The Chant of Savant

Saturday 6 July 2013

Barua ya wazi kwa Pinda toka kwa walevi


Baada ya Waziri Mkubwa, Mizengwe Pindapinda, kupinda na `kupayuka’ huku akifyatuka, kikao cha walevi kimemtuma mlevi kumpa salamu zake.
Kwanza, tunampenda na kumheshimu sana. Ila tunamshauri atubie kabla kiama hakijamshukia. Maana huwa tunasikia akisema `eti’ yeye ni mtu wa God utadhani wapo wa shetani ambaye hakuumba chochote.
Mbona huko nyuma hakuwa hivyo! Ameharibiwa na nini yarabi mwana wa farmer ambaye siku hizi amekuwa mwana milionea anayeweza kuvaa `misaa’ ya dhahabu ya bei mbaya.
Au `maulaji’ yamemlewesha kiasi cha kuanza kale ka ugonjwa kaitwako `Yusufuosis Makambiasis’ aliyesifika kwa kupayuka hovyo.
Sijui ameishia wapi baada ya kurithisha `ulaji’ kwa kitegemezi chake? Bongo kwa utawala wa kifalme sina mfano.
Yaani kila big anajitahidi kuhakikisha mikoba yake anampa kitegemezi chake! Je, wasio na madingi heavy wataishia kutawaliwa na kuliwa hadi lini? Anyway, hii siyo `inshu’ leo.
Kwa sisi wataalamu wa saikolojia, tunaweza kusema kuwa Pindapinda alipopayuka kuwa `ndata’ wawachape walevi hata wakiwanyotoa roho kama walivyofanya kule Arusha, yawezekana alikuwa akisumbuliwa na kile ambacho kitaalamu kinaitwa Cocktail Party Phenomenon (CPP), gonjwa ambalo huwasumbua wale wanaotumia sana hasa utumiaji wenyewe unapokuwa ni wa `dezo’ kama katika hali hii.
Mwenye kuugua ugonjwa huu mara nyingi anaweza kuongea bila mdomo wake na kichwa kuwasiliana. Kitaalamu tunasema kunakuwa na disconnection and confusion among neurons especially axoms in his amygdala. Hayo tuyaache maana ni ya wataalamu.
Kupayuka kwa Pindapinda kumenikumbusha wagonjwa wengine wanaougua ugonjwa wake yaani kihiyo Bill Lukuvy, Mwehujuu Nchembe, Nipe Mapepe Ninaye na Chris Mtikilila ambaye siku hizi hana tofauti na Lyatongolwa kwa kujikomba, ili pate `ulaji’ hata kama ni mchafu na haramu.
Hakuna mtu mwenye akili alitegemea mwanamume timamu kutoa kejeli na matusi ya nguoni wakati wa msiba wa mabomu iliyorushwa na washenzi wanaotumikia washenzi wenzao wanaoona ulaji ukiwaacha kutokana na ulafi na upogo wao.
Tumuulize bwana Pindapinda kwa niaba ya walevi waliotutuma. Kaka unataka wafe wangapi? Je, una habari kuwa kuna taasisi inaitwa ICC au International Criminal Court ambayo wale huiita International Komesha Korti ambayo siku hizi inawashughulikia walevi wa madaraka wanaoamini katika matumizi ya jinai kama uliyotetea?
Walevi wanasema umepinda sana na baadaye anaweza kupinduka kama siyo kufyatuka tena. Hivi kaka hujui kuwa ndata wameishadedisha walevi kibao?
Yaani pamoja na walevi wengi `kudedishwa’ hujaridhika! Kaka umekumbwa na nini au Sumba wameishasumbawanga?
Baada ya kusikia kauli zako za maangamizi yaani Words of Mass Destruction (WDM) kwa lugha ya Kibush kichaka, walevi tulikutana kwa mama muuza mitaa ambayo ni siri kubwa na kushauriana tukukabili ili kukunusuru.
Kwanza, tulikubaliana tukupe ushauri wa bure kuwa ufute kauli yako, kuomba msamaha na kutubia. Pili ujiuzulu japo kwa genge lenu kufanya hivyo ni ndoto.
Tatu, uje kwenye kikao chetu na kutupa `ofa ya ulabu’ ili tuwapoze jamaa wasije kustuka na kuamua kufanya kweli wewe na wenzio mkajikuta pabaya.
Tulihofia yasikukute makubwa kutokana na kujua kuwa umma wa walevi una nguvu kuliko hata bomu la nyuklia.
Ukiamua hao ndata hawawezi `kufua dafu’ zaidi ya kutoka mkuku kama ilivyotokea kule kwa Mwamali Kadhafi wa Kashafi `aliyededishwa’ kama kibaka.
Japo unaweza kuchukulia ushauri wetu kama mawazo ya kilevi na `tishatoto’, ufahamu mambo yamebadilika sana.
Nani alijua kuwa nguli kama Kadhafi angeuawa kama kibaka huku akilialia kama kichanga?
Kwa vile walevi wanakupenda na kukuzimia, wangependa usiaibike wala siku moja kuzomewa au kuja kujilaumu kwa kupayuka. Tunajua ulipitiwa kama ngurumbili.
Ukubali ulichemsha na kupayuka bila kufikiri vilivyo. Hivyo, usione aibu kutubu na kujirekebisha. Rasmi natoa pendekezo la nia nzuri toka kwa walevi.
Kwa vile walevi ni wajanja na great seers, tumeamua. Kama ushauri wetu wa bure utapuuzwa basi tuandamane hadi siku utakapofunga virago na kuachia `ulaji’ ili waje watu wengine wasio wagonjwa.

