How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Tuesday, 2 July 2013

"Wanaopinga Tanganyika walaaniwe"


MAKALA ya mwandishi George Maziku yenye kichwa cha habari “Wanaopinga Tanganyika walaaniwe’ iliyochapishwa katika gazeti hili toleo lililopita, haiwezi kupita bila kuweka mambo sawa.
Kwanza, hakuna haja ya kulaaniana, kuchukiana wala kudharauliana bali kujadiliana kwa hoja zenye mashiko na ushawishi. Pia hakuna wanaopinga kuwepo kwa Serikali ya Tanganyika bali umuhimu na gharama zake.
Nadhani mleta hoja ameshindwa kubaini ukweli uliojificha kwenye gharama. Maziku anaweza kuwa na hoja ila lugha na namna alivyoileta imepoteza hoja.
Pili, ni vizuri kufahamu kuwa kila Mtanzania ana haki kidemokrasia kutoa mawazo yake hata kama hatuyapendi.
Tatu, tukubaliane kuwa kuendeleza u-mimi wa kila upande na serikali yake ni upogo na unafiki unaofanya tuungane shingo upande. Kama tunalenga kuleta maendeleo kwa watu wetu, basi tunapaswa kuepuka gharama zisizo za lazima kama kuwa na serikali tatu.
Nne, tuzisikilize na kuzijadili hoja za wasiopenda kuwepo kwa Serikali ya Tanganyika. Nadhani ni hoja yenye mashiko kupendekeza kuwa tuunganishe nchi iwe moja badala ya kuwa na utitiri wa serikali ambao utambebesha mzigo mlipa kodi maskini wa taifa hili.
Ingawa mashabiki wa Tanganyika wanashindwa kuelewa kuwa wanachohitaji Watanzania si wingi wa serikali bali maisha bora, tusiwakatie tamaa. Tuwaelimishe. Naamini kuna siku wataelimika na kuelewa kilichoko nyuma ya ujio wa Serikali ya Tanganyika.
Tano, tutatoa sababu za kwanini Serikali ya Tanganyika si ‘big deal’ na hakuna mwenye kujua mahitaji ya Watanzania ambaye anaweza kuiunga mkono.
Sita, serikali tatu itaongeza gharama za kiundeshaji kiasi cha kuwakamua na kuwafanya Watanganyika wawe maskini zaidi, hasa ikizingatiwa kuwa ndio watakaokamuliwa pesa ya kuiendesha.
Saba, kama ambavyo imekuwa Serikali ya Baraza la Mapinduzi Zanzibar ambayo tangu kuungana imeendeshwa kwa pesa ya Watanganyika kutokana na ukweli kuwa Zanzibar haina vyanzo vya mapato ya kutosha kujiendesha kwa kiwango cha sasa.
Nane, ujio wa Serikali ya Tanganyika utaua Tanzania. Hii ni kutokana na ukweli kuwa sasa tutakuwa na Wazanzibari ambao hawajawahi kukubali kuwa ni Watanzania na Watanganyika. Je, hapa Watanzania watakuwa wapi kama siyo kubakia kwenye makabrasha na vitabu vya historia?
Tisa, kuanzisha Serikali ya Tanganyika ni kwenda kinyume na dhana na dhamira nzima ya Muungano ambao ulilenga kuwa na serikali mbili kuelekea moja, na si tatu kama watu wengi wasiopoteza muda kuisoma historia wanavyodhani.
Kumi, kutaanza kuwepo utoroshaji wa mali za Tanganyika kuelekea upande mwingine chini ya dhana ya urais na utaifa mpya. Nadhani wanaopendelea serikali tatu wanasahau kuwa tukishakuwa Watanganyika na Wazanzibari kikatiba, watu wa upande wa pili wataanza kufanya mambo kama ambavyo majirani zetu wangetaka kufanya kwenye muungano wa Afrika Mashariki - kila mtu kuchuma na kupeleka kwao.
Kumi na moja, licha ya kumfanya Mtanganyika kuwa punda kihongwe mwenye kubeba zigo la serikali utitiri na maskini, serikali tatu zitadhoofisha uchumi wetu na kuongeza kiwango chetu cha utegemezi kwa wafadhili.
Tujuavyo, watawala wetu wa sasa hawana mpango wowote wa kuwa na serikali inayojiendesha yenyewe bila kutegemea kuombaomba na kukopakopa. Hebu tujiulize. Kama deni letu linaumuka kwa kiwango cha kutisha kwa sasa chini ya serikali kubwa mbili tulizonazo, hali itakuwaje baada ya kuwa na serikali tatu? Nani anapenda kuendelea kuwa tegemezi jambo ambalo ni hatari kwa heshima, mustakabali na uhuru wetu?
Kumi na mbili, turejee kwenye makala ya Maziku. Anasema; “Ni jambo la kushukuru Mungu kwamba Tume ya Warioba imeheshimu maoni ya Watanzania walio wengi, waliotaka mfumo mpya wa Muungano wa serikali tatu kwa kuirejesha Serikali ya Tanganyika.” Si kweli kuwa wanaotaka serikali tatu ni Watanzania walio wengi. Kama wapo wengi basi watakuwa Wazanzibari au ni wa kubuni. Sijui Maziku anaweza kutwambia ni asilimia ngapi ya Watanzania wanaopenda kuwapo kwa serikali tatu na wasiopenda.
Hili ni hitimisho la haraka na jumla linalokosa umakini na uchunguzi wa kina. Pia ifahamike kuwa wingi wa wanaounga au kupinga ujio wa Tanganyika si hoja.
Hatuwezi kutumia falsafa ya ‘vox populi vox dei’, yaani wengi wape hata kama wamekosea. Mbona mwaka 1992 Watanzania wengi walipendelea kuendelea kuwapo mfumo wa chama kimoja kwa kukosa kusoma alama za nyakati, lakini busara za Mwalimu Julius Nyerere kujua kuanguka kwa ukuta wa Berlin zikatumika kuwasikiliza wachache?
Tungekuwa kila siku tunasikiliza wengi hata kama hakuna ushahidi, basi kuna mambo mengi ya kijinga yangepitishwa kama ilivyo kwa sasa bungeni ambako wabunge wengi ni wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na hupitisha vitu vya hovyo kwa wingi wao. Hivyo, tungeshauri tujenge hoja na kujadili hatima ya taifa letu kwa kuangalia mahitaji ya wakati badala ya zana chovu na za kizamani kama wengi wape.
Japo Maziku ameongelea mengi kama ukubwa wa serikali, kwa nukta hizi kumi na mbili tuhitimishe mjadala kuwa hakuna haja ya kulaani wanaopinga uwepo wa serikali tatu. Tuwasikilize, tujibu hoja zao kwa hoja zenye mashiko tukizingatia uwezo wetu wa kiuchumi na utashi na ‘spirit’ ya kuungana kwa Tanganyika na Zanzibar. Tunashauri akina Maziku wajitenge na hukumu za jazba na jumla. Mara nyingi huua hoja tena zinaweza kuwa za msingi.
ChanzoL Tanzania Daima Julai 3,2013.

6 comments:

Jaribu said...

Hao wengine wanashabikia mambo wasiyoelewa. Wanavyoponda hoja ya gharama utafikiri wana hela ya ziada. Ni kama mtu anayeshindwa kubalanca check book yake lakini kila siku ananunua vitu vya kifahari. Waweke serikali moja tu, kama Zanzibar hawataki, (kama anavyosema Mugabe) wajinyonge.

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Jaribu usemayo ni kweli. Ni bahati mbaya kuwa nchi yetu inasifika kwa mingoma na kupenda send offs ukiachia mbali kuwekeza kwenye glossaries na short-time guest houses. Kesho usishangae kusikia Kikwete akijinakibu kama mjinga mwingine aliyewahi kusema kuwa ukiona Clinton kaja ujue uchumi unakuwa. Nadhani atasema sasa uchumi unapaa.

Mtwangio said...

Mhango nakuomba tafadhali unielimishe au uniwekee wazi yale nisiyoyajua katika hatua ya juu kabisa katika huu unaoittwa muungano wa Tanganyika na Zanzibar mimi mwananchi wa kawaida wa tanganyika.

1-Ni madhara gani ya kitaifa ambayo yatayakumba nchi ya Tanganyika endapo watanganyika wataukataa muungano na kutaka warudishiwe nchi yao?

2-Je ni madhara gani ya kijamii au kiuchumi ambayo nchi ya Tanganyika itayapata watapouvunja muungano?

3-Uonikwa kuung'ang'ania huu muungano kuwepo kwake ni kwa masilahi ya wanasiasa wa pande zote mbili na kwa nini tuendelee kuyalinda masilahi yao hayo kwa kuung'ang'ania huu muungano?

4-je kuna sheria yoyote ya kimatifa au uhusiano wa kimataifa sisi watanganyika tutakuwa tumekiuka sisi watanganyika endapo tutauvuja huu muungano?

5-Ni uhakika gani wa mabadiliko ya maendeleo na mafanikio ya mwananchi wa Tanganyika ambayo atakayoyapata kwa kuendelea kuungana na Zanzibar ambayo ameyakosa katika kipindi chote cha muungano wetu zaidi ya kunyanyasika kiana na kubeba msalaba wa wananchi wa Zanzibar?

6-Kwa nini tumekuwa wanafiki wa kisiasa kiasi hichi na kuoneana haya au huruma kwa kuendelea kutetea masilahi ya watu wachache kabisa viongozi,wanasiasa na wafanya biashara watokao Zanzibar.

Mhango,tukiuvunja leo huu muungano naamini kabisa watanganyika tutakua tumejitua mzigo ambao umetuelemea kwa miaka yote hii ya muungano na kupumua kabisa kwamba jinamizi na kabusu ambalo limetuelemea kwa miaka yote hiyo limetutoka.Tukiuvunja leo muungano na watanganyika tukairudisha nchi yetu utaona tu kwamba wazanzibari ambao ndio wanafaidika na nchi yetu ya tanganyika watauomba uraia wa tanganyika kama awana akili kwa sababu masilahi yao na uhai wao utaitegemea Tanganyika kwa kila upande nakumbuka Mwalimu Nyrere moja katika hotuba yake aliwahadharisha wazanzibari ambao wanaotaka kuvunja muungano akisema "je mnaweza kununua nyanya(tungule)kwa pesa ya kigeni?"Ni nyanya Mhango ambayo Mwalimu Nyerere aliitolea mfano kwa maana mengine wajaze wenyewe.

Sasa kuongelea serikali moja,mbili au tatu na nani abebe nini au kipi ni kuturudisha nyuma sisi watanganyika mabao tunaoitaka nchi yetu irudi katika mikono yetu kwa kujivunia uraia wetu na nchi yetu.Je ni uoga au hofu gani ambayo tuliyokuwa nayo sisi watanganyika kwa kutoitaka nchi yetu irudi mikononi mwetu?Mhango naomba unielimishe uenda nimejingikiwa kile ambacho nisichokijua katika faida ya muungano huu kwa mtanganyika.

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Mtwangio nitajaribu kujibu maswali yako kwa kadri ya uoni na uzoefu wangu. Kuhusu madhara tutakayopata baada ya kuvunja muungano ni kwamba hakuna madhara bali neema kwa vile hatutaendelea kuwalisha watu wa visiwani.
Kama nilivyosema hapo juu, hakuna madhara ya kijamii wala ya kiuchumi endapo watanganyika wataamua kuvunja muungano. Sana sana watafaidika na kuondokana na nchi yao kutumika kama kiota cha wazanzibari kuja kuzaliana na kufaidika wakati wao wakiitwa machogo waendapo huko. Kiuchumi kuna madhara chanya ambayo ni kuepuka gharama za kuendesha kipande cha nchi kisicho na mchango wowote kiuchumi kwenye muungano. Chukulia mfano wazenj wanavyopata umeme wa uhakika toka bara wakati bara ni mgao kwenda mbele.
Wale wazalendo ambao si wanasiasa wana haja ya kuuchukia na kuukataa muungano. Njia rahisi ya kuvunja muungano ni watanganyika kutaka iwepo serikali na nchi moja. Upande wa pili hautakubaliana na hili hivyo utaamua kujiondoa wenyewe na zigo tutakuwa tumelitua kirahisi. Hii ndiyo mantiki yangu ya kupinga serikali mbili au tatu. Ni kuendelea kututwisha zigo.

