JUZI nusu mgosi Machungi azipige na ndata bila kujali wangemlipua na mibomu yao ya kigaidi au la. Mgosi akiwa zake mitaa ya Buguruni kwa Mnyamani akipanga kwenda zake Kigogo Mwisho kudai njuluku zake toka kwa mzee Mipawa, si ndata wakamsimamisha na kusema eti ni ombaomba ambaye hapaswi kuonekana jijini kutokana na kuja kwa Rais Black Obamiza.
Kwa vile Mgosi anajua kuwa nilimfundisha huyu dogo wakati nikiwa profesa wa sheria pale Harvard University aliwaambia kuwa waache upumbavu wasidhani walevi wote ni fyatu na taahira wanaoweza kuabudia madaraka na misaada kama wale.
Hakuna kitu kiliwaacha hoi ndata kama Mgosi aliposema; “Nyinyi acheni ushamba. Msitifanye washamba. Huyo Baaka wenu kwa taaifa yenu amefundishwa na afiki yangu Mpayukaji. Isitoshe hapa kuna jeshi au umbea? Mbona mimeshindwa kumlinda Obamiza hadi waje waume toka kwake wakati nyinyi mkiangaia tu?”
Alitema bonge la mate baada ya kumaliza kuvuta msigara kali wake na kuendelea kuwapasha; “Kwa zina ja Zumbe kama nyinyi wanaume si mwende muwakamate ombaomba waiovaa masuti wakiruka na ndege wakiomba na kufichwa Uswazi. Acheni ushamba siku moja mtakujapigwa zongo shaui yenu.”
Kijiwe kilicheka na baadaye kutaka kulia baada ya kushuhudia unafiki wa ajabu. Bila kungoja, Msomi Mkata Tamaa aliamua kumwaga falsafa akisema; “Mmeona unafiki wa mwaka, ombaomba wenye masuti waliamua kuwatimua ombaomba wa manyang’unyang’u ili wasiaibike wakati ombaomba ni ombaomba hata awe na suti, msuli au rubega.”
Alibwia tangawizi yake na kuendelea; “Hakuna ombaomba anayeheshimika hata ajidanganye vipi. La msingi ni watu kutumia akili na kuinua maisha ya jamii zao badala ya kutumia makalio kufikiri kuwaibia na kuwageuza wenzao mabwege.”
Kabla ya kuendelea Mbwa Mwitu keshadandia; “Hivi kuja kwa Obamiza kunabadili ukweli kuwa kaya yetu ni bomubomu na inayoishi kwa kutegemea njuluku za kubomu na kusaidiwa?”
Leo ni bandika bandua. Mpemba naye anakatua mic; “Yakhe mwadhani msipobadilika kuja kwa Obamiza kutawabadili au mtaendelea kuumia. Angalia alivyofunga barabara zenu bila kujali kuwa hii inaathiri uchumi na maisha yetu.”
Mkata Tamaa anaamua kuchomekea; “Who cares kama hamna watu wenye akili kuwatetea? Wao wakienda kule kubomu wanapokewa kwa mlango wa uani na wala hawaonyeshwi hata kwenye vyombo vya umbea vya kule.”
Kapende kapata upenyo; “Hali ni kinyume kayani, wachovu wanashobokea kujipendekeza na kujidhalilisha ili njuluku ya kupeleka Uswazi iongezeke hata kwa gharama ya kuwatosa wachovu.”
Anakamua coffee yake na kuendelea; “Sijui kwanini watu wanapenda kufanya vitu kama vile hawana ‘common sense’, au wanatumia ‘uncommon sense’ kama common sense?” Kapende anavyokanyaga kimombo kila mtu anamwangalia mwenzake na kutabasamu kuona kijiwe kinavyogeuka chuo kikuu kama kile cha Manzese.
Anaendelea; “Kwanini hawataki kukubali kuwa alipokuja bwana mkubwa walijidhalilisha hadi kufanya kaya isikalike? Imefikia mahali walevi tukajiuliza: Obamiza anakuja kuchukua kaya nini?” Kijiwe hakina mbavu.
Mzee Kidevu naye hajivungi. Anakwanyua mic na kulonga; “Hivi hawa ndata na ndutu wetu wa kazi gani? Wanalipwa njuluku za nini tena wakila na kunywa dezo wakati hawaaminiki wala hawawezi kumlinda mtu mmoja na msafara wake?”
Msomi kapata nafasi tena ya kumwaga falsafa. Anaangalia hadhira yake huku na kule na kusema; “Nashangaa uwezo wa kufikiri wa akina Njaa Kaya. Je yeye si rahisi? Akienda kule haendi na zana zote za maangamizi na mibomu yote hii? Rais anakuja kutembea na ndege 56 za kimaangamizi, magari 14 na makachero mia kidogo. Au anakuja kuchukua kijiwe?”
Kabla ya kuendelea, Mbwa Mwitu anaingilia; “Thubutu. Akija hapa tunamtuliza na kahawa na anaondoka na kuacha kijiwe ngangari kama kawa. Nadhani akitaka anaweza kuchukua kijiwe cha ngunguri wanaobomubomu na kujikomba kwake.”
Msomi anachomekea; “Kitu cha kwanza, baada ya kusoma makandokando ya ziara ya Obamiza nilijiuliza kama itifaki inaruhusu. Hivi mnadhani ungekuwa wakati wa Mchonga, huyu jamaa angekuja na mibomu na miefubiai yake kutudhalilisha kama sasa?”
Kabla ya kuendelea, mzee Maneno anachomekea; “Msomi naomba nikupinge hapa. Hapa wa kulaumu si Jadwong bali wenyeji wake walioamua kumfunulia kila kitu.”
“We achia hapo utaua.” Mbwa Mwitu anachomekea na kuacha kijiwe hakina mbavu.
Msomi anaendelea kupeta; “Nadhani tatizo letu kubwa lililoleta huu utegemezi ni ile tabia ya kutokujiamini na kuamini katika uombaomba na kujikomba.”
Kabla ya kuendelea mgosi Machungi anakatua mic; “Mie mwenzenu niipoona tinavyopeekeshwa niliamua kumhamisha bi mkubwa. Maana huwezi kujua kama efubiai wanaweza weekeza huko.” Kila mtu hana mbavu jinsi Mgosi anavyohami ulaji wake.
Wakati tukivunjika mbavu, Mipawa anaamua kutuumiza zaidi; “Da hao jamaa wanaovaa miwani ya mbao nyeusi sipati picha waswahili wangapi watajifanya nao ni Wamarekani. Nahofia magaidi nao watakuwemo.”
Anabusu kashata na kuendelea; “Je, jamaa zangu wanaosingiziwa kujilipua watapona? Nadhani La-kaatare atakuwa na hali ngumu kuliko Mgosi anayehofia kuibiwa bi mkubwa. Jamani eh Michele aka Miwali Obamiza bomba. Umeona akina mafestiledi walivyojipendekeza?”
Mzee Maneno naye anavaa daruga na kudema; “Jamani eh, bi mkubwa Mchele na Obamiza si noma ila majamaa yake na wenyeji wao wanaofanya vitu kama machizi. Wanasahau kuwa ataondoka na maisha yataendelea!”
Mbwa Mwitu anachomekea; “Haya jamaa ni madhalilishaji eti yamemuwekea ngumu Obamiza kugusa hata chakula chetu! Sasa ugeni uko wapi? Kama walikuja na mipiza yao basi hawakuwa wageni wetu bali wavamizi.
“Mwenzenu natamani na rahisi angeenda kule akazira mipiza akaitisha pilau na ugali wetu ili wajue nasi jeuri. Angekuwa Mchonga nadhani kichuli kingepelekwa Marekani.” Kicheko kwa sana tu.
Mipawa anaingia ugani; “Beng’we ina maana hata kuoga, kunyx sorry kunonihino ni kwenye eafosiwani?”
Mchunguliaji ambaye muda wote alikuwa akicheka na kusoma gazeti anaamua kuingia ugani; “Kama kila kitu anataka kiwe u-Marekanini basi angeenda zake Florida na kuigiza kuwa yuko kwenye kijua cha Bongo. Ajabu jamaa zangu watajisifu kuwa uchumi umekua kwa vile amekuja Obamiza kutubamiza!”
“Wehu hao watakaosema uchumi umekua wakati wamefunga anga, barabara, mitaa hata huduma zetu za kichovu. Wakati mwingine tujilaumu kwa kuendelea na kile wakameruni huita colonial hangover yaani ulevi wa ukoloni. Watu wanafanya vitu kama hawana ubongo. Who know? Maybe Masaburi at work.” Msomi anaamua kukandia kwa kimombo na falsafa ya kisomi.
Zile njemba siyo efubiai? Acha niishie kabla sijayafanyia kitu mbaya.
Chanzo: Tanzania Daima Julai 3, 2013.
No comments:
Post a Comment