Baada ya ndata kuingia mjengoni, kuwadunda na kuwaburuza nje wahishimiwa, Kijiwe kimekaa kama bunge kulaani na kujadili kadhia hii ya aina yake kwa kaya yetu. Kwanza, kinalaani kwa herufi kubwa na kushinikiza wote walioko nyuma ya jinai hii wawajibishwe mara moja huku hatua nyingine za kisheria zikifuatia mara moja.
Mpemba anaingia akiwa ameshikilia gazeti la CHAPABUNGE. Analibwaga mezani baada ya kuamkua na kusema, “Yakhe mwaonaje haya maajabu ya maajabu ya ndata kuingia njengoni na kudhalilisha wahishimiwa? Mie wallahi hii lantisha sana. Hivi twendapi jamani?”
“Afadhali Ami umeanzisha mada hii ambayo imekuwa ikinichanganya kiasi cha kushindwa hata kunywa gahawa hasa ikizingatiwa nina mpango wa kugombea ubunge kipindi kichajo,” analalamika Mijjinga huku akiweka vizuri kirongaronga chake mezani ili kila mtu aone alivyo na mtandao wa bei mbaya. Si unajua wabongo tena kwa madaha na kila mchovu kutaka aonekane anazo.
Kapende anakula mic, “Hata mimi kusema ukweli, kitendo hiki, licha ya kuniudhi na kunisikitisha, kimenitisha na kunikatisha tamaa kiasi cha kuhoji uwezo wa watawala wetu wa kufikiri. Wanapata wapi jeuri ya kutumia mamlaka yetu watakavyo utadhani ni mali ya mama zao? Shame on them all!” anajibu Mipawa huku akibwia kahawa yake kwa hasira.
Mgosi Machungi naye hajivungi. Anakwanyua mic, “Hawa ndata wana bahati. Wangempiga mhishimiwa wa Ushoto tingewapiga zongo bia kucheewa naapa waahi.”
Mbwamwitu anadandia, “Mhishimiwa wa Ushoto ni wa chama twawala asingepingwa ingawa kwangu waishimiwa wote ni sawa na wanapaswa kuheshimiwa sawa.”
Sofia Lion aka Kanugaembe anakula mic, “Tuliwaonya mchague Ewassa mkatuzomea. Sasa ona yanaanza kuwakuta makubwa kuliko mliyoepuka. Hakuna kitu kilichoniudhi kama wanawake wenzangu kukatiwa hata shanga na wengine kuporwa vipuri vyao na hawa wahuni walioingia mjengoni.”
Kabla ya kuendelea, Mbwamwitu anachomekea, “Eti wamekatiwa nini da Sofi? Ya kweli hayo na inakuwaje wafanye hivyo? Ina maana kabla ya kuwakatia hizo chachandu waliwapapasa au siyo au sijakupata vizuri?”
Sofia anajibu, “Unaweza kudhani na kusema utakavyo na lolote lawezekana katika vurugu. Hata hivyo, hawa wahuni wasahau kufahamu kuwa kila mwanamke ni mama yao. Hivyo, wamewavua nguo mama zao jambo ambalo ni laana kwao na waliowatuma. Lazima wachovu tushikamane na kulaani na kukomesha ushenzi huu unaofanywa na gendaeka tuliowaamini ofisi zetu. Haiwezekani kutenzwa kama watumwa kwenye kaya yetu wenyewe. Shenzi yao kabisa.”
Kanji naye anachomekea, “Sasa hii data kwanini napasapasa mama yao? Hapana ogopa sheria ya bakaji hii data au kwa vile yeye data basi nafanya yoyote nataka? Kama naendelea fanya hiii vatu naveza chukua sheria kononi yao.”
Msomi Mkatatamaa anakula mic, “Mie siwalaumu ndata ingawa siungi mkono uhuni walioamriwa na wahuni wakubwa kutenda. Mbwa akikung’ata huwezi kuhangaika na mbwa mwenyewe bali aliyemtuma. Hivyo, hapa lazima tujue nani alitoa amri hii ya kihuni, kwa misingi gani, sheria zipi na kwa faida ya nani? Sijui kama huyu–au tuseme hawa–waliotoa hii amri kama wanajua walichokuwa wakifanya pamoja na madhara yake kwao, kaya na mstakabali mzima wa kaya. Kisheria, mihimili mitatu ya dola inapaswa kutoingiliana, kuheshimiana na kuheshimu mamlaka ya mwenzake. Hii ni sheria. Kimakonde hii huitwa separation of powers. Nimefundisha somo hili nilipokuwa chuo huko majuu ambako mtenganisho wa mamlaka uheshimiwa sana. Hivyo, najua hatari inayowangojea kama waishiwa watajiepusha ushabiki wa kisiasa wa vyama vyao na kuamua kuchukua hatua mujarabu kuwashughulikia hawa muafinin na muafina walionajisi Mjengo.”
Anabwia kahawa yake na kuendelea, “Muishimiwa si mtu wala ngurumbili bali ni taasisi inayopaswa kuheshimiwa na kutoingiliwa wala kubughudhiwa, kudhalilishwa wala kutishwa. Ni mwakilishi wa wachovu wote waliotumia njuluku zao kibao kumpata awawakilishe kwa heshima na bila kubughudhiwa. Hivyo, lazima kwanza nilaani kitendo hiki na kushauri waathirika kuchukua sheria hasa kutumia nguvu yao kisheria ku-impeach lisirikili ili lijue wao si watu wa kuchezewa. Kwani unapompiga au kumdhalilisha mhishimiwa, unadhalilisha jimbo zima lililomtuma. Hii ni sheria na si maneno yangu.”
Mzee Maneno anaamua kutia guu. Anazoza, “Mhishimiwa wangu anadai kuibiwa laptop yake huku mwingine akisema alipapaswa na wahuni mchana kweupe ukiachia wengine kuibiwa vidani na vijisimu vyao.”
Kabla ya kuendelea, Kapenda anakula mic, “Hii ni aina mpya ya uhuni unaoweza kuzidi hata wendawazimu maana mwendawazimu hufanya wendawazimu kwa vile si mzima kiakili.
Leo mwaingiza ndata. Kesho si mtaingiza ndutu? Lazima tuulaani kwa nguvu zote huku tukionya usirudiwe.”
Mgosi anapoka mic, “Tinapaswa kushinikiza ili tijue waiotoa amui ya kuwadhaiisha wahisimiwa ili nao wachukuiwe hatua za kisheia bia kujai ukubwa wa vyeo vyao.”
Kijiwe kikiwa kinanoga si likapita karandinga la ndata. Acha tulifurushe huku tukitaka tuwafanyie kitu mbaya ili siku nyingine wakatae amri chafu na mbovu za kuwadhalilisha wahishimiwa wetu. Waheshimu mamlaka ya umma na kutumia sheria bila ubaguzi. Shenzi yao kabisa!
Chanzo: Tanzania Daima, Feb 10, 2016.
No comments:
Post a Comment