Hakuna sharia yoyote ya kimataifa au uhusiano wa kimataifa itakayo kuwa imekiukwa kwa kuamua mstakabali wa taifa letu. Mbona muungano wa Senegambia ulivinjika na kila mtu akaenda kivyake na hakuna kesi iliyofunguliwa. Muungano ni kama ndoa. Ukiona haina maslahi mnatimuana kila mtu anakwenda kivyake.
Kuendelea kuibeba Zanzibar chini ya kiini macho kiitwacho muungano kutaendelea kumtesa mtanganyika kwa kuwabeba wazenj. Hivyo, njia ya kutua zgo ni kuhakikisha tunavunjia mbali muungano au kuunda nchi na serikali moja. Atakayeona au kuhisi anamezwa basi ajiteme nasi tuendelee kivyetu nao kivyao. Simpo.

Nadhani linapokuja suala la unafiki, pande zote ziko hard-wired with hypocrisy. Ukisikia wanapiga kelele unadhani wanawapenda watanganyika. Hata huyu Warioba na akina Shivji hawana lolote bali kutetea maslahi binafsi ya kisiasa. Nchi ombaomba iliyoshindwa kujiendesha ikiwa na serikali mbili inaongeza ya tatu ili ifanywe nini kama siyo kuendelea kubakwa na wanaotupa vijesenti kwenye kofia na kopo la omba omba huyu? Watawala wanapenda watanue wigo wa kuomba ili wapate ten percent nyingi huku wananchi wakizidi kuteketea. Who cares?Muungano hauna tofauti na biashara ya utumwa ambapo watanganyika wananyonywa kwa maslahi ya kipande cha ardhi kisicholingana na hata wilaya moja ndogo ya Tanganyika. Tuukatae muungano unaozidi kuzalisha matatizo na kuwanyonya upande mmoja kwa ajili ya kuneemesha upande wa pili. Ngoja ifike 2015 utawasikia wakisema bila aibu kuwa ni zamu yao sasa kuwa na rais wa muungano. Shame on them!
Nadhani kwa ufupi nimejibu maswali yako ndugu yangu Mtwangio. Kila la heri tuzidi kuelimishana na kuwaelimisha wengine.

Mtwangio said...

Mhango najua wazi una mengi ya kukushughulisha na pia kuwatumikia wasomoja wako.Ningeomba tu kukuuliza kama ifuatavyo siku ya jumapili julai 7 nilipost comment yangu kuhusu kutoa shkurani zangu za kunijibu maswali yangu na niliendelea pia kuchangia mawazo yangu kuhusu swala hili la muungano lakini hadi niandikapo comment hii sijaiyona comment yangu kutolewa je kuna lolote ambalo hukuridhishwa na comment hiyo hata ukaamua kutoitoa?Ninaavyokujua kutokana na maadili yako ya kazi sidhani kwamba wewe ni katika wale ambao mwenye kuwaziba midomo wasomaji wako kutopayuka pale ambapo panastahiki kupayuka.Pia najua ni haki yako kuitoa au kuifuta comment yoyote ile ambayo huridhiki nayo kwa vipimo vyako lakini sidhani kama kulikiuka na chochote kile katika maandshi yangu na kingine nilichokiona ni kupunguza baadhi ya fikra au kuzikata katika badhi ya comment zangu naomba tafadhali unielimishe makosa yangu nisije nikawa mwenye kuyakariri mara kwa mara ahsnte.

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Ndugu yangu Mtwangio. Kwanza pole sana kwa kutoona meseji yako. Ni bahati mbaya hata mimi sikuiona. Hata kama kungekuwa na jambo ambalo sikubaliani au sikupendezwa nalo nisingeifuta zaidi ya kuijibu. Nadhani baada ya kuweka mfumo mpya ambapo junk zinakwenda moja kwa moja kwenye spam huenda meseji yako ilitupwa kule na mfumo. Ni bahati mbaya sana kuwa kwa siku napata junk za hata kirusi na kichina zaidi ya 100. Na ninapofuta junk huwa siangalii. Hivyo nitajitahidi kuwa napitisha jicho kabla ya kufuta. Kumradhi sana ndugu yangu kwa hilo.