How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do
Saturday, 25 January 2014
Mlevi azidi kuing'ang'ania Katiba mpya!
Vulek’a amazulu,
Iyeza iyez’i Ngonyama
Kwancibilik’izintaba
Kwasha nemimfula
Lungis’indlela zakho,
Lungis’ukuhamba kwakho
Iyeza iyez’ i Ngonyama y’ amazulu
Kwa wasiokinyaka kizulu tafsiri hiyo hapo.
Funguka e mbingu,
Yu aja mfalme wa mbingu,
Milima sawazikeni
Na mito kaukeni x2
Nyosheni njia zenu
Nyosheni mapito yenu
Yu aja mfalme wa mbinguni.
Nilikuwa najiimbia wimbo huu wakati nikitafakari mambo mbali mbali. Niliimba wimbo huu kwa sana nilipokwenda kumzika Diba wa Madiba kule Sauzi.
Kwa vile mimi ni mkombozi japo sitoki mbinguni bali kwenye baa, niliona wimbo huu una mantiki sana. Mantiki yenyewe ni kutaka milima na mito yaani bara na visiwa visawazike na kukauka na kuunda kaya moja chini ya katiba moja mpya.
Wewe usomaye utume huu usome kwa sauti na nguvu. Uende uutangaze kwa walevi.
Usimame njia panda kwenye vilima na miinuko na kutangaza ukombozi wa kweli wa walevi.
Usimame kwa kujipiga kifua uutangaze utume huu uliopigwa mhuri wa alama ya mkuu wa walevi ukiwataka kila mmoja ajikomboe toka kwenye jinamizi liitwalo kupenda madaraka na kujilisha pepo.
Hata kama awaleteae habari hii njema ni mlevi, jua ni msomi ambaye hakughushi wala kupewa usomi wa heshima.
Nina shahada ya udaktari wa sheria ya Katiba yaani Constitutional Law PhD kwa lugha ya kimakonde.
Baada ya kugundua kuwa wapo walevi wanaopenda ukubwa kuliko walevi kwa kutaka eti tuwe na sirikali tatu na kaya tatu, nilitaka kumpigia simu Jaji Waryuba kumwambia asitishe majeshi yake.
Baadaye niliona nitampa ujiko. Hivyo, leo nimeamua kuja na pendekezo kuhusu Katiba Mpya ambayo si mzigo wala haina gharama kama hii inayopendekezwa ya siri kali mbili au tatu ambazo licha ya kuongeza mzigo kwa mlevi, inamnyima ujiko kiranja hasa wa muungano.
Walevi wamechoka kuendelea kunyonywa na kuishi kwa njuluku ya kudhalilishwa itokanayo na kuombaomba.
Wamechoka kuishi kwa pesa ya bangi na gongo ambavyo hupandishiwa kodi kila libajeti.
Wanataka ukombozi na mkombozi wao ni mimi aletaye utume huu wa ukombozi. Nasema wazi: Msikubali kuwa na serikali mbili au tatu hata Kaya.
Kama nyinyi ni wamoja kama msemavyo siku zote, fanya kitu kimoja-kuweni na kaya na sirikali moja.
Nilimsikia Waryuba akisema kuwa kama wadanganyika aka walevi watakaa rasimu yake basi wajiandae kuvunja muungano kwa kuzalisha sirikali nyingine ambayo itawaongezea kunyonywa na kudhalilishwa.
Nani anafurahia kunyonywa au kudhalilishwa hata kama ni mlevi? Huu si wakati wa kunyonyana bali kuonyana na kupeana ukweli mchungu hata kama unauma.
Wengi wameogopa kusema kwa vile watawaudhi wachache wapendao kula dezo tena kwa kunyonya damu ya wenzao. Mie sasa nasema: Enough is enough.
Tokana na utaalamu wangu wa uchumi na katiba nimekuja na simpo solution. Badala ya kumtwisha mzigo mlevi kwa kuanzisha utitiri wa siri kali za kilaji, nakuja nasema siri moja inatosha. Nani anapenda kuwa mtumwa wa siri tena kali? Nataka siri moja inayounganisha kaya mbili na sirikali zake mbili na kuunda siri kali moja lililoshikamana kulhali.
Nisemacho ni kwamba jamaa wa upande wa pili waliokuwa wakipewa ulaji wa dezo kama vile uishiwa hata uwaziri hawatakubaliana na hili la siri kali moja kwa vile itafichua siri kali yao ya ulaji vya wengine.
Hata hivyo, ieleweke kuwa kuunda siri kali moja chini ya kaya moja kutaondoa unafiki, ulafi, umimimimi na uwewewewe vilivyotapakaa ambapo walevi wanatwishwa mzigo bila sababu ya msingi.
Wanaopinga siri kali moja watakuja na sababu za kitoto kama vile kumezwa bila kukumbuka kuwa Danganyika ilimezwa kwa miaka 50 na walevi waliendelea kudunda na kula ugali wao huku wakiwamegea na wenzao wa upande mwingine.
Hakuna anayeweza kumezwa na kaya inayoundwa na majina mawili, yaani Tanga-nyika na Zenj.
Utamezwaje wakati kaya si mali ya yoyote bali pande mbili? Hivi kweli mume au mke anaweza kummeza mwenzake au wanakubaliana kumezana? Basi acheni utoto japo mara moja tufanye mambo ya kikubwa. Juzi niliwasikia Nambari Wani nao eti wakilalamika kuwa Waryuba alivuka mipaka.
Walitaka katiba na muundo wa kaya unaowanufaisha wao badala ya walevi siyo? Mshindwe na mnyong’onyee.
Hivi, kwa mfano, upande wa pili unaodai kumezwa mbona umekuwa ukimeza ubwabwa toka Ngeme bila kulalamika? Mbona kwa miaka yote umekuwa ukiwasha umeme wa Kidatu tena kwa gharama ya dezo wakati Wadanganyika wakilanguliwa umeme huo huo na hawakulalamika?
Changu kichungu chako kitamu siyo? Kwanini wasiseme kuwa wanahofia kupoteza nafasi za ulaji wa dezo kupitia kupewa uongozi kwenye kaya waliyoikana miaka mingi iliyopita?
Kwanini hawalalamikii mahanjumati na ofa za kuja bara kuzaliana ilhali wabara wakienda kule wanaambiwa wanapeleka mila chafu kama vile wizi, umalaya, bwibwi na upuuzi mwingine wakati si kweli? Mie naona hakuna muarobaini mwingine wa kukata hizi ngebe na mahusiano ya kugeuzana punda kama kuwa na serikali moja na nchi moja.
Nilishangaa kutoona wala kusikia mawazo yangu pale nilipodai kuwa kama watapendekeza serikali mbili au tatu, basi ni bora wavunje huo muungano ambao siku zote umegeuka mgongano na mnyonyano. Kwanini kipande cha ardhi kisicholingana na hata mkoa mdogo kuliko wote kitutie presha? Si tuwaache waende kivyao waone kama ni busara kuliko kuwang’ang’ania huku tukiwapa kila kitu wasiridhike bali kutaka zaidi?
Ukisema kiumane kila mtu kivyake watu wanaanza kusitasita kwa kujua kuwa wana ulaji toka upande mmoja kwenda upande mwingine. Tuamue tugawane mbao.
Hakuna haja kuendelea kupoteza muda na njuluku kugombea vyeo vya kisiasa wakati uchumi wetu unawekwa kimada na wachukuaji wanaoitwa wawekezaji.
Badala ya kujadili utitiri wa serikali tujadili jinsi ya kumkomboa mlevi lau anywe, kula na kufurahi badala ya kuliwa na utitiri wa marais.
Uliona wapi kaya moja ikawa na viranja watatu? Kama ni hivyo basi kila wilaya iwe na rais wake tuone kama kutakalika.
Inashangaza kusikia watu waliokuwa wakijigamba kuwa muungano wao ni mwanzo wa kuunganisha bara zima. Mtaliunganishaje mkiongeza utitiri wa vijikaya vya ulaji na uongo na ukweli?
Siko tayari kuitwa Mdanganyika. Kama nitakubali basi ni kwenye kaya huru badala ya haya mazingaombwe na uliwaji visivyo na tija kwangu kama mlevi.
Tukiunga na kuwa na siri kali moja, hakuna atakayemtukana mwenzake chogo au kumwita mbara kama ilivyo sasa.
Isitoshe hizi kaya angalau zina cha kuchangia kwenye muungano kuliko hivi vidoa vya ardhi vinavyoogopa kumezwa. Wao wakitumeza sawa. Sisi tukiwameza nongwa. Mambo gani haya ya kizamani?
Chanzo: Nipashe Jumamosi Jan., 25, 2014.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
4 comments:
Umesema kweli, sioni sababu ya kuwang'ang'ania hawa watu. Weka serikali moja tujue moja, au kila mtu aende kivyake. Lakini kama kawaida, hiyo ni too simple. Watu wanataka serikali tatu, mikoa na wilaya kede kede.
Nchi haiendelei kwa kuwa na serikali au mikoa lukuki. Chapati haiongeki kwa kuimega vipande vingi vidogo vidogo. Wacha waende tupumue.
Du! Jaribu umeniacha hoi kwa analogue yako ya chapati. Kweli, niruhusu ninukuu maneno yako kuwa chapati haiwezi kurudufika kwa kuikatakata vipande.
Umeielezea vizuri kuliko nilivyosema mwenyewe, hasa hapo nilipoandika haiongeki badala ya haiongozeki.
Wow! Shukrani hata hivyo nimekunukuu wewe. You still deserve your credit.
Post a Comment