BAADA ya wachovu kuchoka na kuchoshwa na vipigo hata vifo vya ndata, kijiwe kimekutana kuja na suluhu mara moja yaani kuunda jeshi la kujilinda. Jeshi hili si la kujilinda tu bali hata kuwakabili ndata wanaonyotoa roho za wachovu.
Hivyo, kikao cha leo kitajadili ukombozi huu wa wachovu toka mikononi mwa ndata na watawala waliofilisika kama alivyosema Njaa Kaya hivi karibuni.
Msomi Mkatatamaa anaingia akiwa anasonya. Amebeba tabu kubwa liitwalo “Self Defense au Wushu-cum Gung-fu” lililoandikwa na mwandishi nguli wa Uchina aitwaye Tel Hao Juha.
Hata kabla ya kuamkua, mzee Kidevu anamuuliza; “Msomi ina maana unalisoma hilo tabu lote bila kupofuka?” Msomi anajibu; “Mbona hiki kijitabu kidogo?” “Una maana kuna vitabu vikubwa kuliko hilo?” Anauliza Mbwa Mwitu.
Msomi anajibu; “Kweli wahenga walisema kuwa ukitaka kumficha mjinga kitu weka kwenye maandishi. Yaani kusoma kitabu hiki kidogo mnaona kama muujiza, mbona vipo tena vinene vinavyokaririwa?”
Mpemba anaamua kukamua mic; “Yakhe wajua nchi hii watu hawasomi. Hata hao wanaojiita watawala hawasomi. Wapenda zurura na piga picha na wachezaji npira basi.”
“Mpe kahawa Ami amenena jambo kubwa na la maana sana,” anasema Msomi na kuendelea: “Ni kweli. Kaya yetu imeingiliwa na mdudu aitwaye ujuha. Usione mijitu inajisifu. Haisomi. Itasomaje wakati imeendekeza kughushi na shahada za kuzawadiwa? We are manned by a bunch of mere nincompoops and goons.”
Kabla ya Msomi kuendelea, Mgosi Machungi ananyakua mic: “Mgosi usitifanye tilie. Huoni hao mawaziri waliofoji shahada wanaendeea kutesa huku Njaa Kaya akijifanya haoni waa asikii? Namna hii nani atapoteza muda kwenye kusoma?”
Wakati mjadala ukiendelea na kuanza kuwa moto, Mchunguliaji aliingia akiwa na nakala ya gazeti la Danganyika Leo. Kichwa cha habari kilisomeka, “CHAKUDEMA Kuunda Vikundi vya Kujilinda Ndata Watishia Kukibander Atakayeviunda.”
Mzee mzima niliposoma kichwa cha habari sikungoja hata kuingia undani wa stori yenyewe. Kwa vile nilishaona kwenye runinga yangu yule Mamsap wa Ndata akitoa mapofu na kutisha, nilijua sasa kimeumana.
Hivyo, nilitoa wazo nasi tuunde jeshi na si kikundi cha kupambana na ndata ambao wamezidi kwa kutughasi kwa maagizo ya wakubwa mufilis wao. Hata hivyo nimemdeku yule binti.
Kwa vile mimi na Msomi tunaogopewa kwa kuona mbali, pendekezo langu lilizua mjadala si kawaida. Ni kama nilikuwa nilimwaga mafuta kwenye moto wa kiangazi! Mbwa Mwitu alikamata mic na kukamua: “Mzee Mpayukaji kama si kutokuwa Casanova kama jamaa yetu ningekupa dada yangu kutokana na kujaliwa kichwa.”
Kabla ya kuendelea Mchunguliaji aliingilia: “Mbwa Mwitu acha matusi. Unataka kumpa dada yako amfanye chuma ulete siyo?” Mpemba naye anachomekea: “Yakhe mambo ya kupeana walaji yaache. Ushasikia wale wasichana ambao wakiolewa waambwa wachume pesa na kujenga nyumba kwao? Huu nchezo mbaya wallahi. Kwanini utumie mwili wako kama dukaa?”
Msomi kagundua kuwa mjadala utaharibika. Anaamua kuokoa jahazi. “Hayo mambo ya kinu kujenga nyumba waachie wenyewe. Nadhani tujadili hili la muhimu la kuunda jeshi la kujihami.” Anakohoa na kuchezea chezea tabu lake na kuendelea: “Juzi nilimsikia huyu dada ambaye sijui waliomsimika pale walimuibua wapi? Anaitwa Shenzo. Amenichafua God knows. Anadhani hii kaya ni mali ya baba yake na hao washikaji zake siyo?”
Kabla ya kuendelea, Mbwa Mwitu ambaye hakuridhika na hoja ya dada yake kuuawa anachomekea. Anatishia: “Naona wale ndata wanakuja.”
Baadhi ya wanywa kahawa wanaonekana kutishika isipokuwa mimi na Msomi.
Msomi anaendelea: “Waache waje na kama watatuletea ujuha tunafanya kweli kwani sisi si walume kama wao?” Anakunywa kahawa yake na kuendelea: “Wazee mambo ya kutishiana nyau waachie wenyewe waliofilisika na kushindwa.
“Kwa vile mzee na msomi mwenzangu mzee Mpayukaji kaona mbali, lazima tumuunge mkono kwa kujikomboa na kuhakikisha usalama wetu. Bila kuwa na jeshi la kujilinda, tutaendelea kuuawa na kupoteza mali zetu bila sababu.
“Hamkuona hata Obamiza alivokuja aliamua kujilinda?” Ananitazama. Tunatabasamu. Naamua kumpa tafu: “Usemayo mzee na msomi mwenzangu ni tunu. Ni juzi nilikuwa nasoma kitabu kiitwacho “Das Capital”, cha Karl Marx aliyesema kuwa kujitegemea kwa kila hali ndiyo mtaji mkubwa wa maendeleo na utimamu wa binadamu.”
“Usemayo ni kweli msomi. Juzi nilimaliza kusoma kitabu cha Tiffany Madson mwandishi maarufu wa Kimarekani alisema: “The Second Amendment is timeless for our Founders grasped that self-defense is three-fold: every free individual must protect themselves against the evil will of the man, the mob and the state,” alichomekea Msomi huku akiacha kutafsiri.
Mzee Maneno anaingilia: “Msomi Ukameruni huo. Umetuacha kizani sisi ambao tuliogopa umande na kughushi.”
Msomi anaamua kutafsiri nukuu yake kinamna: “Hivyo kujilinda ni haki ya kila mmoja bila kujadili kama mhusika ni kamanda wa ngunguri au ngangari mwenyewe. Hivyo, lazima kijiwe kiwe na jeshi lake la kujihami bila kujali vitisho na uhuni vya madam Shenzo.”
Mgosi ambaye alikuwa akisikiliza na kusoma gazeti aliamua kuchomekea: “Nasikia jamaa imeogopa baada ya kuiwa kue Arusha baada ya kushindwa kuiba kua. Baada ya Chakudema kufanya kwei kue imeamua iunde vikundi vya kujiinda ili kwenye uchaguzi ujao isichakachuiwe kua zake. Nadhani nasi kwa vie tinataka kuaingia kwenye siasa shuti tiwe na jeshi la kujiinda au siyo wagoshi?”
Mara mzee Mipawa na Kapende wanatia timu huku wakiwa na gazeti la Danganyika Daima. Wanatuamkua na kumwaga usongo wao.
Mipawa anaanza: “Wazee muiona hii ngoma ambapo ngunguri wameshikwa pabaya hadi kuweka ndata kimada?” Mbwa Mwitu anauliza: “Nkwingwa mbona hueleweki? Una maana gani kusema ndata wamewekwa kinyumba?”
Kapende kapata upenyo. “Mbwa Mwitu kwanini unapenda kuuliza majibu badala ya maswali? Yaani huoni hii jinai na dhulma inayoendeshwa na Chama Cha Mafisadi kudai wengine wasiunde vikundi vya kulinda kura zao ili kiibe? Nilishangaa kusikia huyu bi mkubwa wa ndata akitishia watu utadhani naye ni kada.” Mzee Kapende: “Acha nikupinge kidogo. Huyu bi mkubwa ni kada sawa na akina Shimboshimbo aliyesimikwa hivi karibuni kuwa balozi. Unadhani hivi vyombo vya dolari vinaundwa na watu wasio makada? Umenoa. Wana kadi zao vibindoni ndiyo maana wanatumiwa japo huko nyuma hawakuwa hivyo. Hii ni jinai ya kujuana na kulindana ambapo huteuana mafisadi kwa mafisadi ili kuendeleza mchezo mchafu. Hakuna mufilisi wa kisiasa kama huu.”
Anakohoa na kuendelea: “Ni kwa vile wewe na Mipawa mlichelewa. Hapa tunajadili namna ya kuunda jeshi la kupambana na ndata hawa waliowekwa kinyumba na kila majambazi kuanzia wanasiasa mufilis, wauza unga, mjambazi hata FBIAI. Litaiwa Redi Bridge.” Naona mchuma wa Shenzo unaingia, wacha niende nikamchombeze.
Chanzo: Tanzania Daima Julai 24, 2013.
No comments:
Post a Comment