Taaria kuwa katika wimbi la kukamata wanaohujumu nchi yetu limemnasa mtoto wa aliyewhi kuwa Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Suleiman Kova aitwaye Masoud linaweza kufichua mengi. Je ni watoto wangapi wa vigogo wako kwenye ulaji wakipiga dili huku wananchi wetu wakiendelea kuteseka bila sababu zaidi ya uroho na upogo wa watawala wetu? Vyombo vya habari vilikaririwa vikiripoti, gazeti la Jamhuri (Januari 6, 2016) liliandika, “JAMHURI limepata malalamiko kutoka kwa wafanyakazi wa Bandari na watu walioko ndani ya Jeshi la Polisi wakihoji ilikuwaje mtoto wa Kova, aliyehusishwa na upotevu wa makontena amekamatwa na kupewa dhamana usiku wa Desemba 29, 2015 huku baadhi ya wakurugenzi waliokamatwa awali wakilazwa ndani.”
Sijui kama Dk Magufuli alisoma gazeti hili au watu wake na amechukua hatua gani. Hivi tunaipeleka Tanzania wapi na kwa faida ya nani tunapoendeleza mchezo mchafu wa kulindana hivi? Kukna uwezekano kuwa kukamatwa kwa mtoto wa Kova, Masoud ni sawa na tone la maji baharini, wako watoto wengi wa vigogo ambao hawajakamatwa na ndiyo sababu hadi leo suala la kauwafikisha mahakamani linakuwa la kusua sua.
Mmoja wa wasomaji aliandika yafuatayo baada ya habari hii kutoka, “Hebu fikiria mameli makubwa yanayoleta mafuta kila siku yanapaswa kulipa TPA shilingi ngapi? Sasa malipo mengi hayafiki sehemu husika maana kuna namna wanagushi kisha wanagawana na ni kikundi cha watu hao hao.”
Siyo uzushi wala siri. Watoto wa vigogo na vigogo wenyewe wanafahamika. Wako kwenye bandari zote, mipaka, viwanja vya ndege, mipakani, wizara, kwenye mabenki hasa BoT kwingineko kwenye ulaji wa haraka. Wapo mbuga za wanyama, madini, biashara hata kwenye balozi zetu nje wapo ukiachia mbali kwenye vyuo vingi vikuu vya nje walikopolekwa ima kwa scholarship za watanzania au fedha ambayo wazazi wao waliwaibia watanzania.
Lazima wakamatwe, wafilisiwe na ikiwezekana wafungwe. Kuwapata si kazi. Ni rahisi kuwasaka na kuwafichua watoto wa vigogo au ndugu zao walioajiriwa kwa upendeleo huku vijana wetu wengi wanaomaliza vyuo hawapati kazi ukiachia mbali kuendelea kuhangaishwa na kongwa la kudaiwa mikopo waliyochukua wakati wakisoma. Chukua orodha ya wafanyakazi wa serikali, utagundua uoza mwingi tu unaoifanya Tanzania isiwe na tofauti na Zaire ya Mobutu au Libya ya Gaddafi kuhusiana na madaraka ya kutumika kifamilia. Ilianzia ikulu hadi kwa mfagiaji ambapo kila kigogo kwa ngazi yake aliunda utawala wake wa kijambazi na kula kwa mikono na miguu tena bila kunawa. Kama mainzi, tabaka hili licha ya kula kwa miguu na mikono bila kunawa, hunya na kutapika humo humo linamolia kama mainzi. Wakati tukilalamikia umaskini –huku utawala uliopita ukisifika kwa kwenda nje kuombaomba na kujidhalilisha –tunambiwa kuwa nchi yetu inaweza kuwa na mabilionea wengi walioupata ukwasi kwa njia ya kuliibia taifa ukiachia mbali kuajiriana kwa kujuana. Mtoa habari anasema wameiba na kuwa mamilionea wenye utajiri wa kukufuru. Ndiyo, wanakula na kunya mle mle wanamolia kama mainzi.
Gazeti liliendelea kuandika tena kwa kushangaa, “Watu wanauliza mbona kuna watu wanatolewa kafara? Kuna mtoto huyu wa Kova, Masoud Suleiman Kova. Yeye ni jipu kubwa tu, na yeye ndiyo pilot kwenye mambo haya kule kwenye ICDs. Sasa jana walikamatwa, lakini kundi lake hawakuwekwa ndani, unaona ehee?”
Kama serikali ya Magufuli haitatafuta namna ya kuwabaini na kuwatia kufuli vigogo wengi waliopenyeza watoto wao kwenye sehemu nyingi za ulaji nchini, zoezi lote linaweza kuonekana kama kushughulika na wasio na washitiri wa kuwakingia kifua wahalifu wanaotuhumiwa kwa kupoteza mabilioni ya shilingi za umma. Hivyo, tuseme bila kumung’unya maneno kuwa serikali lazima itende haki katika ukamataji, ufikishaji mahakamani na ufilisi wa wezi wanaoendelea kuhangaisha taifa letu na kulifanya maskini wakati wao wakigeuka mabilionea wa kutupwa bila sababu. Kama alivyowahi kuuliza rais Magufuli: Hivi nani alituroga jamani?
Kinachoendelea kubainika ni kwamba vigogo serikalini na kwenye taasisi zake waligeuza taifa letu mali yao binafsi na watoto wao na marafiki zao. Rejea rais Mstaafu Benjamin Mkapa alivyojitwalia mgodi wa Makaa ya Mawe wa Kiwira yeye na familia yake na marafiki zake. Ajabu, umma ulipotaka awajibishwe, rais mstaafu Jakaya Kikwete–kwa kujua uoza ambao alikwisha kutenda–alisikika akiwa nchini Sweden akisema: Muache mzee Mkapa apumzike. Kwa Kikwete mapumziko ya Mkapa yalikuwa bora kuliko maslahi ya umma! Kama haitoshi, umma sasa unashuhudia vigogo wa juu kwenye idara fulani ya serikali wakigombea nyumba waliyouziana kitapeli utadhani taifa letu lina nyumba za kutosha hadi linapata za kuwauzia vigogo wake. Huu ni wizi tu hata kama unatendwa na wakubwa. Kuonyesha mfumo wetu usivyo na uadilifu wala aibu hata kidogo, wezi wa namna hii wanajianika hata mahakamani wakigombania mali ambayo kimsingi ni ya wizi. Je kuna nyumba ngapi vigogo wameuziana? Je kuna watoto wangapi wa vigogo, marafiki na makuwadi zao kwenye taasisi za umma? Kuna haja ya rais Magufuli kutumbua majipu haya ya kweli ya kimfumo badala ya kukimbizana na mwizi mmoja mmoja au kikundi huku akifumbia macho vigogo ambao kimsingi.
Chanzo: Dira, Feb., 22, 2016.
No comments:
Post a Comment