Naona yule anaanza kuguna na kutolea picha yangu mimacho utafikiri nimemgusa yeye. Najua tatizo hapo si picha yangu bali kichwa cha habari yenyewe.
Basi soma habari hata kabla ya kuanza kuniporomoshea mitusi hata
kama sitaisikia wala kuguswa nayo. Hujui mie ni mlevi asiyejali kitu
bali haki na kanywaji?
Kwa vile nami ni raia wa kaya hii, basi lazima nitoe mawazo na maoni yangu ili nisikike na kutendewa haki sawa na wengine.
Pamoja na kupinga kuwepo kwa utitiri wa serikali ambazo bila shaka
zitakuwa na marahisi na makando kando yao, hakuna kinachoniumiza kichwa
kama kuona tunakuwa na marais watatu.
Marais watatu? Marais watatu wanaokula, kuvaa, kutanua hata
kuzurura bure siyo? Hapa bado hujagusia ma-first ladies watatu,
vitegemezi vyao, wapambe, mashoga na washirika wao! Du! Tumegeuka kaya
ya kuhomolana hivi! Kwa utajiri upi kama si ulimbukeni, ufisi,
ulimpyoto na kujilisha pepo?
Namna hii uhuru wetu uliokwishageuka udhuru utapona kweli? Najua
sirikali hizi zitategemea pesa ya wafwadhili ambao nao pia watataka
malipo. Kuna uhuru hapa au udhuru?
Najisikia kutapika ninapokumbuka nilivyoapa kuulinda muunganiko
ambao sikujua kuwa “wajanja” watausambaratisha. Haiwezekani tuwe na
sirikali tatu na tuendelee kujidanganya na kuidanganya dunia kuwa tuna
muunganiko. Huu si muunganiko bali mgongano.
Hebu tuwe wa kweli kidogo. Hivi kuna muungano wa utatu wa kweli
zaidi ya ule wa kwenye riwaya wa baba mwana na roho mtaka… stop!? Kama
huu tunaambiwa ni wa ki-Mungu, je huu utatu tunaoletewa ni wa kinini?
Nasikia wapo wanaosema eti utapunguza gharama za utawala. Ya kweli
hayo ndugu zanguni? Laiti wangeniambia kuwa wanafuta utitiri wa wilaya
na mikoa ndipo ningewaelewa.
Kesho tutaambiwa kuwepo na sirikali za majimbo ambapo kila mkoa
utakuwa na rais wake na makandokando yake kama jamaa zetu wa Kenya
wanaogombea hata bendera.
Jamani tunakwenda wapi? Hayo tuyaache watayajibu wahusika kama wanayo majibu yanayoingia akilini na si sanaa kama kawa.
Siyo siri. Bi mkubwa wangu ananizidi ubavu nyumbani kwetu. She is
on top of me in many things. Kwa vile Bi mkubwa wangu ananizidi pawa
nyumbani nami nataka kugombea urahisi, lazima nitake katiba itamke wazi
kuwa haruhusiwi kuanzisha NGO ili nikiupata asinisumbue sumbue
kumuunganisha na wazito wenzangu kutengeza ngawira au vipi?
Bi mkubwa alivyo na tamaa ya ukuu na utajiri si atachuuza urahisi
wangu hata kabla sijamaliza kama siyo kunizulia kashfa kiasi cha
kuutishia? Nani anapenda mambo ya Anna Tamaa au Salima Shari Chinga?
Nani anataka mambo ya Kiwila coal mine au kugombea vyeo uchwara kwenye
chama? Pia sitapenda naye awe rahisi wa NGO yake kiasi cha kunidharau
au hata kutumia ulaji wangu kuusaka ulaji ambao unaweza kunitokea puani
nikimaliza urahisi.
Nitajuaje kuwa ataamua kunipiga talaka baada ya kuchuma halafu
aniache hoi wakati nitakuwa sina madaraka ya kuvutia vidosho wengine?
Pia naongopa nisipopata urahisi wakapata wengine kuona utitiri wa
NGO tatu mara Wanawake na Maulaji (WaMa). Mara Fursa Kubwa kwa Wake za
Wakubwa na madudu mengine (EOTF).
Mwe! Kaya yetu inaliwa mbele na nyuma! Kwa vile nina akili na nia,
nitahakikisha katiba hii haipiti na kama ikipita basi nitajinyotoa roho
ili kuepuka kuliwa kama hamnazo.
Hivi hawa wanaotuambia sirikali tatu wameishafikiri kuhusiana na
mashangingi, ikulu, ndege, walinzi, misururu na mambo mengine ambayo
marais wetu hupenda kiasi cha kuugua wasipoyapata? Nikipiga picha naona
hatari mbele ya safari. Hivi itakuwaje siku ambapo marais watatu na wake
zao watakuwa na misafara ya kwenda uwanja wa ndege au viwanja vya
Sabasaba? Si wachovu tutafia kwenye misururu ya magari jamani?
Hivi mnadhani kukaa masaa kwenye foleni kwenye joto la Bongo ili kuwapisha marais na walaji wao ni mchezo?
Wao wana viyoyozi kwenye mashangingi yao. Wanafunga barabara ili
wafike haraka wakati sisi tunafungiwa ili tusifike kana kwamba hatuna
mahitaji tena ya muhimu kuliko yao.
Tunalipa kodi kuanzia ya kanywaji hadi bangi wakati wao hawalipi
chochote zaidi ya kutumbua kodi zetu. Huu ni utu kweli? Huu ni uongozi
au uongo zii kama si unyonyaji uliohalalishwa?
Nadhani sasa najua sababu ya akina Ewassa na wezi wengine kuutaka urahisi ili wale na kunywa na kutanua kirahisi.
Ukiachia kutaka katiba ipige marufuku my first lady kuwa na NGO au
kampuni fichi ya ulaji, nitahakikisha inapiga marufuku vitegemezi
vyangu.
Siwezi kuhangaikia ukuu halafu vyenyewe vije kutanua utadhani
vimesota kama mimi? Kwanini niapishwe peke yangu na walaji wawe wengi?
I am not that corrupt. So too, I am not that stupid so to speak. I’m a smart guy but not a yo-yo or a yahoo.
Siko tayari kutumiwa na mtu hata awe mke au mwanangu ati. I am the
only guy in the hunk who’s nary partaken corruption of any sort.
Ndiyo maana mnaona ninavyoanikiza kuzuia ulaji wa rahisi nyuma ya
koti la urahisi wa wale wanaopaswa kuwa watu wangu. Mie ni kama Mchonga
bwana. Siandai kitegemezi ndugu wala mke wangu kuchukua madaraka yoyote
hata yawe ya ngazi ya wilaya.
Kwa vile hii katiba tunaambiwa ni ya walevi, basi nitapendekeza tuongeze idadi ya baa badala ya sirikali.
Nitashauri tupunguze bei ya kanywaji na kuhalalisha bangi badala ya utititiri wa sirikali. Tumechoka na siri kali.
Tunataka siri kidogo na rahisi. Heri kuwa na walevi wengi kuliko
marahisi wengi. Maana marahisi wengi hupwakia ulaji wa rahisi rahisi
kiasi cha kufanya mateso kwa walevi wetu yaongezeke kirahisi rahisi huku
walaji wakiongezeka na kutanua kirahisi rahisi. Hii si kaya ya rahisi
wala ulaji rahisi kama ilivyo.
Chanzo: Nipashe Jumamosi 18, 2014.
2 comments:
Yupo sahihi Mlevi katika ushauri wake...Hivi Michelle Obama anamiliki N.G.O naye pia!?
Bwana NN Mhango, Najua awali umekataa kuitwa Dr kwa sababu bado kuhitimu sasa. Isipokuwa vyuo vyetu hapa kwetu kwa sisi wa hapa Bongo tunatoa hizo Digrii za udhamivu kama karanga vile hivyo acha shaka kuhusu hili
Michelle anaogopa hiyo NGO au Ni Genge Ogopa kama ukoma.
PhD ya kwenu naiobopa sana. Sina haraka nayo kwani niombacho ni uhai na kuweka sawa maandiko yangu tu. Shukrani. Hizo zitolewazo kama karanga wape akina Jakaya Kikwete, Makongoro Mahanga, Emanuel Nchimbi, Mary Nagu, Didace Massaburi, Matayo Matayo, Victor Mwambalasa,William Lukuvi na wavivu wengine.
Post a Comment