BAADA ya kuona matokeo ya kura za wagombea ubunge katika majimbo ya Chalinze na Kalenga kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), nilijikuta nikimkumbuka hayati baba wa taifa, Mwalimu Julius Nyerere. Nilitamani angekuwapo akayashuhudia haya. Hata yeye alishajipumzikia ingawa hatutaacha kumtaja kila mara.
Baada ya kushuhudia watoto wa vigogo wakipitishwa na wachovu wa kawaida kuachwa ili wateule wajiunge na wazazi wao kwenye ulaji au kuwarithi wazazi wao nilijiuliza swali moja kuu.
Je, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere angekuwa kipofu na mroho hivi kuruhusu wanae watumie jina lake kujinufaisha kisiasa watu kama Ally Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete wangetia mguu ikulu?
Ukizingatia kuwa Mwalimu aliachia ngazi akiwa na watoto wakubwa kuweza kumrithi, bila shaka angekuwa hovyo hivi angewa- groom (kuwaandaa) ili wamrithi. Lakini hakufanya hivyo.
Kwake uongozi haikuwa nafasi ya kuiba na kuhomola bali kuukomboa umma badala ya kuunyonya na kuuzamisha kama ilivyo. Uongozi haikuwa fursa ya kujihudumia na kujitajirisha, kurithishana na kutumia ukubwa wa jina la ukoo bali kuutumikia umma.
Mwalimu Nyerere, aliamini kuwa ofisi ya umma ni dhamana ya kuutumikia umma na si kuutumia kama ilivyo.
Pamoja na tambo zake kuwa kilipigania na kuleta usawa, CCM kinaingia kwenye vitabu kama chama kinachohubiri maji na kunywa mvinyo.
Walianzia mbali sana. Ukitaka kujua huu ubaguzi na urithishanaji vyeo haukuanza jana, angalia majina kama Dk. Hussein Mwinyi, Emmanuel Nchimbi, Januari Makamba, Vita na Zainab Kawawa, Adam Malima na sasa Ridhiwan Kikwete na Godfrey Mgimwa.
Ni aibu na machukizo kushuhudia wanyonge wakizidi kuandaliwa viongozi watokanao na koo ili waendelee kuwatumia badala ya kuwatumikia.
Watawala wetu wasioona hatari ya kurithishana madaraka wanatuandalia viongozi watakaoendeleza pale walipoishia hata waliposhindwa kutuondoa kwenye adha zilizotulamisha kupigania uhuru.
Huu nao ni ufalme unaoingizwa kwa mlango wa nyuma. Je, Watanzania wataendelea kuubariki na kupigia mhuri ufalme huu wa kifisadi kwa kuupa kura ili ule au wataukataa na kuukatisha? Ni bahati mbaya sana.
Japo tunaweza hata kuzodolewa kuwa tuna wivu wa kike hata wavivu wa kufikiri kuushambulia mfumo huu hatari kwa taifa, tunahitaji kusimama na kuhakikisha tunajikomboa si kutoka kwa wakoloni weupe tu hata hawa weusi. Hata mkoloni mweupe, pamoja na ubaya wake, hakufikia kufuru hii.
Sikumbuki kusoma au kusikia kuwa Gavana Edward Twinning au Horace Byatt au Donald Cameroon kumrithisha mkewe au mwanawe madaraka katika serikali yake ya kikoloni. Huu ni ushahidi kuwa wakoloni weusi ni wabaya kuliko wale waliowaondoa.
Akili ya kawaida inakataa huu ulafi ambao matokeo yake yanaweza kuwa mabaya hasa baada ya kuigawa jamii yetu kwenye matabaka ya walio nacho, wenye damu ya kutawala, watawaliwa na vigogo.
Japo ni haki kwa kila Mtanzania kugombea nafasi yoyote, lazima hili lifanyike kwa kuepuka mgongano wa masilahi. Haiingii akilini eti chini ya dhana ya kila mtu kuwa na haki ya kugombea nafasi yoyote.
Kwa mfano, rais amteue mkewe kuwa makamu wa rais au waziri kama ilivyowahi kutokea nchi moja ya jirani ambapo ‘first lady’ ni waziri katika serikali ya mumewe. Huu ni ulafi hata utendwe na wenye na mamlaka.
Inashangaza kuona majimbo kama vile Arumeru Mashariki ambako mkakati mchafu wa kutaka mwana wa mbunge aliyefariki dunia alipitishwa kumrithi baba yake kana kwamba ile nafasi ni mali binafsi.
Ni bahati nzuri kuwa watu wa Arumeru walikataa aina hii ya ufisadi na ukoloni mpya. Haiwezekani wakubwa watupandikizie watoto wao kana kwamba hapakuwa na Watanzania wengine wenye nia na uwezo wa kuongoza.
Hapa tunaongelea ubunge. Ukienda kwenye sekta nyingine zenye maslahi manono kama vile kwenye balozi zetu nje, viwanja vya ndege, mipakani unapovushwa unga, Bandari, Mamlaka za mapato, Hazina, Benki kuu, Uhamiaji na kwingineko kwenye maslahi manono wamejazana watoto wa vigogo.
Mfano mdogo ni kashfa iliyoibuka miaka ya hivi karibuni ambapo iligundulika kuwa Benki Kuu (BoT) kumejaa watoto wa vigogo tena wengine wakiajiriwa kwa vyeti vya kughushi. Nina majina ya watoto wa vigogo walioko ughaibuni ambako si rahisi kwa Watanzania wa kawaida kutupia jicho.
Imefikia mahali hata mtu akifanya madudu badala ya kuwajibishwa anahamishwa au kupandishwa cheo. Nitatoa mifano ya watoto wawili wa vigogo ambao ni Hussein Mwinyi ambaye aliteuliwa waziri wa Ulinzi na kufanya madudu yaliyoshuhudia vifo vya watu wasio na hatia.
Ajabu waziri huyo hakuwajibishwa zaidi ya kubadilishwa wizara. Mwingine ni Adam Malima aliyeonyesha uhuni wa wazi pale alipoibiwa fedha na vitu vingine hotelini Morogoro alipokuwa amejifungia na bunduki mbili bila maelezo.
Ajabu, Malima hakukaripiwa wala kuwajibishwa zaidi ya kupewa wizara nono ya fedha. Hii ni nini kama si utawala wa kifalme? Kule Saudia wana wa ukoo wa kifalme huwa hawakosei hata wakikosea hawaadhibiwi kwa vile nchi ni mali ya ukoo wao.
Uzuri wa Saudia na Kuwait wametangaza wazi kuwa wanatawaliwa na ufalme. Nasi basi tutangaze kuwa tunatawaliwa na wafalme ili kuepuka kupoteza mabilioni ya shilingi kushiriki uchaguzi unaowarejesha wafalme wale wale.
Kwa kinachoendelea, jinsi kinavyokera na kuchefua, kama Mwalimu Nyerere angetokea kufufuka, basi angeomba afe haraka ili asishuhudie kufuru hii itokanayo na upogo na ulafi wa ajabu.
Maana asingetaka kuishi hasa kama angeshuhudia yale aliyotolea jasho na hata kuwa tayari kufia yakimomonyolewa na wale aliowasaidia kutoka kwenye ujinga na umaskini wakatumia nafasi hiyo kufanya mambo ya kilafi.
Tumalizie kwa kuwasihi Watanzania waukatae huu ufalme uchwara unaopitishwa mlango wa nyuma tena kwa kutumia eti demokrasia ambayo inaendelea kupokwa na vigogo na watu na familia zao.
Hakika kufuru ya Chalinze na Kalenga inafanya nimkumbuke sana Mwalimu Nyerere. Bahati mbaya wenzetu hawakujifunza kwa yaliyowapata kina Muamar Gaddafi.
Chanzo: Tanzania Daima Machi 12, 2014.
2 comments:
Mwl. Mhango, hayo manung'uniko uloandika achana nayo tu. Chama alichoasisi Julius Kambarage kilikuwa ni cha wakulima na wafanyakazi. Hiki cha sasa siyo. Hiki cha sasa ni cha matapeli, walafi na mafisadi.
Siku hizi kuna watoto hata wanaalikana kwenda kujiunga ili kupiga "fursa".
Anon
Nakubaliana nawe ila sitaacha kupiga kelele angalau walevi wasikie na kustuka na kuamua kuchagua chama wanachoona kinafanana nao badala ya kuendelea kuburuzwa na kutumiwa.
Post a Comment