Japo sina uhusiano mzuri na jamaa yetu Njaa Kaya kwa vile anajua
kichaa changu cha kupenda haki, nawaomba watu wa mjengoni watumie turufu
yao kuhakikisha napewa wizara ya Mali ya Siri na Utajiri wa vigogo ili
niinyooshe once and for all.
Naomba wanipe rungu nirejeshe heshima na usalama wa raslimali zetu
kwa vile ufujaji, wizi, ujambazi na ujangili unaoendelea usipokomeshwa,
kuna uwezekano vizazi vijavyo vikakojolea makaburi yetu kutokana na
kuvisaliti kwa tamaa za kipumbavu na ubinafsi vilivyopindukia.
Japo inaitwa wizara ya Maliasili na Utalii, kwa walevi hii si
chochote wala lolote bali wizara ya mali ya siri na utajiri wengine
huiona kama wizara ya mali ya siri na ujangili ambayo wengi
wanainyemelea ili wale bila kunawa tena kwa mikono miwili.
Hatuwezi kuendelea kuvumilia ushenzi huu. Lazima jinai hii ikomeshwe tena haraka na mara moja.
Kama nitapewa rungu, nitarejesha Loliondo na kuwakamata akina
Mhunidin Ndongala na wale wote walioshiriki na kushirikiana kuhujumu
taifa bila huruma wala kuangalia nyani usoni.
Sitanii wala kufanya sanaa kama wale wanasanii mliokwishawachoka.
Wala si fikra za kilevi na bangi. Walevi wanajua fika kuwa waliibiwa na
kutendewa jinai chini ya utawala kidhabu ulioruhusu ufisadi na ujambazi
mbuzi vianze kujichimbia kwenye kaya.
Hivyo, amini nawambieni wenye kusikia wasikie na wenye kuelewa
waeleve maneno haya ya unabii. Lazima Loliondo irejee mikononi mwa
walevi hata kama itabidi kunyonga watu.
Kwani, wao wananyonga wangapi hasa wanapoendelea kuchuma huku dhiki
zikiwadedisha walevi? Isitoshe wananyonga wanyama wetu hovyo hovyo na
kwa kasi ya kutisha kiasi cha wengine kama faru kuanza kutoweka.
“We can’t stay a side and look while our hunk is being raped by
evil’s and devil’s agents in the name of investment. How can we invest
in destruction as if we’re zombies and vagabonds?”
Ili kutimiza ahadi zangu, nitawahoji wote wanaotuhumiwa kuhusika na
ujambazi huu wa kuliangamiza taifa hata kama itabidi kumhoji mzee Ruxa
kwa kunyamazia ujambazi wa Loliondo.
Japo ana kinga, nitataka nimhoji anipe mantiki ya kuruhusu jinai
hii itendeke chini ya uangalizi wake kama hakuwa na maslahi yoyote.
Itabidi nipate maelezo ni kwanini wahusika waliruhusu huu ujambazi wa mchana kama kweli hawakuwa na maslahi binafsi?
Kwanza, nitahakikisha nalipa fidia kwa familia ya marehemu Stan
Katabaro aliyenyotolewa roho na ujangili na kumtangaza shujaa wa
utokomezaji ujangili hasa wa kiutawala na wale wote walioathiriwa na
ujambazi huu wa mchana. Hii itatoa motisha kwa walevi wote wanaojua
madudu na mbinu za watenda jinai hii kujitokeza na kunipa taarifa na
ushirikiano.
Pili, nitawahakikishia usalama wao na familia zao.
Tatu, nitahakikisha nataifisha mali za mawaziri na vigogo wote na
maajenti wao wanaosadikiwa kuigeuza wizara hii mali ya siri na ulaji.
Nne, nitamtimua mtoto wa mfalme wa kimanga ambaye alijinyakulia
Loliondo kupitia kwa mawakala wake washenzi waliokuwa na madaraka.
Wote waliopata vitalu na vibali kupitia rushwa au kujuana wakae
mkao wa kuliwa. Naapa kabisa. Sitanii wala sijaribishi bali kufanya
kweli. Kwani kama walevi tumechoka kugeuzwa mashahidi wa maangamizi yetu
na vizazi vijavyo.
Tano, nitahakikisha namtoza fidia huyu mmanga kwa muda aliotumia Loliondo bila kulipa kodi wala kufuata sheria.
Sita, nitahakikisha wale wote waliouza wanyama wetu nje wananyongwa hadharani mbele ya walevi.
Saba, nitahakikisha wale waliouza mahoteli yetu ya kitalii kwa bei
mchekea wakae mkao wa kuliwa. Wakae wakijua kuwa nikichukua ukanda
nitawanyongelea mbali na kuhakikisha mali zao zinataifishwa huku
nikibatilisha mikataba ya uuzwaji wa hoteli husika.
Nane, nitawasweka ndani vigogo wote wenye kulalamikiwa kupewa vitalu vya uwindaji kinyume cha sheria.
Nadhani akina Pio Msekua, War Kawawa and family, Andaaman Kinamna na Mood Sefu Khatib wananipata.
Najua mambo yao na jinsi ambavyo walitumia madaraka kujinyakulia vitalu.
Tisa, nitakomesha ujambazi unaoendelea ambapo vigogo wa wizara
huenda ughaibuni kutanua huku wakijilipa ‘per diem’ kwa kisingizio cha
kwenda kule kutangaza utalii.
Kumi, nitakomesha uwindaji haramu na ujangili kwa kuwaongoza walevi
kusimamia mbuga zetu za wanyama. Hata uwanja wa ndege na mipakani
nitajaza walevi na wavuta bangi ili waonyeshe wanavyoweza kufanya kazi
vizuri kuliko walevi wa ngawira.
Heri wangevuruga walevi kwa vile ni walevi kuliko washenzi
wanaoitwa waheshimiwa wakati ni wezi wa kawaida tu waliojificha nyuma ya
madaraka.
Kumi na moja, nitaendesha operesheni Tokomeza Ujangili kwa
kuwashughulikia majangili wote yaani wale wa mbugani na wa maofisini.
Sitakuwa na cha msalie Mtume wala nini bali kukamata tu. Pia
sitaruhusu kuingiliwa na kiumbe yoyote awe mdogo au mkubwa. Nikipitisha
uamuzi umepita. Atakayejiletaleta na cheo chake namuanika kwenye
magazeti ili jamii imjue. Wale ndata wanaotumia bunduki na magwanda yao
kufanya ujangili, wakae mkao wa kuliwa. Nitawakamata na kuwanyonga
sambamba na mabosi wao wanaowaachia watende jinai hii kwa walevi.
Wanadhani hatuwajui na jinsi migari yao inavyotumika kufanya ujangili kama wale waliokamatwa kule Mugumu?
Walevi wanawajua wao na mitandao yao. Wanajua kila kitu na wako
tayari kuhakikisha wahusika wote wanakamatwa bila huruma wala upendeleo.
Ifahamike wazi. Sitatoa muda wa watu kujipima na kufanya maamuzi
magumu. Nitafanya maamuzi magumu mwenyewe kwa vile mimi na walevi ndiyo
tunaokabiliwa na maisha magumu yatokanayo na maamuzi na tabia za
kipumbavu za baadhi ya watu kuuza mali ya kaya kwa manufaa yao binafsi.
Hii kaya ni yetu wote kwa usawa bila kujali cheo wala mitandao.
Kama nitaeleweka na kupewa rungu, aminini hii ndiyo saa ya ukombozi wa kaya hii na raslimali zake.
Lazima nirejeshe wizara ya Mali ya Siri na Utajiri kuwa ya Maliasili na Utalii na si ujambazi na ushenzi.
Nawatakieni heri ya Krismas na Mwaka Mpya wa ku fanya maamuzi magumu
Zikomo kwa mbiri.
Chanzo: Nipashe Jumamosi Jan., 4, 2014.
No comments:
Post a Comment