Waathirika wengi walisikika wakiilaumu serikali wakiuliza ilikuwa wapi hata baada ya kuiona ikifanya kazi ya ubomoaji wa nyumba zilizojengwa kwenye maeneo hatarishi, ya wazi na mengine yaliyojengwa kinyume cha sheria ama kutokana na kuvamia viwanja vya wenyewe au viwanja vya wazi. Pamoja na malalamiko ya wahanga kutokuwa na mashiko, bado yana somo kwao na kwa serikali na kwa watanzania kwa ujumla. Baadhi ya masomo toka kwenye kadhia hii ambayo imesababishia usumbufu watu wengi hasa wa kipato cha chini –pamoja na mambo mengine –ni:
Mosi, je serikali imejifunza nini? Serikali inapokuwa legelege–au tuseme jipu–inajikuta kwenye lawama kama hizi hata bila sababu ya msingi. Japo wakati wahanga wanauliza serikali ilikuwa wapi, wanapaswa kujiuliza nao: Kwanini hawakufuata sheria?
Kimsingi, swali kuwa serikali ilikuwa wapi–ingawa serikali haikujibulinatuleta kwenye hitimisho kuwa ujenzi holela si kosa la waathirika tu bali hata serikali yenyewe. Je serikali imejiandaa vipi kukomesha mchezo huu ili kuepuka kuonekana inawaonea wanyonge kwa vile ina maguvu ukiachia mbali kuepuka kuulizwa swali lile: Je serikali ilikuwa wapi miaka yote hii? Je serikali inamejifunza nini kuhakikisha hiki kilichotokea hakitarudiwa siku zijazo jambo ambalo litazidi kuongeza lawama na mateso bila sababu?
Pili, somo jingine ni kwamba baadhi ya watu wetu ni wasahaulifu ukiachia mbali kukwepa kuukubali na kuufanyia kazi uhalisia na ukweli. Je makazi ya mabondeni si hatarishi kwa wakazi wake na taifa kwa ujumla? Hivi unapojenga kwenye mabonde na vyanzo vya maji unategemea nini zaidi ya uharibifu mkubwa wa mazingira ambao athari zake huwakumba waliokuwamo na wasiokuwamo, waliokwishazaliwa na ambao bado hawajazaliwa? Hapa tunaongelea uharibifu wa mazingira. Bado hatujagusia athari za makazi yasiyo rasmi–mara nyingi kuwa–chaka zuri kwa uhalifu wa aina mbali mbali kuanzia majambazi hata wala na wauza unga na makazi yasiyo na mpangilio ambayo ni vigumu kuyahudumia. Je serikali ilikuwa wapi? Jibu la swali hili nadhani kila aliyeshuhudia ubomoaji anaolo. Tumeiona serikali inayohojiwa ilikuwa wapi. Sasa inaanza kufanya kazi yake bado watu wanahoji ilikuwa wapi. Hapa suala si kutokuwapo kwa serikali bali kuangalia namna ya kumaliza kadhia hii kwa kuangalia makosa ya pande zote ili serikali iwajibike lau kuwawezesha wahanga kupata makazi mengine tokana na uzembe wake wa muda mrefu. Hapa tunapata swali jingine muhimu:Je serikali imedhamiria kufanya zoezi hili kuwa endelevu au kuingiza siasa na kuanza kulivuruga kwa kuogopa madhara yake kisiasa hasa kwenye uchaguzi ujao? Ni vizuri sheria zikatumika kisheria na si kisiasa wala kimazoea. Hapa lazima taifa liwajibike kwa pamoja kuhakikisha haki inatendeka pande zote kwa usawa na haraka. Hata hivyo, inakuwa vigumu kuibebesha mzigo serikali kwa kisingizio kuwa haikuwakataza au kuwaondoa wote waliojenga mabondeni wakati walipoanza. Kimsingi, kila mtu anapaswa kujua sheria ili asizivunje akaumia au kupata hasara kama ilivyotokea kwa wakazi wengi wa mabondeni waliobomolewa, na watakaobomolewa nyumba zao. Si utetezi wenye mashiko kwa mwizi kuhoji kwanini mwenye nyumba au mali hakufunga mlango ingawa kiakili kila mwenye mali anapaswa kuzilinda kwa kuwa na milango imara na kuchukua tahadhari zote ili kuepuka madhara yatokanayo na wizi.
Kwa wanaojua gharama maendeleo, serikali haipaswi kuogopa kunyimwa kura kwa kulinda sheria na kanuni. Cha msingi, ifanye vitu vionekane ili wale wanaohisi walionewa waone picha tofauti kuwa kumbe hawakuonewa. Itakuwa ni kitanzi kisiasa kama serikali itawahamisha wakazi wa mabondeni na isifanye kitu kitakacholeta mabadiliko kama vile usafi wa maeneo husika ukiachia mbali kubadili na kurekebisha mfumo mzima wa upatikanaji na usajili viwanja.
Somo jingine ni kwamba serikali inapaswa kuwa kama hewa. Lazima iwepo kila mahali usiku na mchana. Isingoje watu waanze kuweka vibanda vya muda maeneo yasiyoruhusiwa halafu ije kubomoa baada ya wahusika kuwa wameanzisha makazi ya kudumu. Makazi yote yanayoiingiza serikali majaribuni yalianza na makazi ya muda ambayo mamlaka za wakati ule hazikuyazuia na sasa zinalaumiwa. Tunajua chanzo cha ujenzi holela na uvamizi wa viwanja. Mara nyingi hasa wakati wa karibu na uchaguzi, wanasiasa wamekuwa wakiongopa kuwaondoa watu mabondeni kwa kuhofia kunyimwa kura. Pili, zoezi la kuhamisha wakazi wa mabondeni –mara nyingi –limekuwa likitegemea nani yuko madarakani. Mara nyingi –kwa Dar es Salaam –hisia za kuhamisha watu wa mabondeni lilitegemea nani alikuwa mkuu wa mkoa. Kwa vile serikali –kwa ujumla wake –imeamua kushughulikia tatizo hili, basi inahakikisha inalimaliza kabisa huku ikitangaza wazi kuwa atakayejenga mabondeni atakamatwa na kutozwa faini na kufungwa ili kukomesha malalamiko na madhara yatokanayo na ujenzi holela.
Tumalizie kwa kuwasisitizia wananchi umuhimu na faida za kufuata sheria. Unapofuata sheria na kuepuka njia za mkato, unakuwa na uhakika wa makazi na mali yako.
Chanzo: Tanzania Daima Februari 3, 2016.
No comments:
Post a Comment