Pamoja na kuupiga mma kiasi cha kujisahau, sijasahau kaya yangu. Nafahamu sana tu. Nakumbuka sana tena kwa moyo wote na akili zangu zote na kwa uwezo wangu wote. Kaya yangu ni maskini wa kutupwa ambapo mzito wetu aka rahisi aka prezo aka mnene aka baba Riz anasifika kwa kuizunguka dunia akibomu ili angalau wabongo waende wee koma! Nikikumbuka alivyokuja na sera na kauli yake mbinu ya ANGUKA ambayo walevi hawakuipata, natamani kujinyotoa roho ili nisiendelee kushuhudia haya makufuru na mazabezabe ninayoshuhudia.
Najua viherehere wa bwana mkubwa wanasema, “Sasa tumempata huyu chizi mlevi kwa kusema eti sera ya muungu wetu ni ANGUKA.” Wala msijisumbue. Maana ya ANGUKA ni simpo. Ari mpya, Nguvu Mpya na Kasi mpya katika lolote unalofanya. Ukitumia sayansi hii ya ANGUKA lazima uangushe wale uliowaahidi hayo maanguko hapo juu. Hayo tuyaache. Humu si mwake leo. Na kama si kuheshimu sheria na huruma yangu, huenda ningetoka hapa na kwenda kula nyama ya mshenzi huyu anayeibia kaya yangu halafu na kuanza mashauzi ya kipuuzi. Shame on you! Don’t you know that we know you are but a con man? We know everything. If you go on vomiting like that we’re going to teach you a lesson.
Wahenga walisema. Ukishangaa ya mlevi utaona ya mgema. Si nikiwa ndiyo nimerejea kutoka kupata kanywaji si nilikutana kuku wawili wakigombana tena kwa sauti za juu. You know what. Baada ya kukaa na kuwasikiliza kwa muda niligundua kuwa kumbe wale kuku walikuwa mke na mme wakigombea mambo ya unyumba na tabia ya jogoo kuwa na nyumba ndogo kibao. Baada ya kuupata ukweli sikuona haja hata ya kuwasuluhisha. Niliachana nao nikijisemea moyoni, “Mkikutana na wezi wa kuku huenda mtatia akilini.”
Baada ya kushangaa ugomvi wa kuku si nilipata baba lao. Baada ya kutia timu home si mama Domo Kubwa akanipa stori iliyofanya hata ugomvi wetu niliokuwa nimeukimbia asubuhi wa kumwibia njuluku utoweke. Alinipa kisa cha nshomile mmoja aitwaye Jemus Rugemaaalira aliyesema eti madafu bilioni 120 ni vijisenti vya ugoro.
Alisema, “Mume wangu nilikuwa najua wewe ndiwe kibaka wa mibaka kayani mwetu kumbe uongo.”
Kabla ya kuendelea nilimuingilia nikisema, “Mama Domo chunga mdomo wako tusitoane ngeu bure. Wewe ni kuniita mimi mumeo kibaka wa mibaka wakati mibaka yenyewe unaiona ikiwa kwenye ulaji?” Hebu niombe msamaha kabla sijajinyotoa roho ukaishia kuwa mjane usawa huu ambapo unanihitaji kwa mengi.”
Kasheshe na mshikemshike wa kimbembe viliishaje? Si kazi yako kujua. Maana utapata umbea wa kuwapa washirika na washikaji zako bure.
Kwanza, sikumuani bi mkubwa kwa vile tulivyopigika kusikia ngurumbili akisema eti mabilioni ni vijisenti vya ugoro bila shaka mdudu mtu huyu atajhitaji kuchunguzwa bichwa lake. Hawezi kuwa mzima huyu. Kama ni mzima basi kichaa chake bado kichanga. Unashangaa huyu anayesema eti bilioni 120 ni vijisenti vya ugoro kwanza ana uchache kiasi gani? Je ameupataje? Je analipa kodi ya biashara zake uchwara za kutapeli hapa na kule?
Leo nina maya na mpuuzi mmoja aliyelewa fweza za wizi hadi akakufuru tena mchana kweupe. Hivi kama si kufuru ni nini kuita madafu bilioni 120 au dolari za KiObama 75,000,000 vijisenti tena vya ugoro? Huo ugoro ni aghari kiasi gani hadi kugharimu njuluku nyingi ambazo hata rais wako hawezi kupewa kwa mkupuo mmoja anapokwenda ughaibuni mara kwa mara kubomu? Nashauri huyu mjivuni nshomile awekwe ndani mara moja kabla sijajifunza ugaidi nikafa na mtu mie.
Baada ya bi mkubwa kunipa full story ya nshomile mjivuni niliingia porini kusaka habari zake ili lau nimjue na kama ikibidi kumchukulia hatua niwe namjua fika. Kwa vile mimi ni prof wa utafiti, haikuwa kazi ngumu kumfukua na kumpata mtu mwenyewe ambaye kumbe anatia shaka kulhali. Kwanza, niligundua kuwa huyu nshomile anayeita mabilioni vijisenti vya ugoro ni mtoto wa kapuku huko kwao. Nasikia baba yake alimsomesha kwa kulima vibarua kwa majirani zake na alikuwa akilalia ngozi ya mbuzi maisha yake yote hadi siku alipoanza kidato cha kwanza kwenye shule moja mkoani kwake ambayo nitaitaja baadaye.
Pia niligundua kuwa huyu jamaa alizaliwa akiwa tapeli. Alianza kutapeli vifaranga na vitu vingine vidogo vidogo kabla ya kupata elimu na kuitumia kuwaibia walevi.
Nilipokutana na walevi kujadili jambazi huyu anayejulikana kwa kuiingiza kaya kwenye migao na ulanguzi wa umeme kutokana na kampuni la kitapeli la IptL alilo nalo ubia chini ya mkampuni wake wa Vip Engmoneying vikiikamua kaya kwa kutofanya lolote. Jamaa huyu anafahamika alivyoshirikiana na matapeli wa kimalaysia kuiibia kaya. Mlevi mmoja alituacha hoi aliposema kuwa vyombo vya habari viliripoti kuwa huyu jamaa na majambazi wenzake walianzisha utapeli wao kwa jumla ya dola 50 lakini wakawa wanalipwa dola 100,000 kwa siku simply for doing nothing. Mlevi alituacha hoi aliposema kuwa hii kampuni ya Vip Engmoneying ni mali ya vigogo na huyu nshomile anatumiwa tu na wenyewe wenye mali ambao ni wazito kayani. Ndiyo maana huu utapeli wake akauita Vip Engmoneying. Huyu hana tofauti na akina Kagodamn walioiba pesa za EPA. Hawa kitaalamu tunawaita vyangudoa wa kiuchumi wanaoweza kutumiwa na fisadi yeyote mwenye madaraka. Wako tayari kujiuza kwa yoyote anayetaka kuwatumia atakavyo ilmradi mkono uende kinywani.
Katika research yangu niligundua kuwa huyu mjivuni nshomile na tapeli analindwa na dingi ambaye wakati mkenge na ujambazi huu ukisainiwa alikuwa waziri mkubwa wa wizara husika.
Baada ya walevi kudurusu historia ya nshomile huyu, wametoa mapendekezo kwa wachovu kuchagua wapingaji kwenye uchaguzi ujao ili hawa mafisi na mafisadi wakamatwe na kunyongwa kwa kupigwa mipini kama mbwa aliyeiba mafuta ili kutoa somo kwa wengine.
Chanzo: Nipashe Machi 15, 2014.
8 comments:
Je huyo dingi anayemlinda huyu Wasibota Sasquatch ni yule dakta uchwara mwenye homa ya kuzurura?
Jaribu unauliza jibu? Hujui kuwa huu wizi uitwao IPTL ulianza jamaa akiwa waziri wa nishati? Kimsingi, wawili hwa ni kama nyani na ngedere na pori ni lile lile sema nyakati ndizo tofauti. Huoni jamaa ameuza hisa zake baada ya kugundua kuwa mwenzake anaachia ngazi karibuni?
Pesa ya ugoro!!!!!, nafikiri hii ndiyo kauli mbaya na dhihaka kwa wapiga kura(kuliko hata sababu za kuomba kufungiwa kwa blogu moja huko za nyuma kwa kuonekena kwamba inachangnia kukiuka maadili) wao wasioukuwa na unafahamau tosha juu ya thamani ya kura zao kuchagua viongozi kupitia C,C,M...Ushaidi wa huo umbuumbu ni uchaguzi wa Kalenga hivi karibuni na ufuatao hivi punde wa Mbunge Ridhiwani
Anon usemayo ni kweli ila watanzania wengi hawaelewi. Ukitaka kujua kuwa tumeshikwa na kushikika, kumatwa na kukamatika angalia baadhi ya ndugu zetu wanavyotoa povu kukataa usiwepo uraia wa nchi mbili wakati magabacholi na mafisadi na vitegemezi vyao wanao. Acha waliwe ipo siku watastuka au wawe kama wakenya ambao ukabila kwao ni dini na uhai wa taifa sawa na ulimpyoto kwa watu wetu.
Shida ni kwamba Waafrika siyo ni kwamba hatuna akili kama watu wengine, ni kwamba utamaduni wetu unatudumaza. Siyo watu wa kufikiri kuwa kuna njia bora nyingine, au utawala bora mwingine. Sisi kuchangamka na kufikiri utawala mbadala ni shida sana, na hatuna udadisi. Msishangae kuona CCM bado inafaulu kuwarubuni mamilioni ya watu wenye akili zao timatu. Mmarekani mzungu asiye na elimu nyingi aliwahi kuniuliza, "Inakuwa nyie Waafrika mlikuja kushindwa na wazungu wachache, mara nyingi si zaidi ya hamsini wanateka nchi nzima?" Jibu lilikuwa gumu, lakini linaweza kutoa mwanga kwa swala la wezi wa CCM kufaulu kuwaibia na kuwadanganya Watanzania miaka nenda miaka rudi.
Jaribu umeuliza swali ambalo mara nyingi limenifanya nionekane kama mwenye kulaumu tu wazazi wetu. Kwa ufupi ni kwamba waafrika tuna tatizo ya kupenda kusifiwa hata kwenye upuuzi. Ndiyo maana unaona dini za kimapokeo zimeleta uhasama kiasi cha watu kuchinjana tena wakiwa ndugu moja wakifia ahadi za kipumbavu. Nadhani unaona kinachoendelea CAR kwa sasa ambapo wakristo weusi wanauana na waislamu wenzao weusi. Tuna tatizo la kutojiamini. Ndiyo maana ilikuwa rahisi kwa mzungu kuja kutwambia kuwa mila zetu ni za kishenzi au mwarabu kutwambia kuwa ndugu wa muislamu ni muislamu na si yule anayezaliwa naye. Ndiyo maana Afrika imejaa mahekalu wa miungu ng'ombe na moto wa kihindi wakati waswahili wenzetu walioko kwenye visiwa vya Anjuman wakitumiwa na magabacholi hawa hawa kama wanyama wa kuonyeshea watalii. Niliwahi kuandika issue hii ya waswahili wenzetu kuendelea kuishi kwenye ujima na ubaguzi bara hindi wala haikupata wala wasomaji achia mbali wachangiaji. Hii inaweza kukuonyesha uhovyo wetu. Angalia hata kwenye suala la uraia pacha ndugu zetu wanavyotoa povu kutukatalia wakati wakijua magabacholi na majambazi wanaowatawala na kuwadhalilisha kila siku wanao urais wa nchi zaidi ya tatu.
Aisee ile mimi niliiona lakini nikapigwa butwaa nikawa sijui niseme nini. Maana kila unapoangalia unakuta watu weusi wanapelekeshwa. Haya sasa India, Sudan huko walikuwa wanauzwa utumwani, (kulikuwa na mchezaji vikapu mmoja Manute Bol alifilisika kwa kuwanunua ndugu zake wa Sudan Kusini kutoka utumwani). Ukija kwenye nchi zetu "huru", huku unawakuta Waswahili wenzio wanakunyanyasa kuliko hata makaburu. Kwa hiyo ile ya Wahindi niliipata, ila wakati inauma sana mtu inabidi unyamaze.
Ndio maana mimi naona sisi Waswahili wenyewe kwanza tujisafishe. Hatuwezi kuwalaumu watu wengine sana wakati wenyewe tunafanyiana ujinga huu. Kikulacho ki nguoni mwako.
Kwa mfano nikikumbuka wale mabaniani wa RITES waliokuja na porojo tu halafu wakalipwa mamilioni ya fedha. Ukweli ni kwamba hao wasingeweza kuja kuiba Tanzania kama wasingealikwa na Kikwete na wezi wenzie. Huko Mara polisi wanaua watu kwa sababu ya migodi ambayo inawanufaisha wezi wa nje na wenzao wa ndani.
Na leo sitaki hata kuzigusa hizo dini za Mashariki ya Kati. Na ukisha jua sayansi kidogo, unaelewa kuwa zote hizo ni simulizi, nyingine za kusisimua lakini bado simulizi. Kumuua mtu mweusi mwenzio kwa sababu anaamini "spiel" tofauti na yako, kwa mimi ni ujuha wa hali ya juu.
Jaribu hao ndiyo ndugu zetu. Kuna kipindi napanga kuandika kitabu ambacho ima kitawafumbua macho au watanichukia. Ni bahati mbaya nilianza kukiandika miaka ya 90 lakini nikapoteza mswada kiasi cha kuupa ubongo miaka ya kupoa na kuona kama naweza kuwasha jet tena na kuandika mambo makubwa.
Post a Comment