How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Monday, 8 February 2016

Tulaani udhalilishaji wa wabunge


            Kitendo cha hivi karibuni cha polisi kuingia bungeni na kuwabughudhi, kuwadhlilisha na kuwaondoa wabunge bungeni–licha ya kusikitisha, kustua na kudhalilisha–kinapaswa kulaaiwa na watanzia wote bila kujali itikadi zao kwa nguvu na namna zote. Kwanza, bunge ni muhimili na taasisi inayopaswa kuwa huru, kuheshimiwa na kutoingiliwa na yeyote au muhimili mwingine wa dola katika shughuli zake. Chini ya dhana ya mtenganisho wa madaraka wa mihimili ya dola (Separation of power), hakuna muhimili wenye mamlaka kuliko mwingine au unaopaswa kuingilia mamlaka na shughuli za muhimili mwingine.  Mwanafalsa Charles Secondat de Montesquieu (18 January 1689–10 February 1755) anatambulika kama Msomi aliyechangia kwa sana juu ya uwepo wa dhana ya mtenganisho wa madaraka. Aliwahi kusema, “The love of democracy is that of equality” mapenzi ya demokrasia ni mapenzi ya usawa” wa wote na mihimili ya dola.
            Kisheria, dola hujengwa na mihimili mitatu yaani Bunge, Mahamaka na Utawala. Na mihimili yote hii ina haki na mamlaka sawa na inapaswa kufanya kazi kwa kuheshimiana bila kuingiliana wala kunyanyasana.
Pia, hakuna muhimili unaoruhusiwa kisheria kufanya kazi ya muhimili mwingine au mingine. Na huu ndiyo msingi mkuu wa utawala bora na wa sheria. Sasa unashangaa, nani huyu aliamuru jeshi la polisi–si kuingia bungeni–tu bali kuwadhalilisha waheshimiwa wabunge? Unauliza maana ya kinga ya wabunge–ukiachia mbali ukweli kuwa huyu aliyefaya hivyo, licha ya kuvunja katiba ambalo ni kosa kubwa kuliko yote nchini, alipata wapi mamlaka ya kufanya hivyo na kwa faida ya nani na kwanini?
            Kuna haja ya mamlaka iliyotoa amri hii ya kuvunja katiba kujulikana na walioko nyuma ya kadhia hii kuwajibishwa mara moja kwa ajili ya heshima ya bunge, taifa na wabunge kwa ujumla. Maana, kilichofanyika ni suala la kisheria linalobaini kuwa kuna mgongano wa mamlaka jambo ambalo ni hatari kwa ustawi na heshima ya taifa. Kitendo cha polisi kuingia bungeni ni kulinajisi bunge mbele ya wananchi ambao ndiyo wenye serikali. Hivyo, aliyetoa amri lazima ajulikane na kushughulikiwa vilivyo ili liwe somo kwa wengine wasiojua mipaka na kanuni za mamlaka yao. Mbunge–si mtu binafsi awe wa upinzani au wa chama wa chama tawala–ni taasisi na ni kielelezo cha wale anaowawakilisha bungeni. Ndiyo maana tunatumia fedha na muda mwingi wa umma kuwachagua ili wafanye kazi zao bila woga, kubughudhiwa wala kudhalilishwa. Na hii ni kwa dunia nzima na si Tanzania tu. Je tunafundisha nini vizazi vijavyo kama tunashindwa hata kusimamia na kuheshimu sheria tulizojiwekea wenyewe kwa hiari yetu?
            Leo polisi wanavamia bunge na kuwadhalilisha wabunge. Je watashindwa kuwadhalilisha hata kuwaua wananchi kama ilivyozoeleka? Watazoea na kesho watavamia mahakama na kufanya kama watakavyo. Je hapa hatujajenga taifa la vurugu na uvunjaji na ufujaji sheria na mamlaka? Nani anataka serikali na taifa lisilo na nidhamu kama hili? Je hawa waliotoa amri ya kizembe, kihalifu na kidhalilishaji wanawafunidisha nini polisi zaidi ya tabia mbaya ukiachia mbali kuwadhalilisha wabunge jambo ambalo linawadhalilisha wabunge wote. Kama si kutawaliwa na kutekwa na siasa zilizojaa ushabiki wa vyama, wabunge walipaswa kuisusia serikali na kupiga kura ya kutokuwa na imani nayo. Wanao uwezo huu ingawa hawautumii kutokana na siasa za majitaka zilizojikita kwenye ushabiki wa vyamba badala ya maslahi ya taifa na bunge kwa ujumla.
 Mbunge Said Kubenea wa Ubungo (CHADEMA) alikaririwa hivi karibuni akisema kuwa baadhi ya wabunge walivuliwa hereni hata shanga. Ni aibu kiasi gani? Mbunge ni mbunge bila kujali kama ni wa upinzani au chama tawala. Hivyo, unapomdhalilisha, kumbughudhi, kumnyanyasa, kumkwida na kumtoa nje ya bunge vitendo hivyo havimlengi mbunge kama mtu bali taasisi nzima ya ubunge, wabunge wote–na juu ya yote–jimbo zima lililomtuma aliwakilishe Bungeni. Ukimvua nguo mwanamke yoyote unakuwa umemvua mama yako nguo. Hivyo, kitendo hiki kinapaswa kulaaniwa. Wabunge wana hadhi na heshima yao ambayo haipaswi kuvunjwa wala kushushwa kwa namna yoyote. Ningeshauri wabunge wa wote waliodhalilishwa wagomee bunge ili wahusika waliowadhalilisha wajulikane na kuchukuliwa hatua kabla ya serikali–ambayo ndiyo ina dhamana na jeshi la polisi kuwaomba msamaha na kuahidi itafanya hivyo tena–ndipo warejee bungeni. Tunataka utawala bora na wa sheria unaozitumia sheria bila ubaguzi, upendeleo wala unyanyasaji. Cheo ni dhamana. Kesho upinzani unaweza kuunda serikali na kuamua kulipiza kisasi jambo ambalo litaliingiza taifa kwenye machafuko yasiyo ya msingi. Kisheria, polisi haawapaswi kujihusisha na siasa za vyama ili kutenda haki sawa kwa wote. Je unapowatuma polisi kuwaondoa wabunge wa upinzi, hujawahusisha kwenye siasa za vyama jambo ambalo ni kinyume cha sheria? Kwanini kutumia polisi au FFU wakati bunge linapaswa kuwa na polisi wake wa kibunge? Huu ni uhuni wa hali ya juu sana ambao si wa kualaaniwa tu bali wa kupaswa kupingwa hata kwa maandamano.
            Tumalizie kwa kutaka serikali ifanye yafuatayo:
Mosi, iwaombe masamaha wabunge na kuwaacha wabunge waunde tume ya kushughulikia kadhia hii.
Pili, waliohusika wafukuzwe kazi mara moja huku wakingoja kuchukuliwa hatua nyingine za kisheria kwa kuvunja katiba.
Tatu, rais mwenyewe atoe tamko la kulaani uhuni huu huku akiahidi serikali yake kutorudia tena jinai hii.
Mwisho, itungwe sheria ya kuzuia polisi kujihusisha na shughuli zozote za bunge vinginevyo iombwe na bunge kufanya hivyo kama kuna ulazima kisheria. Leo mnaingiza polisi. Kesho mtaingiza majeshi. Tunakwenda wapi? Bunge ni chombo kitukufu kisichopaswa kudhalilishwa wala kuingiliwa.
Chanzo: Mwanahalisi, Feb., 8, 2016.

No comments: