How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Wednesday, 5 March 2014

Mgimwa hauziki, Kalenga si wapumbavu

JAPO anafahamika kwa uhovyo wake, Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambaye pia ni Waziri Mdogo wa Fedha, Mwigulu Nchemba, ameonyesha ukweli wa uhovyo wake wakati akihutubia mkutano wa kampeni kule Nzihi jimboni Kalenga.
Akimnadi mgombea wa CCM, mtoto wa mbunge wa zamani aliyefariki dunia mwanzoni mwa mwaka huu, William Mgimwa, Godfrey Mgimwa, naibu katibu mkuu huyo, alikaririwa akisema, “Mtumeni kijana akashughulikie maji.  
“…mtumeni kijana akashughulikie umeme. Mtumeni kijana akashughulikie sehemu ambako watu bado wanapanda kwenye miti ili wawasiliane kwa simu.”
Mwigulu alibwabwaja mengi tu tena bila kufikiri kuwa alikuwa akijisuta yeye na CCM yake! Kumbe maendeleo anayojisifia kuletwa na CCM ni kiini macho!
Aliongeza, “Mtaji wa Wana CCM akiwamo Godfrey Mgimwa, mtaji wa mbunge wa CCM ni mafanikio ya wananchi…lakini mtaji wa wenzetu wale ni pale nyinyi mtakapokuwa na matatizo ili wailaumu serikali.” Mwigulu anaishi dunia ya gani?
Alisema eti wapinzani hawapendi maendeleo ya wananchi. Hii si kweli. Mbona watu wa Iringa Mjini wenye mbunge wa upinzani na hawalalamiki yeye kuwaletea matatizo zaidi ya kukwamishwa na CCM kama alivyokiri Mwigulu?
Aliendelea, “Hata katika akili ya kawaida, Rais anatokana na CCM, mwenyekiti, madiwani, wabunge, mawaziri…nyie leo mje mchague kadubwana kengine sijui kutoka wapi ndiyo kashughulikie maji kwa, mbunge, waziri wa CCM uliiona wapi?”  
Kwanza, hakuna mwananchi kadubwana. Haya ni matusi ya wazi kwa wananchi wote wasio vigogo.
Ni vizuri amesema hili kuwa kumbe CCM ndiyo kikwazo cha maendeleo kutokana na mawaziri wake kutoa huduma kwa kuangalia nani ni mwanacha au mbunge wa CCM au kwa kuangalia eneo husika kama limechagua mpinzani au Mwana CCM.
Namna hii huwezi kujitapa kuwa unaongoza nchi kwa misingi ya haki bila upendeleo kujuana na ubaguzi wa wazi wazi kama alivyokiri Mwigulu.
Maana yake ni kwamba usipochagua CCM lazima utakomolewa.
Inashangaza kusikia eti Mwigulu huyu ni msomi wa kiwango cha shahada ya pili tena ya mambo ya uchumi. Je, yawezekana akawa mingoni mwa tunaowajua kuwa waliotuhumiwa kughushi lakini Rais akawakingia kifua, mmojawapo akiwamo Mwana Iringa, William Lukuvi wa CCM?
Kuna haja ya kutaka Mwigulu achunguzwe akili zake.
Maana mambo aliyosema licha ya mengi kuwa ya uongo ni ya kujisuta yeye na chama chake bila kujua.
Anaposema wapinzani wanatamani Watanzania wakose maendeleo ili wailaumu serikali anamaanisha nini wakati CCM inayounda serikali iliwatapeli na kuwaahidi maisha bora yaliyoishia kuwa maisha balaa?
Je, Mwigulu anadhani Watanzania ni wajinga na majuha anaoweza kuwahadaa kila unapofika uchaguzi kama walivyozoea? Je, Mwigulu amesahau kuwa wananchi wa Tanzania wanajua uhovyo wa CCM na serikali yake ambazo ziko pale kunufaisha kikundi kidogo cha watu akiwamo yeye na huyo mgombea wake kwa kuendekeza utawala wa kifisadi na kujuana?
Wananchi wanajua kuwa CCM imekuwa ikiwarudisha nyuma kimaeneleo kwa kuruhusu makada wake waibe fedha na kuificha ughaibuni kama ilivyowahi kufichuliwa na mamlaka za Uingereza zilizowafichua makada wa CCM, Andrew Chenge na Idris Rashid.
Wananchi wanajua makada wa CCM walioiba pesa ya umma na kukingiwa kifua na Rais Kikwete kama kampuni ya Kagoda  ilichota pesa kwenye mfuko wa madeni ya nje EPA na wengine wengi lakini wakaambiwa wazirudishe wasamehewe.
Kuonyesha matatizo ya akili ya Mwigulu alisisitiza kuwa Wana Kalenga wapeleke kijana akatetee mambo ambayo yamesababishwa na CCM yenyewe hasa ukosefu wa maendeleo.
Haiingii akilini Mgimwa ambaye amesomea Ulaya wakati wenzake wakihenya hapa nchini atetee eti elimu wakati akijua kuwa elimu iko Ulaya na ndiyo inayowawezesha wao kuwatawala watoto wa maskini waliowatengeneza baba yake na CCM yake ili waendelee kurithishwa madaraka na kuwatawala hao hao.
Anasema kuwa wachague kijana wa CCM awaletee maendeleo, maji, mawasiliano, umeme na mambo mengine mengi.
Je, kati ya CCM na wapinzani nani kiongozi wa kuleta matatizo?  Ajabu wakati akisema hayo alisahau kuwa baba yake mgombea amekuwa mbunge na hakuweza kuleta vitu hivyo.
Rejea CCM kutuhumiwa kuiba pesa ya umma kuanzia ile ya EPA ya mwaka 2005, ambapo zaidi ya dola 115,000,000 ziliibwa kutoka Benki Kuu.
Rejea wizi wa hivi karibuni wa dola 300,000, 000 ulioripotiwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Fedha za Serikali uliofanyika hazina.
Je, hapa nani analeta maendeleo na matatizo ya wananchi? Je, huyu kijana ambaye baba yake alishindwa kuleta maendeleo tena akiwa waziri wa fedha atafua dafu?
Rejea maisha ya Watanzania kuzidi kuwa mabaya wakati rasilimali zao zikiwanufaisha wageni.
Nani amesahau utoroshaji wa wanyamapori hai kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) hapo Novemba 24, 2010)?
Nani amesahau jinsi Tanzania ilivyo kinara wa ujangili huku baadhi ya wabunge na vigogo wa CCM wakiwa watuhumiwa wakubwa?  Nani amesahau tuhuma dhidi ya bosi wake Mwigulu, Katibu Mkuu wa CCM Abdulrahaman Kinana ambaye kampuni yake ilituhumiwa kusafrisha nyara za umma lakini bado akateuliwa kuwa katibu mkuu?
Je, hapa CCM inakosa kujua na kushiriki ujangili ambao gazeti la Uingereza la Mail on Suday hivi karibuni lilisema ni sehemu ya kutunisha mtaji kwa ajili ya uchaguzi wa CCM?
Tumalizie kwa kumshauri Mwigulu kuwa aache matusi. Yake yakifichuliwa atazimia. Asiongopee wananchi kuwa CCM inawatakia maendeleo wakati ukweli ni kinyume.
Akubali kuwa mtoto wa kigogo mwenzake hauziki. Akubali kuwa Iringa si wageni wa mageuzi. Akubali kuwa watu wa Kalenga watafuata mfano wa wenzao wa Iringa Mjini waliomchagua  Peter Msigwa (CHADEMA) anayeonekana kuwa mwiba kwa CCM hasa mafisadi.
Chanzo: Tanzania Daima Machi 5, 2014.

No comments: