The Chant of Savant

Tuesday 16 July 2013

Sikujua Obamiza ndiye mkuu wa Kaya!

“Ama kweli mgeni njoo wenyeji wakome waive na ikiwezekana waipuliwe.”
Anaingia mgosi Machungi akiwa ameshikilia gazeti la Danganyika Daima mkononi. Inaonekana leo kimemkubali, maana huwa si mnunuzi wa magazeti msambaa huyu.
Mbwa Mwitu anamuuliza, “Mgosi unamaanisha nini na nani aliwe na kuipuliwa?”
Mgosi anajibu, “Si hao viranja wenu wanaojiuza kama vyangudoa!”
Msomi Mkata Tamaa anaonekana kukerwa na alichokiona. Anakwanyua mic, “Kwa walioshuhudia nguvu ya bwana mdogo Obamiza na jinsi alivyowahenyesha viranja wenu ambao hudanganya kuwa nao wamo, watakubaliana nami huyu ndiye rais.”
Anakunywa tangawizi na kubofya Kinokia chake na kuendelea, “Uliona wapi mgeni anakuja kwenye kaya na kukupangia alale wapi, alale na nani, ale nini apokelewe na nani? “Nikikumbuka wakuu uchwara walivyopangishwa foleni kama watoto wa shule za kata sina hamu. Akiondoka Obamiza utayaona yanajishaua kuwa nayo yamo.”
Mzee Maneno anachomekea, “Nasikia wengine walikataliwa hata kumpokea kwa vile wana sura za kigaidi au walighushi vyeti vya elimu.”
Anakohoa na kuendelea, “Walahi naapa kama Mchonga angekuwapo ama angejinyonga au kutafuta uraia kaya nyingine.”
“I truly don’t know and I won’t know. How come that people are acting as if they only have masaburis upstairs?” Msomi anamwaga Ukameroni wake na kutuacha hoi.
“Msomi hiyo Masaburis nayo ni kimombo?” Mzee Mipawa anauliza.
Hatuna mbavu!
“Nimeongea kimombo kwa makusudi ili salamu zimfikie Obamiza anielewe,” Anajigamba Msomi.
Kuona Msomi anazidi kukomba ujiko nami mzee mzima naamua kukamua mic, “Mna habari jamaa wanajua hasira zangu? Walitaimu wakati niko zangu Sauzi kwa Madiba vinginevyo ningewatokea FBI wake na kuwauliza lini walikuwa ndata wa kaya hii. Ajabu mindata nayo imekaa inasubiri wapingaji ikawalipue na kuwaulia mbali.
“Mliona jinsi Obamiza alivyolazimisha vilaza wetu kumuingiza bibi yake kayani hata bila kufuata utaratibu wakati wazito uchwara wetu wakizuiwa hata kushikana naye mikono?”
Kabla ya kuendelea mzee Mipawa anadandia mic, “Lakini tuliwaonya mchague watu kama mzee Mpayukaji tuwakomboe mkakimbilia takrima sasa wanawatakrima kuwakrimia wabamizaji. Mtaliwa sana.”
Msomi kapata upenyo. Akandamiza mic, “Inahitaji akili ya kiwendawazimu kumuachia mtu kaya yako afanye atakavyo kuanzia geshi hadi ndata. Kwanza, nina mpango wa kumshtaki Obamiza kwa kuangusha sirikali ya kaya kwa muda aliokaa kayania. Hakuna aliponitisha kama alivyotetea kale kamchezo kalikolaaniwa na vitabu vyote!”
Mpemba aliyekuwa akivuta tasbihi anachomekea, “Walllaahii mie humo simo!”
Kapende anachomekea, “Kesho utasikia watu wanajipeleka kwa Obamiza awabamize. Wamezoea kubamizwa. Na inaoneka wamenogewa na vitu vyake. Maana anavyokata pochi kwa kaya ombaomba si kitu cha kuachia. Je tutaendelea kubamizwa na Obamaiza na misaada yake hadi lini?”
“Yakhe kama kubamizwa wabamizwa weye si mie. Hiyo nsaada akawape mamba lakini si mie wallahi,” Mpemba anachomekea na Kiswahili chake cha Kipemba na kutuacha bila mbavu hasa anaposema hataki kubamizwa na misaada ya Obamiza.
Hakuna aliyetuacha hoi kama Mbwa Mwitu aliyedai kuwa alishuhudia MaFBi wakiwavua nguo tuliodhani ni waheshimiwa kuona kama walikuwa wamebeba zana za maangamizi.
“Yaani mgeni wenu hawaamini wenyeji pamoja na siku zote kujilisha pepo mkitembea na misafara wakati ni kanyaboya? Kumbe duniani ni mmoja anayestahili ulinzi na misafara yaani Obamiza.”
“Si kweli usemavyo Mbwa Mwitu. Hapa tatizo si Obamiza. Mbona huu upuuzi na udhalilishaji hatukuusikia Sauzi? Alichomekea Msomi huku akiendelea kubwia tangawizi yake.
Kapende aliamua kutuumizia mbavu, “Waheshimiwa mna habari kuwa hata Njaa Kaya alipigwa sachi kabla ya kukutana Obamiza?”
Tulicheka hadi wengine wakapelekwa hospitali kutokana na kuumia mbavu.
Anaendelea kukmwaga vitu, “Nilisema kuwa hii kaya inaliwa mkasema natukana. Mmeona Wamaarikani walivyokataa hata zimamoto yetu iliyozea kuitwa na kuwaambia waathirika kuwa wanabipu au hawana maji?”
“Hapa mgosi nakubaiana nawe. Maana ukiangaia tiivyo na midini na kia aina ya midude inayotakiwa dunia nzima akini bado tu maskini basi azima kuna wanaokula.”
Hata hivyo, kijiwe kimeandika barua ya kumpongeza Obamiza. Kumbe hii misafara tunayoshuhudia na waishiwa wetu ni kupoteza muda. Ingekuwa si hivyo nao tungeona wakimwambia Obamiza kuwa huwa wana walinzi na mabaunsa na wanastahili usalama. Kumbe hola!
Je, wajua kuwa ule mgodi maarufu wa midayamondi kule Maganzo haujawahi kulipa kodi? Je, wajua kuwa Richmonduli-Downs na Symbisis Danganyika ndiyo walioula kwenye ziara ya Obamiza? Ngoja nikatafute bangi nibamize nisijembamiza mtu mie!
Tuonane wiki ijayo washirika.

No comments: