Kuendelea kuwa na balozi Ombeni Sefue–ambaye, kimsingi, alikuwa mshauri mkuu wa rais mstaafu Jakaya Kikwete anayedaiwa kuacha nyuma madudu kibao–ni licha ya kuchafua sifa ya serikali ya awamu ya tano, ni kuendelea na madudu yale yale bila kujua au kwa kujua jambo ambalo litaishushia hadhi serikali ya awamu ya tano bila sababu zozote za msingi. Sijui kama rais John Pombe Magufuli analijua hili. Kwa vile Magufuli ameingia na staili mpya ya utendaji, anapaswa kuwa na watu wapya pale asipolazimika kama vile kwenye uteuzi wa baraza la mawaziri.
Mfano mdogo wa karibu ni ikulu hiyo hiyo ikiwa chini ya Kikwete na Sefue huyu huyu ni kuhusishwa kwenye kashfa ya Escrow ambapo Mnikulu wa Ikulu, Shaban Gurumo alikiri kukatiwa shilingi 80,850,000 na mtuhumiwa mkuu wa Escrow. Kuna uwezekano fedha hii ni kidogo tu inayojulikana na inaweza kuwa iliingia kwenye mikono mingi. Japo hatusemi kuwa Sefue alishiriki moja kwa moja, kama ofisi yake ilishiriki basi naye alishiriki.
Bila kupindisha maneno, Sefue atakuwa ni jipu linalopaswa kutumbuliwa kama ilivyokuwa kwa msemaji wa Kikwete Salva Rweyemamu aliyeonjeshwa ulaji akasahau kuna kesho hadi alipofurushwa hata kabla ya Magufuli kukanyaga ikulu. Hivyo, wengi wanaojua jinsi serikali zinavyofanya kazi, wanashangaa Magufuli kuendelea kuwa na Sefue kama msaidizi wake mkuu wakati alishaonyesha alivyoshirika kwenye uoza wa serikali iliyopita si kama mtu binafsi bali kwa nafasi yake.
Kwa vile Magufuli ni mpya kwenye kazi yake, wengi wangedhani angeanza na timu mpya kama alivyopatia kwa kumteua waziri mkuu mpya asiye na doa au makamu wa rais. Hata kwa wasaidizi wake hasa katibu kiongozi lazima ateue mtu toka nje ya uoza uliopita. Maana katibu kiongozi ndiye mpishi mkuu wa sera za serikali. Na lolote lililotendwa na serikali yake lazima limkumbe. Inakuwaje Magufuli aeleze uoza alioukuta kama ulivyoachwa na mtangulizi wake ashindwe kumwajibisha Sefue. Kimsingi, kama Sefue ni mchafu hivyo–na si kwa kumpakazia hasa kutokana mapishi aliyofanya wakati wa Kikwete–uwezekano wa kumchafua Magufuli hata kuhatarisha heshima na sifa yake ni mkubwa tu. Ni suala la wakati ukweli utadhihirika na uongo utajitenga.
Kwa hatua za hatari anazochukua Magufuli dhidi ya mafisadi wakubwa na wadogo, uwezekano wa kula na wabaya wake ni mkubwa kiasi cha kuhatarisha hata maisha yake. Kwa wanaojua uzalendo wa marehemu Edward Sokoine na alivyojikuta akipigana vita peke yake kwa kuamini kuwa aliokuwa nao walikuwa naye wakati si kweli, hawatashangaa kusoma haya na kuyafanyia kazi. Hata hivyo, tuweke bayana. Hakuna tunayemshuku zaidi ya kutaka kuonyesha umuhimu wa Magufuli kuwa na timu mpya ili aendelee na mambo yake mapya ambayo–yanawafurahisha watu wa chini–la yanawakera wakubwa ambao walizoea ufisadi kama sehemu ya kujipatia mlo wao na si mlo tu bali utajiri wa kutaka kuridhisha vichaa na uroho na roho mbaya za vitu. Maana wengine hawaibii umaskini wala uhitaji bali roho mbaya na mazoea mabaya.
Tunafahamu kuwa ufisadi mwingi hasa mkubwa nchini huwa haufanyiki bila kuhusisha ikulu mara nyingi. Rejea kufichuka hivi karibuni kuwa mhindi aliyetorosha wanyama wetu alikuwa na vibali toka Ikulu. Hivyo, tunajua fika kuwa ufisadi mwingi unaozidi kuibuliwa lazima utaigusa ikulu kwa njia moja au nyingine na Sefue hatanusurika hasa ikizingatiwa kuwa amekaa pale kwa muda mrefu, ukiachia mbali serikali yake na Kikwete kufanya madudu mengi ambayo yanamlazimisha rais Magufuli kuchukua hatua kali kiasi cha kuwakwaza wengi waliozoea ubwete na dezo chini ya serikali hiyo. Ushahidi mwingine wa kimazingira ni ile hali ya serikali iliyopita kutowachukulia hatua watuhumiwa wa ufisadi na uchafu mwingine kama vile ujambazi na uuzaji mihadarati ambavyo rais mstaafu alisema alikuwa ameletewa orodha na vyombo vya usalama akaamua kuiatamia kwa sababu ajuazo. Hata hivyo, kwanini kuhangaishwa na watu wachache wakati Tanzania ina idadi ya watu inayozidi milioni 40. Kwanini kung’ang’ania viraka–na hata magamba wakati tunao watu wengi tena wenye uwezo wa kutosha wanaoweza kufanya kazi husika?
Kuzidi kuonyesha kuwa ikulu lazima ilishiriki kwenye ufisadi mwingi chini ya utawala uliopita, rejea mfano mwingine ni kuuzwa kwa mbuga ya wanyama ya Loliondo chini ya utawala wa awamu ya pili. Nani hajui kuwa dili lote lilifanyika ikulu?
Tumalizie kwa kumtaka ima Magufuli ateue timu mpya na katibu kiongozi mpya au Sefue mwenyewe ajing’atue ili kuendelea kulinda heshima yake iliyobaki. Akifanya hivyo, atakuwa amejijengea heshima na kuacha mzigo umuandame bosi wake kuliko yeye kung’ang’ania kukaa ikulu wakati watanzania walio wengi wanahoji: Iweje Sefue aonekane safi wakati ikulu na serikali alivyotumikia kwa muda mrefu vimeonyesha wazi kuwa vichafu? Tunaomba kutoa hoja tena kwa upole. Ni ushauri wa bure tu.
Chanzo: Mwanahalisi Feb., 29, 2016.