The Chant of Savant

Tuesday 25 March 2014

Vunjeni Bunge la Katiba, okoeni fedha zetu

KWA waliofutatilia na kusikiliza hotuba ya Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete, ya zaidi ya saa mbili  kwa Bunge la Katiba (CA) kule Dodoma watakubaliana nasi kuwa alikwenda kule kuvuruga mambo na kujivua nguo hasa alipopoteza fursa ya kujijengea heshima akajipinda kupingana na tume aliyoiteua mwenyewe.
Alipoteza fursa na muda kwenye kuizodoa na kulumbana na tume aliyoiunda mwenye, jambo ambalo kwa mkuu wa nchi linamuonyesha mtu mbabaishaji na anayefanya mambo bila kujua anachofanya.
Wapo wanaona kama Rais Kikwete, hakukosea hata kidogo hasa ikizingatiwa kuwa hakwenda kule kama rais japo alilipwa na kutumia ndege ya rais.  Wanasema kuwa alikwenda kule kama kada na mwenyekiti wa chama aliyekwenda kufanya kazi moja— kutetea sera ya chama chake ya serikali mbili.
Kweli, hakuna cha maana kitaifa alichofanya Rais Kikwete, wala kutamka kwenye hotuba yake ambayo wengi wameiita maelekezo ya semina zaidi ya kuonyesha unazi na ushabiki wa hoja za chama chake.
Kwa kumbukumbu ni kwamba Rais Kikwete, alikaririwa akiwalaumu Watanzania kwa kujikita kwenye hoja moja ya serikali tatu au mbili badala ya hoja nyingine muhimu kwenye rasimu.
Ajabu, baada ya Rais Kikwete kutoa lawama hizo, naye aliingia mkumbo huo huo wa kutumia muda mwingi kwenye maelekezo, vitisho, kujibu mapigo, mipasho na madude mengine kujadili muungano huo huo akitetea serikali mbili wazi wazi.
Kwa waliozingatia aliyosema Rais Kikwete, alichotoa si hotuba bali alipiga kampeni.  Hivyo, hotuba yake si ya kupingwa tu bali hata kulaaniwa kwani ameonyesha ‘double standard’ ya kuhadaa Watanzania kuwa anataka wawe na katiba yao kumbe ni katiba yao CCM na si Watanzania wote.
Wengi wanaona hakuna hata mantiki ya kuendelea na Bunge la Katiba kwa vile Rais Kikwete ameishamaliza kazi. Hivyo, kinachoendelea licha ya kufuja pesa ya umma ni kutaka kuwatumia kama mihuri ya kubariki Katiba ya CCM.
Tunajua wabunge na wapenzi wa CCM hawatakubaliana na ushauri wa kuvunja Bunge la Katiba. Pia wachumia tumbo wanaofuata malipo hawatakubali kuachia ulaji wa dezo, wanaoweza kufanya kinatochatakiwa si wengine bali wapinzani.
Wapinzani susieni hii ‘shoptalk and sideshows’ zinazoendelea Dodoma. Badala yake unganeni na kufanya nchi isitawalike ili sauti ya umma na utashi wao viheshimiwe. Msipofanya hivyo mtaendelea kuchezewe na kuhujumiwa tu.
Rais Kikwete amethibitisha asivyo na dhamira safi kwa taifa wala asivyoheshimu mawazo kinzani tena yatokanayo na umma. Ametumia hoja ya nguvu na ujanja ujanja badala ya nguvu ya hoja.
Ametumia mtindo wa kuvizia kufanikisha anachotaka.  Kama alivyokiri, rasimu imeandikwa kiweledi na haina cha kuingiza binafsi bali mawazo ya umma. Sasa kosa la tume liko wapi?
Rais Kikwete, amekosa busara hata katika kupinga serikali tatu. Ametumia mtindo wa kuvizia na kutegemea kuvunjwa kwa kanuni ili aondoke na ‘credit’ hata asipostahili. Kisheria, hotuba ya Kikwete ilipaswa kupingwa.
Inashangaza kuona wale waliomzuia Mwenyekiti wa Tume iliyoandaa Rasimu ya Katiba Mpya Jaji Joseph Warioba, hawakuliona hili. Je, hawakuliona au walitumiwa tu kuwezesha uhuni na uvunjaji wa kanuni uliofanywa na mtu anayejiita mtu wa viwango? Viwango kama ni hivi hakuna katiba bali kitabu cha kubariki ubazazi wa CCM.
Akiongelea muungano akitetea serikali mbili alisema: “Tunaweza kupoteza kitu tulichokijenga kwa gharama kubwa kwa nusu karne iliyopita. Tanzania inaweza kuwa nchi iliyojaa migogoro na matatizo mengi ambayo hatunayo.”
Kuna sehemu Rais Kikwete alifikia hata mahali kufanya uhaini alipotoa kitisho cha mapinduzi kana kwamba ameishayaandaa.
Si kazi ya Rais Kikwete, kufundishia faida au hasara za muungano. Ni mara ngapi watu wanashuhudia majengo tena marefu ya zamani yakibomolewa na kujengwa majengo mapya ya kisasa? Hivyo, gharama si hoja sana hasa ikizingatiwa kuwa demokrasia na haki ni gharama siku zote.
Rais Kikwete, alitumia muda mwingi kuidhalilisha, kuijibu na kuisingizia tume. Mfano, alikaririwa akisema: “Akitokea kiongozi ye yote wa nchi washirika akatunisha misuli dhidi ya Rais wa Muungano au kupinga maamuzi ya Serikali au chombo cha Muungano, Rais na serikali yake watakuwa hawana lo lote la kufanya.
Kwa kweli uhai wa Muungano katika muundo wa Serikali tatu ni wa mashaka makubwa.”
Mwenyekiti Mao wa Uchina alikuwa na msemo maarufu kuwa kama hujafanya utafiti huna haki ya kuhoji. Ni bahati mbaya Rais Kikwete hajatwambia amefanyia utafiti wapi zaidi ya kuja na hadithi ya Comoro ambayo haifanani kabisa na hali yetu Tanzania.
Kwa vile Kikwete hakuja na utafiti wowote wa kisayansi, alichofanya ni kuwadanganya wananchi badala ya kuwaaminisha kuwa kinachoendelea kinalenga kuwaletea katiba wanayotaka na si hii ya kupachikiwa na kina Kikwete na CCM ili waendelee kutawala kijanja kijanja.
Kikwete aliendelea kudanganya kwa makusudi. Aliongeza kusema: “Na pili, ni kuibuka kwa hisia za utaifa (nationalistic sentiments) wa zamani kwa nchi washirika.”
Aliita hali hii kama ya hatari wakati akifahamu fika kuwa katika Muungano wa serikali mbili Wazanzibari siku zote wameendelea na utaifa wao na haikuwa hatari.
Je, inakuwa hatari Watanganyika wanapoonyesha hisia za utaifa? Kikwete hapa anamaanisha nini zaidi ya kuchanganya mambo kwa kuyapa tafsiri potofu na ya kupotosha? Kuwa na hisia za utaifa ndiyo uzalendo wenyewe na kutokuwa nazo ndiyo usaliti wenyewe.
Ngoja nitoe mfano mmoja wa hapa Canada ambapo wananchi wake wana sifa moja nayo ni kusema: ‘But we are Canadians’. Yaani kumbuka sisi ni Wacanada kuonyesha maana ya utaifa wao.
Tumechukua sehemu kidogo ya hotuba iliyojaa uongo na vitisho ya Kikwete kutokana na kuwa makala moja haiwezi kuichambua kwa utuo. Kwa ufupi ni kwamba alichofanya Kikwete akishirikiana na kada mwenzake Samuel Sitta, kuvunja kanuni na kuamua kutoa semina elekezi kinaua maana yote ya kuwa na bunge la katiba.
Kuepuka kupoteza muda na fedha za Watanzania na kuwafanya kuwa mihuri ya kubariki uovu, Bunge la Katiba lingevunjwa tuendelee na Katiba ya sasa hadi atakapotokea rais mwenye uwezo na nia ya kuandika katiba mpya afanye hivyo badala ya huu usanii. Tunaomba kutoa hoja.
Chanzo: Tanzania Daima Machi 26, 2014.

2 comments:

Anonymous said...

Ubadhirifu wa fedha za umma unakuja kwa njia nyingi tofauti....kutengeneza kampuni fake kama Richmond, mikataba tatanishi IPTL, machimbo ya dhahabu, na mashimo yake ambayo hivi punde yatakuwa ndiyo yatakuwa makaburi yetu.

Hata hili zoezi linaitwa kwa ajili Katiba Mpya kimtazamo ni matumizi yasiyo sahihi ya fedha za Umma...Hivyo ni sahihi limalizike sasa na haraka. Angalau kuokoa hizi pesa za Karanga(Njugu)...Kama Bwana Rugemalira na $100,000 fedha za ugoro inayopatikana kwa siku kwa nchi ambayo wanannchi wake wanaishi chini Dola moja kwa siku...Haya matusi siwezi kusahau kamwe tusi lingine lilotukanwa huko nyuma na Chenge kwamba £500,000 ni vijisenti tena huyu ni kiongozi wa Umma anatutukana sisi...Ni Maumivu kweli moyoni.. Bwana NN Mhango

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Anon
Huyu Rugemalira ingekuwa amri yangu angeozea gerezani. Hata hivyo ana hofu gani wakati washirika wake wakubwa ndiyo wenye madaraka. Umetonesha moyo wangu ulipoandika kuwa mashimo yaliyotoa madini yetu yategeuka makaburi yetu. Hali ni mbaya tunapaswa kubadilika na kuwakabili hawa manyang'au na slave masters wanaoutuuza wazi wazi tena kwa bei ya pesa ya ugoro.