Taarifa kuwa baadhi ya wezi na wakubwa katika kaya yetu walikuwa ikiingiza mafuta bila kulipiwa ushuru kwa miaka mitano zimewaudhi wanakijiwe nusu ya kufikia kutaka kupasuka. Licha ya kulaani ujambazi huu, kijiwe kinataka hata rahis aliyepita achunguzwe na kufikishwa kwa pilato. Maana inavyoonekana huu ni mpango uliohusisha wakubwa wa juu kwenye lisirikali.
Kapende anaingia akiwa ameramba suti leo utadhani anakwenda kurora! Kwa wasiojua kurora ni kuoa. Anakula mic, “Jamani mmesoma hii habari juu ya waduwanzi na majambazi wakubwa kufunga mita ya mafuta na kuingiza wese kayani kwa miaka mitano bila kulipa hata senti? Hivi tutaliwa hivi hadi lini?
Mpemba anakula mic, “Mie wallahi jana hata sikula. Baada ya kupata hizi habari nilitamani nshike panga na kukata ntu kichwa wallahi.”
Mpemba anakula mic, “Mie wallahi jana hata sikula. Baada ya kupata hizi habari nilitamani nshike panga na kukata ntu kichwa wallahi.”
Mbwamwitu anamchomkea Mpemba, “Kuchukia hakusaidii wakati wenzio wakifurahia. Tunapaswa kushinikiza wahusika nao wazimwe tena kwa miaka 500.”
Dk Msomi Mkatatamaa anaamua kutia buti mapema tokana na uzito wa mada ya leo, “Ukisikia mara nyingi tunasema kaya ilikuwa kwenye autopilot chini ya Njaa Jaa la Kaya kwa miaka kumi ndiyo huku. Japo kusema tunaliwa kunakera na kuamsha hasira, hakuna ubishi tumeliwa kwa miaka kumi tutake tusitake. Hapa tunaongelea mafuta. Je ni mazabe mangapi hajafumliwa? Utashangaa hawa unaowaona wakitukoga kwa ukwasi wao ndiyo hao hao walioasisi na kutenda kadhia hii ambayo ni maangamizi ya kujitakia yatokanayo na upogo, upofu na uroho wa tunaodhani ni wenzetu. Lazima hapa Dokta mwenzangu Kanywaji achukue hatua kuwafillisi na kuwazima kwa miaka 500 kama asemavyo mheshimiwa Mbwamwitu. Enough is enough.”
Kabla ya Msomi kuendelea, Mijjinga anamchomekea na kusema, “ Sitaki kukukatisha tamaa kama jina lako. Tokana na mfumo wa hovyo tulio nao, utashangaa wahusika kufikishwa kwa pilato na kutoa chochote kitu na kuhukumiwa kusafisha hospitali kama majizi tuliyoshuhudia juzi yakipewa adhabu hii. Waarabu wa Pemba hujuana na kwa vilemba na lao ni moja na wanakula pamoja.”
Msomi anaendelea, “Nakubaliana nawe mheshimiwa Mijjinga hasa ikizingatia kuwa ufisadi katika kaya yetu ni wa kimfumo ambao dokta mwenzaangu Kanywaji anaonekana kuukunakuna badala ya kuufumua na kuufuma upya. Bila kuja na sheria za kupiga watu shaba, tutaendelea kuumia, kulalamika na kutwanga maji kwenye kinu.”
Msomi anakohoa kidogo na kuendelea, “Kama dokta Kanywaji amegundua hili, basi na mtangulizi wake alijua, ila kwa vile kuna namna alinufaika na ujambazi huu, aliamua kunyamaza na kupiga fedha. Wako wapi majambazio wa Escrew au EPA ambayo Njaa Jaa Kaya alituhumiwa moja kwa moja pamoja na Ben Tunituni Makapi kuasisi na kutekeleza? Sijamsikia dokta Kanywaji akiwatumbua jipu zaidi ya kuhangaika na majipu uchungu huku majipu na mabusha yenyewe akijifanya hayaoni wala kuyajua.”
Mipawa ananyakua mic, “Hata nami sina shaka na usemayo kuwa Njaa Jaa Kaya alijua na kuwa nyuma ya kila kitu kama ilivyokuwa kwa Richmonduli aliyomtwisha Ewassa akabaki anachekelea kama kawaida yake. Lazima naye atumbuliwe jipu tena mara moja bila kumwangalia nyani usoni hata kama ni mkubwa kama sokwe.”
Mgosi Machungi aliyekuwa anarejea kutoka msalani anaamua kula mic, “ Hapa azima tiambiane ukwei. Njaa Jaa Kaya anahusika moja kwa moja na hawezi kujinashua hapa. Nami naanza kuwa na wasi wasi na dokta Kanywaji hasa kwa ukimya na ugoigoi wake katika kushughuikia majipu na mabusha. Kwei leo nimekubai tinaiwa hata kama ni neno baya kutumia. Hata hivyo, nao akina Njaa Jaa Kaya azima waiwe watake wasitake. Kwanini tisiandamane kwenda ikuu kumshinikiza dokta Kanywaji awazime hawa mbwa miaka 5,000 ii iwe somo kwa wengine wanaodhani kaya yetu ni shamba la bibi kwa kila nyani kujiia atakavyo?”
Kanji anaamua kutia guu kinomi, “Hata mimi roho iko uuma sana. Sasa kama jambazi yote hii nafanya witu kama hii na Jaa Jaa Kaya nakaa naangalia kwanini hapana peleke yeye pango haraka jamani?”
Mheshimiwa Bwege anaamua kukwanyua mic, “Mimi sina imani na yoyote hasa ikizingatiwa kuwa dokta Kanywaji na Njaa Jaa Kaya wote ni watoto wa chata lilelile la kulindana, kulinda na kufanya ufisadi. Bila kunkamata Njaa Jaa Kaya na kutupa lupango, kila kitu ni sanaa na maigizo kama kawa. Haiwezekani kampuni lililofanya hujuma hili linajulikana halafu tunaendelea kupiga kelele. Bila shaka kampuni hili ni mali ya wakubwa majambazi waliowezesha upigaji huu wa hatari ambao ni jinai ya maangamizi kwa wachovu wote.”
Mzee Maneno anakwanyua mic, “Kweli kaya yetu ni ya waliwaji. Hamkusikia vigogo wawili wakigombea nyumba ya umma waliouziana kana kwamba tuna nyumba za kutosha kwa wachovu wetu? Hamuoni dokta Kanywaji alivyowagwaya kalu na abusiii waliojazana kwenye nyumba za Msajili wakati wana majumba kibao wakipangisha kwa ma-TX? Nani anamdanganya nani? Napendekeza tujichukulie sheria mikononi kama tunavyowafanyia vibaka. Twende tukachome ofisi za hilo kampuni huku tukiwasaka majambazi wote mmoja mmoja na kuwapiga nari na; kuondoa udhia.”
Kijiwe kikiwa kinachanganya lilipita gari la kampuni ya Oilryx; tulilikimbiza na kulipiga nari.
Chanzo: Tanzania Daima Feb., 24, 2016.
No comments:
Post a Comment