Wapendwa
wasomaji wa safu hii,
Kabla
ya kuwaletea nini ajenda na mjadala wa kijwe cha leo, tuonaomba kwa niaba ya wazee wa kijiwe na kwa unyenyekevu msamaha kwa kutokuwa hewani kwa
takribani mwezi. Tunawashukuru kwa utulivu na uvumilivu wenu. Maana kuna
msomaji aliniambia kuwa alikuwa na mpango wa kutangaza maandamano ya kutaka
kujua kwanini kijiwe hakikuwa kikitoka.
Mengi yalisemwa.
Wapo waliodhani kuwa tumekolimbwa au kunyamazishwa. Wapo waliomzonga mhariri
kutaka kujua kunani. Wapo waliosema nimekamatwa baada ya kukibandiwa kabla ya
kumwangosiwa au kumvungiwa na mambo mengine mengi. Wapo waliodhani kuwa Kanji
na Kanungaembe Sofia walitia mtima nyongo wasijue wachawi si wao bali wengine. Nawashukuruni
sana hasa msomaji wangu Shaddy Mijjinga ambaye alinisumbua na maswali kweli
kweli.
Kwa ufupi ni
kwamba wote tu wazima kuanzia mimi Mgosi Machungi, Msomi Mkatatamaa, Mbwamwitu,
mzee Mipawa, Kapende, mzee Maneno na mzee Kidevu na akina Mchunguliaji bila
kuwasahau ami Mpemba, bi Sofia aka Kanungaembe na dugu moja Kanji.
Pia n achukua
fursa hii kutoa rambi rambi kwa kufiwa na mzee Mandela ambaye bahati nzuri
nilihudhuria maziko yake ingawa kwa staili tofauti na wale mafisadi waliokwenda
kula kuku na kutalii. Wanakijiwe walinichangia uchache nikawakilisha na
rambirambi zao. Sitaki niseme makufuru niliyoshuhudia kule ambapo malaika alizikwa
na wenye dhambi kibao.
Tuyende ku nchito.
Kijiwe cha leo ni cha aina yake. Naona kama kawa mgosi Machungi anaingia akiwa
amevalia kanzu yake na kofia ya tarabushi.
Mpemba naye keshajaa tele kama pishi la mchele huku Kapende na Mipawa
wakiwa tayari ugani farasi kufungiana nyama na nyangwa.
Msomi kama
kwaida yake hakosi mabuku makubwa mkononi huku Mbwamwitu akiwa na bashasha
zake.
Mpemba
analianzisha, “Yakhe hebu tupe habari za safari yako kwa Madiba.”
Nakunywa kahawa
yangu huku nikijiweka vizuri kwenye benchi.
Nasema, “Kwanza
nawashukuru nyote kwa kuniwezesha kufika Sauzi. Licha ya kufikia J’burg kama
wao wanavyoiita Johannesburg nilifika kijijini kwa Mandela kule Mvezo. Ni kama
Butiama. Hakuiba wala kujenga makazi ya kifahari kama yale ya kijijini kwa Zuma
Nkandla. Sema kwa jina la Mandela na wema wake, bado Mvezo panaheshimika kuliko
hata hiyo Jo’beg.”
Mpemba
anachokemea, “Yakhe wataka sema paheshimika kama Nsata au Bwagamoyo?”
Msomi anadakia,
“Ami acha utani. Huwezi kulinganisha chawa na tembo. Huwezi kulinganisha pango
la wezi na hekalu la Mungu.”
Msomi anakunya
kahawa na kukatua kashata na kuendelea na kuchomoa gazeti la kikameruni toka
nchi jirani na kusema, “Umeona hiki kibonzo kinachoonyesha viranja wetu
wakiingia kwenye viatu vya Madiba na kupwaya?”
Kapende
anachomekea, “Hao pamoja na kumezwa humo aangalie wasivijaze vinyesi au
kuviguguna kama panya kama siyo kuvipiga mnada.”
Kijiwe hakina
mbavu isipokuwa Kanji na bi Sofi ambao walionyesha wazi kutopenda vimondo
vilivyokuwa vitupwa kwa walaji wa kaya.
Sofi
anachomekea, “Kwani mawazo ya huyo mchora vibonzo ni msahafu hadi yawe kweli?”
Mipawa anakwanyua mic haraka, “Ukitaka kujua
ukweli wa jambo uangaliage jinsi watu wanavyolipokea au kulipenda au kuliponda.
Hiki kibonzo kimeeleza ukweli ndiyo maana wengine unawachoma.”
Mbwamwitu
anadakia, “Unawachoma wapi?
Mipawa anajibu
kwa mkato, “Popote watakapoona unawachoma.”
“Yakhe mie naona
mambo ya kuchomana tuyaache tuongelee uaminifu na mchango wa Madiba ati.”
Nlisema kwa
ufupi kuwa Madiba hakuwa fisadi wala mpenda maulaji kama wengi wa waliomzika
toka barani kwetu.
Kwa vile
tulikuwa na mambo mengi ya kuzungumzia, tulirukia kwenye hali halisi ya mambo
kwenye kaya ambapo tunafunga mwaka.
Mgosi Machungi
anasema, “Wagosi naona tinafunga mwaka kwa mkuu kuendelea kuzuua kiasi cha
kutisha. Juzi tilimuona akienda kwa akina Bonjour, mara kwa Diba mara kwa Nyayo
sijui kwanini hajifunzi.”
“Ajifunze nini
wakati wanaopaswa kumshikisha adabu hawajifunzi?” Anajibu Msomi kwa kejeli.
Anaendelea, “Mie
naona tungeangalia hili la Mzigo sorry Mzito Kabwela kuonyesha makucha yake
asijue watayakata kabla hayajaparura.”
Mipawa
anadandia, “Mbona walishayakata kiasi cha mtu mwenyewe kuanza kuweweseka!”
Kapende naye
hajivungi, “Hakuna kitu kilimmaliza huyu limbukeni kama Chama Cha Mafisadi
kuonyesha eti huruma kwake. Wao ya Chakudema yanawahusu nini?”
Sofia anadandia,
“Kwani ni vibaya kumuonea huruma mtu hata kama ni adui yako?”
Kanji ambaye
alikuwa kimya naye anaamua kukatua mic, “Hapana baya Sofi. Naona chama penda
vatu diyo maana naona huruma kwa Bwela.”
Mzee Maneno
ambaye naye alikuwa kimya anaamua kuweka timu, “Ukiona hivyo jua lao moja. Si
nasikia walikuwa wakimlipa pesa nyingi ughaibuni ili aibomoe chakudema na
hajakanusha.”
“Kwa vile msimu
wa wanasiasa kusiasia urongo na kamba zao unawadia, tunapaswa kujiandaa kuona
mengi.” Alidokeza Kapende.
Mgosi naye
hakutaka kujivunga, “Nashauri mwaka ujao tijiandae kuwatia adabu wanaotaka
kutitumia kama majembe. Tihakikishe pesa ya ughaibuni inaejeshwa, kina Kagoda
wanakamatwa, mafisadi wanaojipitishapitisha wakihonga njuuku za wizi wanapigwa
chini na mambo mengine.”
Mipawa
anaingilia kati, “Tuazimiege kuwa mwakani badala ya kutwambia kilimo kwanza
watwambie mibwimbwi na kuficha njuluku nje kwanza.”
“Yakhe mie naona
mwakani iwe ni kamba kwanza ukweli mwisho. Hivi ile nguvu ya soda ya Mwakiwembe
ya kupambana na wauza bwimbwi nayo imeishi wapi?” Alichomekea Mpemba.
“Si ajabu hata
wale dagaa wa airport washarejeshwa kwa mlango wa nyuma au kuhamishiwa kwingine. Bongolalaland hii ati,” Anajibu
Mchunguliaji.
Msomi anadakia,
“Nadhani Mwaki naye ni mzigo kama Mizengwe, Mgimua, Chiizi, Milima na Hawa wana
Ghasia na wengine. Nadhani kama kungekuwa na uwezekano wa kuwachapa bakora hawa
jamaa ingewafaaa sana. Maana they are good for nothing so to speak.”
Naona bi Sofi na
Kanji wanaamua kukitoa baada ya kugundua kuwa vimondo vingi vinaelekezwa kwenye
genge lao.
Kwa ufupi ni
kwamba kijiwe kimepania kuja na ukali mpya mwaka mpya kuhakikisha wababaishaji
na mizigo wanapigwa chini.
Kikiwa kijiwe
kinanoga si mvua ikaanza kunyesha! You know what followed guys. Guess what.
Kila mtu alitimka kutafuta pa kujikinga.
Chanzo: Tanzania Daima Jan., 8, 2014.
No comments:
Post a Comment