Ufuatao ni utabiri wa Shehe, Maalim,
Nguli, Ustaadh, Alhaj, Dk, Profesa Mpayukaji Msemahovyo njukuu wa Msemakweli wa
Waambie Waelewe katika kile ambacho wataalam wa nyota huita al khabar mutawatir.
Kwa taaluma yangu ya ilm al mubashir al
nujm al maarif na shams ul maarif al kubra na ilm huroof. Mimi ni nguli katika
sayansi iitwayo An-Najm uth-Thaqib na madude mengine mengi yenye majina magumu.
Kwanza, naomba msamaha kwa kuchelewesha
utabiri huu tofauti na mazoea. Kwani huu utabiri ulipaswa kutoka tarehe moja
Januari ila kutokana na udhuru haikuwa hivyo. Unaposoma utabiri huu ujue
unasoma kitu ambacho kiliandikwa mwaka jana kwa ajili ya mwaka huu.
Natabiri kuwa kutakuwapo ongezeko la
wizi wa mali ya umma a mbao utafutatiwa na ngurumo toka Karatu na kwingineko. Zile
ngurumo zilizokuwa zikisikika toka Kigoma, Arusha na Iramba zilikuwa ni
danganya toto. Ili kuepukana na mvua ya ufisadi na wizi wa mali na fedha ya
umma lazima ngurumo zisikike toka nchi nzima.
Natabiri pia kuwa kutakuwa na ongezeko
la ujangili na utoroshaji wa nyara na fedha za umma ughaibuni. Nyota
zinaonyesha kuwa mali hizi zitapelekwa India, China na Mashariki ya Kati.
Natabiri kuwa majangili wengi watakaoshiriki kuua na kusafirisha nyara hizi
watakuwa wageni wakishirikiana na wenyeji wakiwamo hata ndata na baadhi ya
maafisa wa serikali.
Kutakuwa na mafuriko kuanzia ya mvua
hadi bidhaa na dawa feki. Mafuriko haya licha ya kuathiri wengi yataua wengi
kama hatua za kuyadhibiti zisipochukuliwa haraka.
Natabiri kuwa atakufa kiongozi
king’ang’anizi wa muda mrefu upande wa kusini.
Natabiri kuwa kuna ndoa moja ya mkeka ya
kisiasa upande wa pili na ule mwingine iliyodumu kwa muda sasa itavunjika
kutokana nammoja wa wanandoa kuona muda umemuacha na nyota yake inazidi
kuchafuka kiasi cha kuhitaji kusafishwa.
Natabiri kuwa wanasiasa wataendelea
kuumbuka huku wale waliojiona wanaweza kutumia ujana wakiangushwa na wazee. Wale
wenye majina yanayoanza na Z, K, P na M wakae mkao wa kuadhirika. Hata chama
dume kitakuwa na wakati mugumu wa kumeguka na kuchakaa kiasi cha kunyang’anywa
tonge kama uchaguzi ufuatao hautahusisha uchakachuaji. Vyama vyenye majina
yanayoishia na M, F, I viko hatarini. Vyama vyenye majina yanayoishia na A vina
nafasi kubwa ya kufanya maajabu.
Natabiri kuwa kutakuwa na mgawanyiko
mkubwa kwenye vyama vyenye kuishia na F na M kutokana na ima kuchokwa kwa
viongozi wake au kuparaganyika kwao.
Pia natabiri kuwa kutakuwa na kashfa
nyingi zinazowahusu wake na watoto wa watawala zitafumka kiasi cha kutishia
mstakabali wa tawala za wazazi au waume zao.
Natabiri kuwa mwanasiasa mmoja mkubwa
mwenye cheo kikuu ataanguka na afya yake itazidi kuwa mbaya kiasi ambacho si
rahisi kujua nini kitakachofuatia kati ya kifo na uzima.
Natabiri kuwa waziri wa masuala ya
njululu atakufa baada ya kuugua muda mfupi tena akiwa ugenini akitibiwa.
Natabiri kuwa kutakuwapo ongezeko la
madudu kiutawala likiandamana na kutupwa watoto wengi mitaani.
Natabiri kuwa watazuka wagombea wengi wa
urais ima wenye utata na kashfa au wenye kutumia majina ya baba zao. Wengi
watakuwa na majina yanayoanza na herufi J, E, H na A. Hata hivyo, umma
utawakataa na kuwazodoa kwa vile hawana sifa yoyote zaidi ya majina ya wazazi
wao na tamaa ya kutaka kuufanya utawala kuwa wa kifalme wa kurithishana.
Natabiri kuwa gharama za maisha
zitapanda kiasi cha watawaliwa kuwachukia watawala huku vitendo vya
kujichukulia sheria mkononi vikiongezeka. Mawaziri wengi watazomewa kila
watakapoenda kufanya ubabaishaji kuanzia Mbeya kwa warusha mawe. Natabiri kuwa
kukutakuwa na ulannguzi mkubwa wa nishati kutokana na kuwapo kwa mikataba ya
kijambazi.
Natabiri kuwa wenye nyumba wengi
waliojaa mijini kwenye vibanda vyao watakimbilia mashambani na kuwaachia
wapangaji au kuuza kabisa. Kwa jiji la Dar es Salaam natabiri wenye vibanda
wataviuza na kwenda kujibanza Uzaramoni mashambani kutokana na ukali wa maisha.
Natabiri kuwa kutakuwa na ongezeko la
wasanii hasa wale wa kisiasa ambao mustakabali wao utakuwa mahakamani lakini si
kwenye vyama vyao.
Natabiri kuwa kutakuwa na ongezeko la
ndata kujihusisha na uvunjaji sheria kama vile utekaji magari, ujambazi hata
ujangili ukiachia mbali Jeiwii kuwaonea wachovu kwa kuwapiga wakigombea mambo
ya kipuuzi kama mabibi na kadhalika.
Nataibiri kuwa kutakuwa na mapigano
kwenye nchi moja changa ambayo yatasababisha vifo vingi na ukatili mkubwa
upande wa kaskazini.
Natabiri kuwa vyama tawala vingi
vitapoteza madaraka au kuwa na serikali zinazohusisha wapinzani.
Natabiri kuwa kiongozi mmoja wa juu
atatumia pesa nyingi kwenye safari zisizo na umuhimu kwa walipa kodi. Nyota
yake inaonyesha kuanza kufifia kiasi cha kuhisi kuwa anapaswa kuanza kutafuta
mahali pa kuwekeza iwapo lolote litatokea.
Natabiri kuwa mwaka huu utashuhudia
kuzidi kuzama kwa ilm kwenye ngazi zote kuanzia chekechea hadi vyuo vikuu.
Rushwa ya ngono na shahada za kughushi vitaongezeka huku ajira za kujuana
zikizidi kuongezeka pia.
Natabiri kuwa wasani hasa wanamuziki na
wachungaji wengi wanaotumia joho la sanaa na neno la Mungu watajikuta kwenye
kashfa za kusafirisha mihadarati.
Natabiri mgosi Machungi atahamia Ushoto
huku Mpemba akizamia Dar es salaam ili aongeze vitegemezi. Natabiri kuwa Kanji
atakwenda India na kukuta surprise ya mwaka ambapo bi mkubwa wake atakuwa
amemuongezea vitegemezi vitatu toka mtaani huku bi Sofi ataongeze mkorogo mpaka
aungue na kuumbuka. Natabiri Msomi Mkatatamaa atatangaza nia ya kugombea urais
mwaka 2015 kwa chama chake kiitwacho People’s Help and Development (PhD).
Natabiri kuwa wale wanaojigamba kuiweka
polisi mifukoni mwao, mifuko yao itapasuliwa na nguvu ya umma. Mipawa na
Kapende watatabiriwa baadaye.
Mnakaribishwa ofisini kwangu na utabiri
ni bure isipokuwa ukitabiriwa kifo unaacha hati ya nyumba, gari hata talaka ya
bi mkubwa.
Ofisi ziko Manzese mitaa ya kati nyumba
namba 666.
Chanzo: Tanzania Daima Jan., 15, 2013.
4 comments:
Umenivunja mbavu na huo utabiri wa Sofi na mkorogo. Nilikuwa nafikiri huyo Sofi ni hadithi lakini sasa nimeipata.
Jaribu,
Sofi yupo kwa sana na ni mama mwenye maulaji yake yatokanayo na kujua kuwahudumia wakware nao wakampa ulaji. Her real name is Sofia Lion kama ukiitafsiri kwa kimakonde.
Wakwere na Wazaramo ndugu moja, na siku hizi wameanzisha ujinga wa ukanda. Imekuwa nongwa siku hizi, "Sisi watu wa pwani hivi, sisi wa watu wa pwani vile!"
Tukirudi kwenye mkorogo, nisingekuwa na mambo mazito zaidi ya taifa, ningeaanzisha kampeni ya kupiga vitu mikorogo. Huku utajua mama wa Kiafrika kutokana na uso wake uliochubuliwa.
Ukitaka kuchukiwa piga kampeni dhidi ya nkorogo sorry mkorogo. Utaanzia wapi? Kama utawalenga akina mama wanaopaka utanoa. Ukiwalenga wanaume wanaowamotisha akina mama kupata mkorogo utanoa maana hawaupaki.
Kaka usiniponze. Nimesema anawahudumia wakware si wakwere hata kama nao anawahudumia. Hii falsafa ya upwani ni ujinga wa kawaida maana ukiangalia wanaojiita wapwani wanaishi bara na si pwani. Wengi hata kuogelea hawajui lakini wanajiita watu wa pwani. Hivi kweli Chalinze ni pwani? Na Lushoto je? Sitashangaa siku moja kusikia watu wa Morogoro wakasema nao ni watu wa pwani kwa vile ni kabila moja na wakwere.
Post a Comment