Mkoa wa Tabora.
“Kama ilivyo kawaida, kulikuwa na maandalizi ya mapokezi ya Baba wa
Taifa, wakati huo akiwa katika mwaka wake wa mwisho wa kuongoza taifa
letu kama rais.
“Alifika eneo la mapokezi akitokea uwanja wa ndege, na burudani kadhaa
zilifanyika; kisha akapewa nafasi kusalimu wananchi kabla ya kuingia
ndani kwa ajili ya vikao vya ndani. Kama kawaida hakuchelewa kupiga
vijembe palepale.
“Akawashukuru wananchi kwa kufika kumpokea. Kisha akasema; ‘Kwa niaba
ya miti hii na mawe haya yaliyopigwa rangi, napenda kuwashukuru viongozi
wa mji wa Tabora.’
“Akasema mawe yale na miti ile haijafanyiwa usafi muda mrefu lakini
sasa kwa ujio wake vimepata fursa ya kupigwa rangi na kumwagiwa maji.
Wananchi waliangua kicheko kikubwa.
“Kisha akarusha kijembe kingine kilichowauma viongozi wa mkoa. Akasema
yeye hapendi harufu ya rangi inayopakwa kwenye kuta na mawe kama njia
ya kupamba na kufanya usafi.
“Akasema anasikitika kuona viongozi wanang’ang’ania kupiga rangi kila
mahali anapokwenda wakidhani wanamfurahisha, wakati kimsingi wanamkera
sana. Hakuna aliyepiga makofi.”
Hadi hapa nani zaidi kati ya Obama na Nyerere? Wamarekani wameamua
kututusi nasi tumekubali. Wamejenga hoja kuwa hapa si salama, kwa hiyo
inabidi wao wenyewe wachukue jukumu la kumlinda rais wao na kutufukuza
sote mjini.
Wao wamegeuka wenyeji, sisi tumegeuzwa wageni, tena wageni hatari kwa
sababu wote kwa pamoja bila kujali nafasi zetu tunazotambiana nazo,
tunaonekana ni magaidi mbele ya Wamarekani na rais wao.
Lakini ukweli usemwe, hivi wapi ni salama kati ya New York na Dar es
Salaam? Askofu Desmond Tutu wa Afrika Kusini aliwahi kuwatibua
Wamarekani katika mdahalo mmoja uliohusu usalama.
Aliwaambia Wamarekani kuwa alikuwa anajisikia salama akiwa Soweto
kuliko akiwa New York. Alipoulizwa sababu alisema watu wengi wa Marekani
wanatembea na silaha mifukoni mwao, kwa hiyo kuna silaha nyingi
mitaani, kwenye treni, mabasi na hata kanisani.
Akasisitiza kuwa idadi ya silaha nyingi zilizo mitaani hata kama zina leseni, kwake ni tishio la usalama.
Rais Obama, iwe amekaribishwa kwetu au amejileta mwenyewe, wengi
tulidhani ni mgeni wa kuishia sebuleni. Kinachoendelea sasa ni kama
anatulazimisha tumkaribishe chumba cha kulala. Kwa ujio wake hakuna siri
ya taifa itakayobaki bila kuwekwa wazi mbele yake.
Tumesikia waheshimiwa wetu waliozoea kupigiwa mizinga 21 na
kutandaziwa zulia jekundu. Lakini safari hii ni makachero wa Obama
watakaoamua nani aingie kumpa shikamoo Obama
Kada na Mbunge wa CCM, Kapteni John Komba, aliwahi kuimba wimbo
uitwao: ‘MGENI’. Katika wimbo huo anaeleza mgeni alivyoingia chumbani na
kumwaga upupu. Matokeo ya upupu huo, baba na mama wanajikuna.
Obama anataka kuingia chumba cha kulala ili afanye nini huko? Mbona
rais wa China amemtangulia? Mwanamwali wetu atakuwa salama kweli?
Simaanishi Salma, namaanisha mwanamwali wetu wa taifa, yaani gesi,
dhahabu, pembe za ndovu na tanzanite.
Kwa nini hataki kusubiri tumletee sokoni au angalau sebuleni? Anaingia
chumbani kutafuta nini? na ‘kitanda’ hicho kitalaliwa wangapi?
Waafrika tunaruhusu mme mmoja, wake wengi; lakini si mke mmoja waume
wengi! Hii mila yetu hivi sasa inapigwa vita lakini inavumilika.
Hii ya mwanamwali wetu wa taifa kugombaniwa na wanaume wengi
itatuletea upupu, kwa sababu waume wengine wanaoingia huko ‘hata kupima
hawajapima!’
Tena kwa Obama ni hatari zaidi kuingia chumba cha kulala, kwa sababu tumemsikia huko Senegal akipigia chapuo ushoga.
Asivyo na dogo, na kwa jeuri hii ya Wamarekani, Rais Obama anaweza
kurudia kauli hiyo hapa Dar es Salaam, tena akasindikizwa na vicheko na
tabasamu za watawala.
Kwa tabia yake hiyo ya kushabikia ushoga, kuna hatari akaingia
chumbani na kumfukuza bibi harusi, ili abaki na baba yetu. Je, atakuwa
salama?
Yawezekana lugha hii ya kishairi ikawauma baadhi ya wasomaji, hasa watawala na maswahiba wao. Lakini huu si utani.
Tumevuliwa nguo, tumedhalilishwa. Utu wetu umeondolewa kwa hiari ya
watawala wetu. Kumbe haya ndiyo madhara ya kutembeza bakuli bila kikomo.
Tumekuwa tunashangilia kumwona rais wetu akishinda na kulala kwenye
ndege, huku akidai anakwenda Ulaya, Asia na Marekani kuhemea.
Sasa ulaji umegeuka ‘uliwaji’. Kwa hakika tumeliwa na kugeuzwa
kitoweo. Na sasa hawataki kulia kitoweo hiki sebuleni, bali chumba cha
kulala. Tukubali kudhalilika kwa kiwango hicho? Na bado tunadai sisi ni
raia wa nchi huru?
Chanzo: Tanzania Daima Jumapili Juni 30, 2013
4 comments:
Simlaumu Obama kuja na watu wake. Huyo Dakta wetu akihongwa suti tano tu anaweza kuwaacha shemeji zake wamlipue Obama. Jamaa dau lake ni dogo sana.
Hata na hivyo vyombo vya usalama vinachojua ni kuwalipua wananchi wasio na hatia. Ukiwaambia wafanye kazi yao ni kama kuwatukana. Nakumbuka mara ya mwisho kuja Tanzania nilipoibiwa hotelini nikafanya kosa la kurepoti uhalifu. Not only ikabidi niwapatie usafiri polisi, ilibidi niwape hongo halafu na mwisho wake wakaniambia kuwa ni ndugu zao niliokuwa nao ndio wezi wenye kwa hiyo inabidi wakamatwe. Kwa hiyo ikabidi nitoe hongo nyingine wasikamatwe. Nikakutana na jamaa wa Australia naye aliibiwa kwenye basi na yeye pia "akaibiwa" na polisi.
Sidhani Tanzania kuna kitu Marekani ambacho hawawezi kukipata sehemu nyingine. Nchi zinazopeleka mafuta kwa wingi Marekani ni Canada na Mexico kwa asilimia 11 kila moja. Hata gesi asilia inasafirishwa kwa maboma ni kama bilioni 220 cubic feet. Inayofuatia ni gesi inayogeuzwa maji (Liquified Natural Gas). Incidentally, nasikia makachero wa Iklu walikuwa wanataka kumkamata bibi kizee aliyetishia kuigeza maji gasi ya Mtwara kama ingesafirishwa kwa bomba kwenda Dar. Ma-genius wa Ikulu hawakujua kuwa itakuwa ni rahisi kupeleka kwa meli!
Tungesisitiza asilimia watu tungekuwa mbali. Kuna nchi nyingi tu hazina rasilimali lakini zimepiga hatua kama Japan, Korea Kusini, Singapore, Taiwan, nk. Na kama ukiwa na madini halafu na viongozi wa CCM unajiona afadhali uwe masikini tu.
Jaribu, wanaojua kilichokuwa kinaendelea ni kwamba Bwana Mkubwa alikuja kwa sababu kuu mbili.
Mosi kufuta nyayo za Xi Jinping rais wa Uchina aliyembelea Bongolalaland hapo Machi 28. Na pili kuhakikisha yale machimbo ya Uranium hayaingii kwenye mikono ya jamaa.
Interesting! Maana hizo sababu walizokuwa wanatoa zilikuwa haziridhishi.
Hawana sababu zozote za msingi bali umbea na uongo wa mchana kweupe. Hata hivyo, soon ukweli utadhihiri na wahusika wataummbuka. Silly them!
Post a Comment