Tumepania kuhakikisha tunafanya kweli hata kama tutapaswa kuumizwa na hao ndata wako.
Tuko kwenye kampeni na ushauri kwa `bi wakubwa’ zetu kutusaidia kuandamana kwa kuvua nguo ili ulaaniwe na kigwena chako ambacho kimehalalisha ukandamizaji (Lwakatareing), utekaji (Kibanderings), vipigo (Ulimbokering) na mauaji (Mwangosirings) ya walevi.
Wana mpango wa kuonana na `bi mkubwa’ Tununu kwanza, ili wampe siri yao kama mother na madhara yatakayokukumba na familia yako.
Amini hivi si vitisho bali watafanya kweli ili likupate la kukupata. Jiulize wako wapi akina Ommy Ngunguri Mahitason?
Wako wapi akina Beno Mkaa Hapason aliyejifanya Mungu mtu asijue angeishia kuwa kituko na aibu kiasi cha kuhitaji kulindwa na Njaa Kaya ili asinyee debe?
Kaka, ninakushauri usidharau utume huu unaojikamilisha yaani self-fulfilling prophecy kwa kimakonde.
Kwani katika pita pita yangu mitaani nilishuhudia na kusikia hata ndege mbuzi na hata tumbili wakilaani kauli yako ambayo sisi tunasema ni bahati mbaya kiasi cha kukushauri utubie mara moja.
Kitu cha maana kufanya mbali na kuomba radhi na kutubu na kufunga ni kukubali kuwa `chata’ lako limeishiwa na hakuna anayelitaka tena kutokana na kutekwa na mafisi na `mafwisadi’ ukiachia mbali kutumia ndata kunyotoa roho za walevi.
Najua utasema tumetumwa na Chakudema kukupa fwacts hizi, huko Arusha utasingizia siasa na Ntwara nako je?
Ningekuwa wewe ningeanza kufanya mazoezi ya kuwa msemaji mkubwa wa upingaji baada ya kutupwa nje kama kiama na kuutema ukuu wa sirikali mjengoni ambako nako kumegeuka uwanja wa fujo ambapo mabondia uchwara kama Jay Nkamia wanatishia maisha ya wenzake.
Hata hivyo, ashukuru Mungu anawaonea akina mama. Angemgusa mtu kama kama Pita Msigwa si angeumizwa vibaya `jore’ huyu? Jay Nkamia `jore’?
Washikaji wangu wa kule Haubi Maziwa, Makomango, Babayu, Mombose, Chinyika, Chase, Gonga, Mbugutole, Farqwa, Itanda na Magu mpo?

Chanzo: Nipashe Jumamosi 6, 2013

No comments: