Kwa wanaokumbuka ndoa ya waziri mkuu wa
zamani Edward Lowassa na kampuni la kitapeli la Richmond lililosababisha
atimuliwe madarakani, hawana shaka kuwa ndoa hii haiwezi kuvunjika. Hata
ikivunjika, bado mirindimo na legacy yake haviwezi kumuacha Lowassa huru. Kama
kongwa shingoni, Richmond itaendelea kumuandama Lowassa hadi kaburini. Huu
ndiyo ukweli.
Hivi karibuni Shirika la Ugavi wa Umeme
Tanzania (TANESCO) liliomba Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA)
kuliruhusu kupandisha bei ya umeme kuanzia Januari 2014 na 2014 kwa kiwango cha
aslimia 40. Hii si habari njema kwa watanzania hasa wale akina yakhe ambao
mizigo ya utawala imeishawajeruhi vibaya sana. Binafsi niliposoma habari za
ulanguzi huu wa umeme, picha ya kwanza niliyoiona ni ya urais wa Lowassa
ukiyoyoma. Niliona ulanguzi huu kama msumari wa mwisho kwenye kaburi la Lowassa
kisiasa. Nina sababu za kuona picha hii.
Kwanza, licha ya kuwakumbusha watanzania
kashfa iliyosukumizwa chini ya busati ya Richmond, upandishaji bei za umeme
ambao kimsingi ni ulanguzi, unawakumbusha skandali nzima kama vile ilitendekajana.
Pili, kupandisha umeme, mbali na kuamsha
kumbukumbu za watanzania, kutaamsha hasira zao hasa ikizingatiwa kuwa akina
Lowassa, licha ya kujinadi kutaka kugombea urais, wanaendelea kuwakoga kuwa
urafiki wao na wenye madaraka si wa kukutana barabarani. Hii ndiyo siri ya
Lowassa kutofikishwa mahakamani hata baada ya kukiri kuhusika na Richmond. Rejea
alivyopewa kitanzi cha kujipima na kuamua na kweli akaamua kuachia madaraka
ikiwa ni ushahidi kuwa alihusika vilivyo na kashfa hii.
Wapo wanaokwenda mbali na kusema kuwa
Lowassa hakupenda kuwajibika. Kilichomsukuma ni kunusuru serikali ya rafiki na
mshirika wake rais Jakaya Kikwete.
Pili, ni kuepuka yasifumuliwe mengi
ambayo mwenyekiti wa Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza kashfa hii Dk Harrison
Mwakyembe alisema kuwa kama wasingeficha baadhi ya mambo nchi isingetawalika. Na
kweli, baada ya akina Mwakyembe kuficha waliyoficha walipewa vyeo kama malipo
ya fadhila. Samuel Sitta, spika wa bunge aliyeanzisha mchakato ule
alinyamazishwa kwa kupewa uwaziri sambamba na Mwakyembe huku mjumbe mwingine
Stella Manyanya akipewa ukuu wa mkoa.
Japo kugombea urais ni haki ya kila
mtanzania, kuna haja ya wale wanaotaka kufanya hivyo kujipima. Leo tutatoa
ushauri wa bure kwa Lowassa kuwa anafaa kujipima na kufanya maamuzi magumu
ambayo ni kuachana na ndoto za urais. Sidhani kama watanzania waliwahi
kumsamehe kwa harasa na karaha aliyowatia. Maana huu upandishaji holela wa bei
za umeme ni matokeo ya kazi ya mikono ya Lowassa na wenzake aliowafia msalabani
ili kuwakoa.
Bahati nzuri Lowassa amekuwa bingwa na
mwalimu wa kuwaambia wenzake wafanya maamuzi magumu. Naye anapaswa kufanya
maamuzi magumu hayo hayo kwa kuwekeza kwenye kujisafisha au kueleza ukweli na
kuomba msamaha badala ya kuotea urais akidhani watanzania watakuwa wepesi wa
kusahau hivyo.
Kimsingi, mzigo wa ugumu wa maisha
utokanao na ulanguzi wa nishati unaowakabili watanzania kwa sasa una mkono wa
Lowassa. Lowassa hawezi kukwepa lawama ingawa amekuwa akijtahidi kujisafisha
kwa kutoa matamko yanayoonekana kuwatetea wanyonge ukiachia mbali kumwaga
mamilioni ya shilingi ambayo haelezi alivyoyapata. Wapo wanaoona kuwa
anachofanya Lowassa ni sawa na kumuua samaki halafu ukatumia minofu yake
kuwalisha samaki wengine. Tofauti ni kwamba fedha anazomwaga Lowassa zinatokana
na hao hao anawapa. Mwalimu Nyerere aliwahi kusema kuwa ukiona mtu anawanunua
wenzake jua naye amenunuliwa. je ananunua nini kama siyo kujenga mazingira ya
kujilipa baada ya kupata madaraka ambayo yamegeuka biashara kubwa yenye
kutengeneza utajiri haramu haraka? Natamani Lowassa ajitokeze na kukanusha
madai yangu ili nimuumbue zaidi. Najua hatafanya hivyo. Kama kawaida yake,
atasoma na kupuuzia akidhani tatizo litajiondoa, ataendelea na umbuni wake
ambaye huona adui akaficha kichwa mchagani akidhani na adui atafanya hivyo wakati
siyo.
Wanaompenda
na kumtakia mema Lowassa wanamwambia wazi wazi kuwa hafai ingawa hapendi
kusikia ukweli huu: Achana na urais na ashukuru Mungu kwa rafiki yake
kumwepusha na kesi mahakamani. Je watanzania ni wasahaulifu au mataahira hivyo
wamzawadie mtu aliyewaingiza kwenye matatizo kama yeye? Ni ajabu kuwa Lowassa katika matamko yake ya “kuwatetea”
aliowanyonga na kuwateketeza kwenye dili la Richmond haongelei ufisadi na ulafi
unaoangamiza taifa letu. Nadhani kama Lowassa anataka kuwatendea haki wanyonge,
basi ajadili mambo muhimu hasa ufisadi, wizi, rushwa, kulindana, kujuana na
mengine kama hayo. je anao udhu wa kufanya hivyo? Thubutu!
Japo Lowassa amekuwa akiwalaumu maadui
zake kuwa wanahujumu mipango yake ya kumrithi rafiki yake, anapaswa kujilaumu
na kukubali ukweli kuwa alichofanya hakiepukiki. Kama kuna mtu ameamua
kumuumbua Lowassa na kuzamisha ndoto zake za kuwa rais si mwingine bali
aliyetoa wazo la kupandisha/kulangua umeme hasa kipindi hiki tunapokaribia
uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.
Lowassa si kwamba hafai tu kugombea
achia mbali kuwa rais, hata atakayemuunga mkono atamponza. Japo ana mtandao
mkubwa, sambamba nao anayo dhambi kubwa ya kuhujumu watanzania kwa kuwaingiza
kwenye matatizo yasiyokwisha ya mgao na ulanguzi wa umeme wa kila mwaka. Ana
mzigo wa kusababisha maisha magumu kwa watanzania. Maana unapopandisha bei ya
umeme unasababisha kila kitu kipande kiasi cha maisha ya watanzania wa kawaida
kuzidi kuwa magumu. Kinachofanya dhambi ya Lowassa iwe kubwa zaidi ni ile hali ya
yeye kuendelea kutesa akimwaga mamilioni ya pesa huku watanzania wakifa kwa
magonjwa yanayozuilika na ambayo serikali ingeweza kuyatokomeza kama si
kuruhusu madudu kama Richmond ukiachia mbali mengine kama IPTL. Lowassa hana pa
kukimbilia. Ataendelea kuandamwa na jinamizi la Richmond linalosababisha maisha
ya watanzania yazidi kuwa magumu na kukosa maana.
Kwa machache haya, je pamoja na kupanda
na kulangua umeme Lowassa bado ana ndoto ya urais? Je watanzania watakubali
kuchagua mtu ambaye alishawaumiza ili awaumize zaidi?
Chanzo: Tanzania Daima Jan., 15, 2013.
2 comments:
Namna mojawapo ya kuwatala watu ili nchi isiwe na maendeleo nikuwa wafanya wananchi wawe wajinga na washindwe kujitambua inawezekana huyu Bwana analijua suala vizuri na kwa sababu yupo ndani mfumo huo...
Basi hana shaka na hilo...Ukitaka uthibitisha angalia washabiki anaowapata katika hizo pilika pilika zake za ndoto alizosema hivi karibuni
Anon
Ni kweli ujinga na umaskini ni nyenzo nzuri za kutawalia. Ila kwa dunia ya kitandawazi na kitandawizi ya sasa ni tofauti. Hakuna kitu kitaibadili ramani ya siasa za Afrika kama simu za mkononi. Taratibu watu wetu wanaanza kuamka na kupata angalau taarifa.
Post a Comment