Taarifa ambazo hazijakanushwa naibu
waziri wa Mawasiliano Sayansi na Teknolojia, January Yusuf Makamba anajipigia
debe kugombea urais haziwezi kupita bila kujdaliwa. Taarifa zilizokaririwa na
vyombo mbali mbali ni kwamba Makamba ana mpango wa kugombea urais kwenye
uchaguzi mkuu ujao wa 2015. Wengi wanajiuliza Makamba ana sifa gani zaidi ya
jina la baba yake ambalo nalo linahusishwa na ufisadi, kujuana, kurithishana
madaraka na propaganda tu? Kwa umri alionao na historia yake ya kuingia kwenye
siasa kupitia mgongo wa baba yake, sijui kama January ana jingine la mno. Je watanzania
wataendelea kubariki utawala wa kifamilia ambapo kila anayepata nafasi
serikalini uhakikisha anamrithisha mtoto wake au jamaa yake? Hii ni jinai hata
kama imezoeleka na kuanza kukubalika. Hii ni hujuma kwa watanzania wasio na
majina makubwa wala mjomba wa kuwabeba ili waingie katika ulaji wa kula kwa
mikono miwili tena bila kunawa wala kuona aibu. Ni aina mpya ya ufisadi wa
kimfumo inayolenga kuiteka nchi na kuigeuza shamba la bibi la baadhi ya koo
zenye majina makubwa.
Hii si mara ya kwanza wala ya mwisho
kuongelea suala hili. Leo utasikia akitajwa Makamba. Kesho utasikia Nchimbi. Kesho
kutwa utasikia akitajwa Mwinyi na kadhalika. Namna hii nchi haiwezi kuendelea
kwa vile wahusika wanajuana na kulindana ukiachia mbali kulipana fadhila. Tusiruhusu
Tanzania kufikia kuwa nchi ya hovyo kama zile ambapo rais anamteua mkewe kuwa
waziri huku akimuandaa mwanae kumrithi. Tuondokane
na taifa ambalo kila aliye karibu na mkubwa naye ni mkubwa.
Je watanzania wataingia mkenge kama Kenya
ambao walichagua jina la mwanzilishi wa taifa hilo kwa sababu ya kikabila? Je Makamba
anataka kuingia kwenye orodha ya watoto wa vigogo waliopata madaraka simply
because baba zao walikuwa wazito kama vile Aman Abeid Karume, Ian Khama, Faure
Gnassingbe Eyadema (Togo), Joseph Laurent Kabila (DRC) na Ali Omar Bongo (Gabon).
Je Makamba hajaridhika na ulaji kwenye
kundi lake la wateule watoto wa vigogo la akina Emanuel John Nchimbi, Dk.
Husein Ali Hassan Mwinyi, Adam Malima, Mbaraka Abudulwakil, Vita
Kawawa, na Zainab Kawawa ukiachia wale waliotamalaki kwenye balozi zetu huko
nje?
Hapa hujawataja wakuu au waliowahi
kuwa wakuu wa wilaya watokanao na koo za vigogo kama vile Gerald J.
Guninita,Paul Mzindakaya,Festo Kiswaga, Khanifa M. Karamagi, Husna Mwilima, John
V. K. Mongella, John B. Henjewele, na Agnes Hokororo.
Hata ukienda kwenye ofisi nyingine za
ulaji wapo kama vile Dk. Hawa Rashidi Kawawa (Mganga Mkuu Msaidizi wa Jiji la
Dar es Salaam), Dk. Guni Kate Kamba (Mganga Mkuu wa Manispaa ya Kinondoni), Dk.
Asha Omar Mahita – (Mganga Mkuu wa Manispaa ya Ilala) na Dk. Amani Kighoma
Malima (Mganga Mfadhiwi wa Hospitali ya Temeke).
Ndani
ya CCM wapo Ridhiwan Kikwete, Dickson Membe, Freddy Lowassa, Ashura Hussein
Mwinyi, Ben Samuel Sitta, Deborah Mwandosya, Irene Pinda, Felister Ndugai,
Christopher Ndejembi, Sharifa Bilal, Hawa Kigoda, Judith Mukama, Jerome Msekwa,
Mboni Mhita na wengine wengi.
Benki
kuu nako hawakosi. Wapo wakihomola na kulinda maslahi fichi ya baba zao. Wapo Salama
Ali Hassan Mwinyi, Filbert Tluway Sumaye, Zaria Rashid Kawawa, Blasia William
Mkapa, Jerriet Marten Lumbanga, Pamela Edward Lowassa, Rachel Muganda mtoto wa
mke wa Daudi Balali aliyeliingiza taifa hasara ya mabilioni ya EPA na aliyekuwa
gavana wa Benki Kuu,Salma Omary Mahita,Justine Mungai,Kenneth Nchimbi,Violet
Philemon Luhanjo,Liku Kate Kamba,Thomas Mongela na Jabir Abdallah Kigoda. Ni uroho
na roho mbaya kiasi gani? Hapa hatujataja walioko kwenye taasisi nyeti kama
vile TRA, Ubalozini, Mambo ya Nchi za Nje, Viwanda, Hazina, Uhamiaji, Mizani,
na kwingineko kwenhye maslahi manono. Kimsingi, kinachofanyika, ni kwa watawala
wa sasa na waliopita kuwaandalia watoto wao na jamaa zao kuendelea kutawala
hata baada ya wao kuondoka. Hapa ndipo utawala wa kifalme usio rasmi na
kuwalindana unapotengenezwa mchana kweupe huku watanzania wakiendelea kuwaamini
kuwa wapo kuwakomboa wasijue wapo kuwakomoa na kujikomboa wao binafsi na koo
zao. Huwezi kuwa na kujuana kwa namna hii ukashindwa kuwa nchi ya kifisadi nay
a kiukoo (nepotic and clannish country). Huwezi kuliepuka hili hata kidogo.
Nadhani watanzania wamechoka na utawala wa
kurithishana iwe ni serikalini au chamanni. Je hawa watoto wasio na majina
mazito watatawala lini nao? Je Tanzania ni nchi ya kifalme chini ya ufalme wa
vigogo wa Chama Cha Mapinduzi na serikali yake? Tufikie mahali tuambiane ukweli
kuwa kuna haja ya kuwakataa watoto wa vigogo ambao kimsingi wanataka kuendeleza
utawala wa familia na mawazo mgando yale yale na sera za kujuana na kulipana
fadhila.
Japo Makamba kama mtanzania yeyote
anayo haki ya kugombea uongozi ngazi yoyote, ukiangalia historia na uzoefu
wake, unashangaa sifa atazipata wapi zaidi ya jina la baba yake. Ukiangalia hata jinsi alivyopata elimu yake
ya sekondari kuna mazabe. Ningependa kusikia siku moja akijitetea kuhusiana na
tuhuma kuwa alinunua jina la mchovu ili kuweza kusoma kidato cha tano na sita. Kama
ni kweli alifanya hivi, huyu anaweza kufaa kuwa rais? Akipata urais atawanunua
wangapi? Bahati mbaya watawala wetu wanapokabiliwa na kashfa na tuhuma kama
hizi huwa wanakaa kimya ili zijifie wasijue kuna watu wasiosahau.
Tuhitimishe kwa kuwashauri watanzania
kuwa macho na watu wanaotumia majina ya baba au mama zao kuusaka uongozi. Tuwafichue,
kuwazodoa na kuwaambia fika kuwa hawatufai. Kama wanafaa basi wanafaa
kuondolewa kwenye nyadhifa walizozipata kutokana na ukubwa wa majina ya wazazi
wao au mitandao ya kujuana ya kiulaji iliyotamalaki nchini. Inatosha basi
kumwambia mtu kama Makamba kuwa hana sifa za kuweza kugombea achia mbali kuwa
rais wa Tanzania. Walichokula kinatosha. Tuwaachie wengine wenye uchungu na
uwezo wasimame lakini si wachovu wanaojificha nyuma ya umaarufu na mitandao ya
wazazi wao.
2 comments:
Monarchy State!!!?
Nicely put Anon. Bravo.
Post a Comment