BAADA ya kuona watu wanataka kutoana roho kwa ajili ya vijiserikali vitatu mgosi Machungi amekuja na jibu. Pia ameona aje na muarobaini wa kuzuia kaya kuwa ya usultani au kifalme kama kijiwe kilivyopendekeza wiki iliyopita hasa ikizingatiwa kuwa wana kijiwe hawana damu ya kifalme.
Mgosi anasema amefanya hivyo ili kuokoa njuluku za umma zinazoliwa bila kufanya chochote. Pia alisema anataka kuepusha vifo vinavyoweza kutokana na kugombea mshiko pale mjengoni ambapo kila mtu anataka atoke akiwa bilionea kama si milionea.
Si Mgosi eti anataka kila mwenye kutaka kuanzisha serikali ruksa.
Bahati mbaya amesahau kuwa sera za ruksa ndizo zilizotufikisha hapa!
Baada ya Mgosi, kuona ulaji ulivyo mkubwa kwenye Katiba huko Dom kaona njuluku ipo ameamua kuja na namna ya kuidaka yaani kuanzisha serikali hadi chooni.
Aliingia kwa mkwara ‘God knows’. Maana tulipiga kahawa na kashata mpaka tukalewa na kuanza kuitukana. Nauli ya kwenda nyumbani kila mtu alipata.
Mgosi alikufuru pale alipotaka tuwachokoze ndata na kuwapiga halafu awalipe, ila tuliogopa kutoana ngeu na manundu tukaamua kumuachia balaa la utajiri wake wa muda.
Alisema, “Kwanini tisianzishe sera ya kila mtu kuwa na seekai yake?”
Mpemba anajibu: “Hii rahisi yakhe. Mie nenda kuwa rais Pemba wallahi.
Mipawa naye anakatua mic: “Lazima Mkoa wa Simiyu uwe chini yangu wagu wangu.”
Mijjinga naye hajivungi. Anakwanyua mic: “Natangaza kuanzia leo. Geita ni nchi yangu na mimi ndiye rais pekee. Watu kama Kanji na bi Sofi mkitaka kuja Geita lazima muwe na passport vinginevyo nawapiga PI. Pia wale wauza bwimbwi wakome. Wakija kule nanyonga badala ya kuwalea kama ilivyo kwenye kaya hii.”
Kijiwe hakina mbavu jinsi watu wanavyotambiana huku wakitangaza umilki wa mikoa utadhani kina Carl Peters na Mungo Park zama zile za utwahuti uliozaa ukoloni.
Kapende hataki aachwe kwenye mbio hizi za kutangaza urais. Anasema: “Lazima Lindi iwe chini yangu nione hawa wezi wa gesi watakula wapi kama si lupango chini ya serikali mpya ya ukombozi ya rais Mheshimiwa, mtukufu, Dokta, Profesa, Shehe, Alhaj, Maalim, mjua yote, kipenzi cha wote na chaguo la Mungu Kapende. Pia natangaza kuwa mafisi na mafisadi waliokwisha kukaa mkao wa kula gesi watauawa kwa kupigwa mawe.”
Kanji, kuona watu wanavyogawana kaya asijue yeye atakuwa mgeni wa nani anaingilia kati, “Jamani hapana vunja ungano. Sisi sote dugu moja. Kwanini kila mtu na koa yake? Iko taka mimi rudi Bombai jamani ife njaa?”
Mgosi anasema tena kwa nyodo: “Kia mtu ave na kwao ati. Kwani kuna ubaya gani kama Kanji utaudi kwenu Bombai? Utiache tupange maendeeo yetu Kanji.”
Kanji hakubaliani na mgosi. Anajibu: “Veve Chungi taka leta vita. Kama vatu yote nakaa kwao nani tafanya biashara dugu yangu?”
“Nshasema Tanga mai yangu. Kama unataka au hutaki si uende kwenye Bombai dugu yangu Kanji. Hiyo biashaa unayosema inasaidia nini kaya yetu zaidi ya kuhamisha mitaji kwenda Bombei na kwingineko?”
Baada ya Mzee Maneno kuichukua Pwani na Mzee Kidevu Mtwara, huku Msomi akipewa uwaziri mkuu wa Muungano, mzee mzima Mpayukaji napewe ukuu kaya hizi zote zilizotangaza ufalme wake lakini zikiwa chini yangu.
Hali hii kidogo inampa Kanji matumaini. Kwani chini ya muungano wa falme hizi mpya lazima kutakuwapo na mianya ya ufisadi ambao utawahitaji kina Kanji ili wanene wakiufanya wawe wa kuwafichia siri zao kama ilivyotokea kwa Chavda na gabacholi wa rada na mkangafu wa ndege wa mkuu.
Baada ya unyakuzi huu wa mikoa kikao kinakubaliana yafuatayo:
Mosi, wake zetu tatawapingia mikoa iliyobaki. Pili, nyumba ndogo na vitegemezi watasimamia wilaya zote katika nchi mpya.
Tatu, vyama vya siasa vyote vitafutwa. Kwanza, havina maana na vyanini wakati kila mtu ana serikali yake. Hapa hakuna chama twawala wala twaliwa bali serikali tu. Mbona mashule na vyuo wana serikali na hakuna noma?
Watu wanakula vitabu wengine wanakwenda kupiga uchangu na kupata shahada zao za nonihino na maisha yanakwenda. Bongo hii bwana. Unatumia ubongo hata kama kwa kutumia ule wa massaburi ubongo ni ubongo.
Kama alivyosema jamaa yangu Njaa Kaya kuwa raha ujipe mwenyewe. Nasi wana kijiwe tunataka kila mtu ajipe raha mwenyewe mkoani mwake na serikali yake.
Kama alivyosema Ben Makapu Tunituni kuwa mtaji wa maskini ni nguvu yake na mtaji wa wachovu ni kila mtu kuwa na serikali yake. Hii itaepusha ufisadi ambapo watu wanaiba njuluku za umma na kuficha Uswazi ya Uswizi.
Unakuwa na serikali yako unajilipa kodi mwenyewe. Hapa hata wale waheshimiwa walioishiwa hadi wanalipana posho za makalio tutawapiga marufuku maana wanakwenda kufanya mambo ya malavi davi who wants them na usawa huu wa miwaya wakiugua wamalize njuluku zetu kwenda India na Sauzi. Shame on you!
Pia Mgosi anapendekeza ndata wapigwe chini ili kila mwenye serikali yake akodishe kampuni za ulinzi ambazo hazitozi watu rushwa wala kuwatisha. Hapa ndipo Kanji anapenda kwa vile atawakusanya walevi wawili watatu na kufungua kampuni ya ulinzi halafu anakwenda serikalini kupewa tena ya ulinzi na siku zinakwenda au vipi?
Wale wazee wa mabao mtakula mafi yenu. Maana tutaleta kompyuta za kuongoza magari ambazo tunajua haziwezi kuomba rushwa. Hata waliozoea kushinda kwa kuchakachua mtakula mafi yenu.
Kwa vile kikao cha leo ni cha kusukuti jinsi ya kuukata, hakuna longo longo nyingi zaidi ya kusukuti na kusukuti.
Pia kijiwe kinapanga kuhakikisha zile njuluku zilizofichwa uswazi zinaletwa na kutumika kugharimia hizi serikali zetu tunazopanga kuunda ili kujikomboa kama wakubwa wanaojikomboa kwa kurithisha maulaji kwa vitegemezi vyao.
Kijiwe kikiwa ndiyo kinanoga si akapita mdada mmoja akiwa amevaa mlegezo kama wahuni wa kisasa. Acha tumzomee! Changu huyu nuksi! Si kikao kilivunjika kutokana na watu kwenda kuzomea na kutaka kumvua nguo changu ili atembee uchi kama anatangaza!
Chanzo: Tanzania Daima Machi 26, 2014.
No comments:
Post a Comment