How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Friday, 26 February 2016

Mlevi kumualika Obasanjo uchakachuaji Zenj


            Baada ya rafiki yangu wa zamani Jenerali Olushe Obasanjoo kuonyesha asivyo mwoga wala mnafiki kwenye uchakachuaji uliosha kwa M7, mlevi anapanga kutia timu Abeokuta kwenda kumpa shavu na kumtaka aje Zenj na kupayuka baada ya uchakachuaji unaotegemea kufanyika hivi karibuni. Jamaa hakumlazia damu mfalme M7. Alizoza wazi kuwa alichakachua na kuwaburuza wapingaji wake. Kama asemavyo Dk Kanywaji Mugful, Msemakweli ni mpenzi wa Mungu na si Mnafiki. Laiti Mugful angeamua kushughulikia unafiki wa kuchakachua kura, nadhani angeishi kwa kadri ya anachohubiri.
            Obasanjoo alikuwa mkuu wa msafara wa Jumuia ya Makoloni ya Kiingilish aliyesimamia uchakachuaji ambapo mfalme M7 alishinda kwa mara ya ishirini. Kwa vile nasi tumekuwa na Jechia Salimu Jechia ambaye alifuta matokeo ya uchaguzi uliopita bila sababu za msingi hata za kilevi, tunaamini tukipata wapayukaji kama hawa huenda wapuuzi wanaoharibu mambo wanaweza kunywea. Kwanza wanajua huyu jamaa licha ya kuwahi kuwa rahis ni mjeshi tena mwenye cheo cha jenerali kama mimi ambaye tulikutana kule kwa Aldershottukichukua mafunzo yetu ya kijeshi toka kwa mkoloni wetu kama ilivyokuwa utamanduni. Maana, wakoloni kwa kujua ujuha wetu waliamua kufundisha wajeshi wetu ili waweze kuangusha serikali ambayo hawakuwa nayo maslahi kama ilivyotokea kule Nigeria, Ghana na kwingineko.
            Nani alijua kuwa mzee Obasanjoo angemtolea nje Kagutuka M7 kuwa alishinda kwa nguvu ya mituringa ya kutumia ndata na ndutu? Kwa vile tushajua ushindi wa bao la mkono mara nyingi hutegemea ndata na masoja, lazima tuhakikishe tunawaalika washikaji wetu wenye vifua kama vile mzee Olushe waje kutupa kampani kuhakikisha hakuna jambazi wa kura anayechakachua matokeo.
            Kama siyo kufanya mambo kibongobongo nadhani walevi wa Zenj walipaswa kujua sababu ya kufutwa matokeo na nani alikuwa ameshinda kabla ya kuelekea kwenye vituo vya kupiga kura ili kuepuka kwenda kubariki uchakachuaji kama ilvyofanyika UG juzi. Maana kwa tuliofuatilia maandalizi ya uchakachuaji wa UG tulishajua mshindi hata kama ameshinda kiharamu. Ukiangalia upande wa Zenj pia, hata kama huvuti bangi na kupiga bwimbwi kama mimi unaweza kutabiri nani ataibuka mshindi hasa ikizingatiwa kuwa waliowahi kusema kuwa hawawezi kuachia ulaji kwa vijikaratasi yaani kura ya kula. Hivyo, ina maana kwa kutumia mitutu, uchakachuaji na jinai nyingine lazima itumike sayansi ya mtaalamu mmoja wa uchakachuaji aitwaye Nipe Ninaya Mapepe aliyekuja na nadharia ya bao la mkono.
            Nikiangalia wapingaji walivyoshupaa kutaka kujua kilichosababisha kufutwa matokeo Zenj huku walaji wakiminya, nagundua kuwa upande ulio kimya lazima ushinde kwa vile haulalamiki kwa vile unajua kilichofanyika kwa maslahi yake. Maana, kwa jinai aliyetenda Jechia–ambayo, bila shaka, mzee Olushe angelaani kwa kinywa kipana–hakuna mtu mwenye akili asiyenufaika nayo anaweza kuikalia kimya hata asilalamike achia mbali kutolaani. Japo wengi wanaogopa kuronga kuwa kilichotokea Zenj ni dhuluma, mlevi–kwa vile huwa hana breki–anasema wazi wazi kuwa kilichofanyika ni jinaiiiiii, dhulumaaaaaa na aibuuuuu kwa kaya yooote come what may.
            Japo mimi si tapeli anayejifanya mtabiri kama yule habith Shehena Yaya ambaye alisisha utapeli wake kwa kitegemezi chake, naweza kutabiri nani atashinda Zenj. Ni rahisi kutabiri kama ilivyo kwa kichanga kulia. Hata hivyo, hawa majipu na mabusha wanaochakachua uchaguzi wanapaswa kujua kuwa tunakokwenda wanaweza kuleta machafuko. Kwani lazima waongoze wao wakati wameishaonyesha kuchemsha kila hali tena kwa miaka nenda rudi?
            Kwa vile hawa jamaa hawataki kuacha nchezo wao, Mlevi anataka kufunga safari–tena kwa kujigharimia–kwenda kumualika mzee Olushe aje asimamie uchaguzi wa Zenj.  Baada ya kufika Abeokuta na kumwalika Olushe, nitamuomba akifika awaulize akina Jechia sababu hasa za kufuta matokeo ya uchaguzi halali na kwanini na kwa faida ya nani na walikatiwa kiasi gani na wanategemea nini huku tuendako iwapo walevi watazinduka toka ulevini na usingizini. Kuna haja ya walevi kuzinduka na kuondoa ving’ang’anizi wanaotaka kuwa wafalme kupitia sanduku la kura kama ilivyo kwa M7 ambaye ameanza kutawala UG wakati nikiwa darasa la saba na sasa mwanangu anamaliza chuo. Mijitu mingine, imezeeka hata akili lakini bado inajiona ndiyo yenye akili kuliko wengine kiasi cha kukutaka kuendelea kuwala na kuwatawala. Ishindwe na ilegee. Kwanini isiige mfano wa Olushe aliyetawala na kuwaachia wengine?
            Ngoja nimtumia ujumbe brother Olushe kupitia hapa. Kaka, kwanza nakukaribisha Bongo uje ujienjoi. Ila sitaki uje na wale jamaa almaarufu mumu wasije kuwaliza walevi wangu kwa ile kitu yao ya Kinigeria. Nakuomba sana brother uje hapa uwapayukie akina Jechia ambao inaonekana lisirikali linawatumia kuchakachua kura ili chama twawala kiendelee kula kule Zenj. Bradha Shining umeinyaka hiyo?
            Ala kumbe nimelewa!
Chanzo: Nipashe, Feb., 27, 2016.

No comments: