Nyingine ni ile hali ya kuweza kuvamia viwanja vya watu na kuvifanya vyake. Tatu ni ile tabia yake ya kudharau amri za mahakama, si mara moja wala mbili.
Nne ni ile hali ya kuwa chambo kinachosemekana kutumiwa na mtoto wa kigogo mmoja mwenye madaraka ya juu nchini, ambaye muda si mrefu ataanikwa hadharani ili historia baadaye imuhukumu ipasavyo ili liwe somo kwa wengine.
Kisena huyu ni mtata kweli kweli kama alivyoibuka kupitia utatanishi. Sijui kama huyu Bob ndiye Jokala aliyefukuzwa Mirambo Sekondari kwa usaliti au yule Jokola wa Nsumba Sekondari kule Mwanza.
Sijui kama ni huyu huyu Kisena aliyedaiwa kuwanyonya wakulima wa pamba Kanda ya Ziwa au yule aliyedaiwa kupewa upendeleo wa kusafirisha mahindi kutoka Mkoa wa Ruvuma kwenda Arusha.
Sijui kama ndiye huyu huyu aliyeumbwa na mwanasiasa mmoja wa upinzani aliyewahi kuvuma kwenye eneo la Kanda ya Ziwa huku akinawirishwa na waziri wa zamani toka mkoa mmoja wa kati mwenye kukumbwa na kashfa ya kubaka.
Sijui ni huyu huyu Kisena aliyekuja kufunga ndoa na waziri mmoja wa zamani toka jimbo mojawapo la Jiji la Dar es Salaam wakashirikiana kwenye unyakuzi wa UDA?
Na mwisho sijui kama ni yule yule aliyefunga ndoa na mtoto wa kigogo (…) kama inavyosemekana.
Je, Bob huyu huyu ndiye mwenye jeuri ya fedha hizi kiasi cha kudharau hata mahakama au ni chambo tu wenye mali wamejificha nyuma yake?
Kuna haja ya kumtafiti huyu jamaa tuone hiyo pesa aliyonunulia UDA kaipata lini na wapi na kwa njia ipi!
Tatizo la taifa letu kwa sasa ni kuendekeza mfumo wa kijambazi ambapo wenye madaraka, wake zao, watoto wao, hata marafiki zao wamebariki jinai.
Mtu hajulikani anakotoka, kisha anakuwa bilionea na hakuna anayehoji kama ni jambazi, muuza unga, fisadi, mfanyabiashara halali au kibaraka wa wakubwa!
Nani atahoji iwapo wanufaika ndiyo wenye mamlaka? Je, mamlaka yao yakikoma watajificha wapi? Je, kila mkubwa ajaye atakuwa rahisi na fisadi wa kuwalinda kama walivyolindwa wale waliopita?
Kisena amenikumbusha kisa cha Giriki mpumbavu aliyewahi kutamba kuwa serikali ya awamu ya kwanza ilikuwa mfukoni mwake. Baada ya baba wa taifa Mwalimu Julius Nyerere aliyesifika kwa usafi na ulevi wa maadili kupata habari zake kwenye vyombo vya habari kutokana na tabia yake ya kujisomea na kuandika na si kusomewa wala kuambiwa, aliamua kumuita na kuhoji ukubwa wa fuko lake linaloweza kumeza serikali nzima.
Nyerere hakumkawiza. Alimfurusha Giriki mpumbavu na limbukeni bila kujali kama alikuwa mwekezaji au mchukuaji. Huu ndiyo ulikuwa mwisho wa stori ya Giriki huyu mwenye majivuno.
Tukija kwa Kisena anayeweza kudharau amri ya mahakama, tunashangaa ni kwanini Rais Jakaya Kikwete hajasoma habari yake. Je, ameisoma au bado kweli hajaisoma? Je, rais wetu hasomi magazeti? Hata mashushushu wake?
Je, amesoma au kuambiwa akaamua kuminya kiasi cha kuacha mhimili mmojawapo wa dola udharauliwe jambo ambalo linainyang’anya serikali yake uhalali licha ya kuidhalilisha, kumdhalilisha rais na taifa zima kwa ujumla?
Je, serikali yake iko kwenye fuko la Giriki huyu wa Kiswahili? Je, inakuwaje wananchi waendelee kushuhudia kufuru zake wasichukue hatua?
Amejipatia UDA kwa bei ya kutupwa huku umma unaangalia kana kwamba UDA si mali yake.
Je, nani anampa kiburi Kisena? Ni mkuu gani au mtoto hata jamaa yake? Je, Kisena ni kuwadi ilhali wenye mali kiasi cha kudharau mahakama ni wakubwa wasiopenda kujulikana?
Ukidharau mahakama (contempt of the court) unatenda kosa la jinai ambalo huadhibiwa kisheria. Je, ni kwanini mahakama imenywea? Je, kwanini serikali imenywea? Je, inatoa picha gani kwa wengine wenye fedha au mahusiano na wakubwa mafisadi kama katika sakata hili? Uko wapi utawala wa sheria?
Anatumia polisi kulinda uvunjaji wa sheria. Rejea maneno ya ofisa wa juu wa polisi wa kituo cha polisi cha Chang’ombe: “Hivi nyie mnajua UDA ni ya nani? Mnataka kuhatarisha ajira yangu, kama Nchimbi ameng’olewa, mimi ni nani?” Je, kwa kuhoji watu kama huyu mkubwa wa polisi aliyejitetea kuonyesha utata wa mhusika hawezi kubanwa akaeleza anachojua juu ya nani anamilki UDA kwa sasa?
Je, ni kwanini watu kama hawa ambao wamenukuliwa na vyombo vya habari wanaachwa bila kuhojiwa ili kusaidia kutatua kitendawili hiki? Ajabu Takukuru bado wako kimya hawataki kuingilia kana kwamba hili haliwahusu!
Japo taifa letu kwa sasa lina uhovyo wake kama vile kuzidi kuongezeka kwa ufisadi, bado hatukupaswa kujiruhusu kufikia kiwango hiki. Kuendelea kushuhudia Kisena akidharau mahakama ni kuwapa wengine kama yeye kuidhalilisha tena na tena huku wakipoka haki za wananchi jambo ambalo linaweza kujenga ustaarabu wa wananchi kujichukulia sheria mkononi kama ilivyotokea hivi karibuni kule Kanyama, Mwanza ambapo Mwenyekiti wa zamani wa CCM wa Mkoa wa Mwanza aliuawa kinyama na wananchi wenye hasira.
Ni rahisi kufika kule hasa tukiendelea kuwafumbia macho watu wachache wanaojiona wako juu ya sheria kutokana na uswahiba wao na wakubwa.
Tumalizie kwa kuitaka serikali iige mfano wa Mwalimu Nyerere wa kumkamata Giriki na kumfurusha. Mahakama nayo isingoje kutetewa bali iamke na kusimama kwa miguu yake hasa ikizingatiwa kuwa huitwa ‘extra debito judiciae’, yaani chemchem ya haki.
Chanzo: Tanzania Daima Jan., 13, 2013.
4 comments:
Huyo jamaa sidhani kama ana ubavu wa kujifanyia mwenyewe anachotaka. Sitashangaa kama Dakta Mzururaji ndio yuko nyuma yake.
Jaribu umepatia maana aliyeko nyuma yake ni mzururaji mtoto ambaye ni bingwa wa kusaka ngawira kulhali. Ni bahati mbaya gazeti liliogopa kuandika jina la mtoto wa kigogo niliyekuwa nimemtaja kama RizONE.
Ala! Mhango una habari moto moto kama CIA! Uvumilie magazeti yetu haya, wanaogopa kufungiwa kama Mwananchi au kMwangosiwa.
Jaribu, Najua kila kitu ndiyo maana hata wanapochakachua habari zangu mie huchapisha orijinali hapa ili kuwapa wasomaji wetu uhondo wanaoukosa kwenye magazeti nyumbani.
Alluta continua tutaendelea kuwakaanga bila huruma.
Post a Comment