How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Sunday, 21 July 2013

Wanaume wabambikizwa watoto


  Mkuu: Asilimia 48 siyo wa baba halali
Mkemia Mkuu wa Serikali Nchini, amesema zaidi ya asilimia 48 ya wanaume waliojitokeza kupima vipimo vya vinasaba (DNA), wamegundulika kubambikiwa watoto.
Takwimu hizo alizitoa jana kwa mujibu wa vipimo vya DNA vilivyochukuliwa miaka mitatu kuanzia mwaka 2010.
Ripoti hiyo ilitolewa jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Kitengo cha Makosa ya Jinai na Vinasaba, Gloria Machuve, wakati akielezea kazi za ofisi hiyo katika uchunguzi wa vinasaba vinavyotokana na matukio na mashauri mbalimbali.
Alisema asilimia 48.32 ya watoto waliofanyiwa vipimo vya DNA kwa kipindi hicho, wamegundulika hawalelewi na baba halali.
Alisema utaalamu huo wa kuchunguza vinasaba ulianza mwaka 2010, ambapo hadi kufikia mwaka 2012, mafanikio makubwa yamepatikana kwa kutatua mashauri na kuwatambulisha watu uhusiano wao.
Pamoja na kubaini watoto hao, pia alitaja matukio mengine yaliyotumia teknolojia hiyo kwa utambuzi ni mauaji, majanga ya kimaumbile, ubakaji, wizi, utambuzi wa binadamu na jinsia tawala.
Alisema kwenye utambuzi wa uhalali wa watoto, sampuli mbalimbali kutoka kwa watu tofauti zilipimwa na kuonyesha asilimia kubwa ya watoto hawalelewi na baba halali.
"Idadi hiyo ni kubwa watoto walionekana hawana uhalali wa vinasaba vya mzazi wao (baba), lakini takwimu hii siyo kwa nchi nzima ila tu kwa wale wanaofika kwetu na kutatua mashauri ya kufahamu watoto wao," alisema Machive.
Alisema kwa kutumia teknolojia hiyo, sampuli za wazazi na watoto huchukuliwa na kuingizwa katika mashine yenye uwezo wa kuchambua vinasaba kugundua uhalali wa mtoto.
"Vinasaba huwa havidanganyi, ikiwa mtoto vinasaba vyake havifanani na baba ni dhahiri siyo wa kwake ila alidanganywa kwa sababu mbalimbali," aliongeza.
Machuve alifafanua kwamba vinasaba vina umbo la majimaji yenye kemikali, ambayo yana taarifa kamili ya mtu husika ikiwa ni asili yake, umbo, rangi na jinsia.
Hata hivyo, mtaalamu wa DNA, Fidelis Segumba, alisema teknolojia hiyo imeweza kutatua kesi ya mauaji ya Albino na vikongwe mkoani Shinyanga na Sumbawanga. Pia majanga kama milipuko ya mabomu Mbagala na Ukonga, kuanguka kwa majengo jijini Dar es Salaam, ubakaji na mimba za utotoni mkoani Mbeya, kuwatambua wahamiaji na wizi wa Benki ya NMB wa mwaka 2006.
Aidha, alisema gharama ya kupata huduma hiyo ni Sh. 100,000 kwa sampuli na kuwataka wananchi kupeleka mashauri yao katika ofisi zao za kanda zilizopo mikoa ya Mwanza, Arusha Mbeya na Dar es Salaam.
Segumba alisisitiza kuwa wanatarajia kuongeza ofisi zaidi katika mikoa ya Dodoma na Mtwara kuwarahisishia wananchi huduma hiyo.   
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI 

No comments: