The Chant of Savant

Tuesday 16 February 2016

Serikali itangaze mgogoro na India



            Kitendo cha binti wa kitanzania kupigwa, kudhalilishwa, kuchomewa gari na kuvuliwa nguo hadharani na wananchi wenye hasira mjini Bangalore India licha ya kuwa cha kibaguzi na cha kinyama, kimedhalilisha taifa letu. Hakuna namna nyingine ya kuelezea jinai hii itokanayo na ubaguzi–tena unaofanywa na jamii ambayo tumeifuga hata baada ya kuletwa na wakoloni kutuhujumu kwa kununua mazao yetu kwa bei nafuu na kuwauzia waliowaleta–ni cha kulaaniwa kwa nguvu zote. Kitendo hiki kinaibua chuki na dharau dhidi ya waafrika kwa ujumla wao vilivyokuwa vimejificha kwenye jamii ambayo tumekuwa tukidhani ni wenzetu kumbe siyo. Huu ni ushahidi kuwa–kwa wabaguzi hawa–hata wanyama wana thamani kuliko mtu mweusi.
            Kwa mujibu wa NDTV ya India, binti mtanzania alifikwa na balaa hili baada ya kijana wa Kisudan kumgonga mama wa kihindi jambo ambalo lilihalalisha mashambulizi dhidi ya muafrika yeyote waliyemuona mbele yao. Japo wengi wanaweza kurahisisha tukio hili kama watu wenye hasira ambao wako katika kila nchi, kitendo cha kulenga mtu kwa sababu ya rangi yake–na si ushiriki wake katika kutenda kosa–kinaonyesha ubaguzi na chuki vya wazi wazi dhidi ya waafrika. Sijui kama waliotenda jinai hii ya kibaguzi wanafahamu kuwa wana ndugu zao wateule wanaoishi kwenye nchi za hao hao weusi wanaowachukia, kuwabagua, kuwadhalilisha na kuwadharau. Je kama na wahanga wa ubaguzi huu–Mungu apishie mbali–wataamua kufanya jino kwa jino, kutakalika. Ndiyo, maana hakuna mtu mwenye akili zake ataonewa, kunyanyaswa, kubaguliwa na kudharauliwa asijihami kama mtu binafsi au jamii. Hii ni hulka ya binadamu yeyote mwenye akili timamu ingawa waafrika hawana silka na hulka ya ubaguzi au ulipizazi visasi. Hata hivyo, mambo yamebadilika.
             Tuseme wazi bila uficho wala woga. Kumekuwa na unafiki na woga wa kuwaambia wenzetu kuwa mfumo wao wa kibaguzi haupaswi kuwa nafasi katika bara hili. Ni bahati mbaya kuwa ni watu wachache waliokuwa na ithibati na uthubutu wa kuliona hili na kulisemea wazi wazi wakiongozwa na marehemu mchungaji Christopher Mtikila ambaye ukali wake angalau ulipunguza makali ya ubaguzi wa wazi.
            Pamoja na ndugu zetu wa kihindi kuishi nasi kwa miaka nenda rudi, wamejitahidi kuendeleza mfumo wa kibaguzi –utokanao na jadi yao ya matabaka, caste system–nasi, kwa woga, ujinga na hata ufisadi, tumeuvumilia na kuuzoea kana kwamba ni haki. Sasa unaanza kutugeukia ambapo watu wetu hawana hata uhuru wa kwenda kwao na kuishi bila bughudha kama wanavyoishi kwetu.  Ni vizuri unapoibua hoja kuitolea ushahidi. Hebu jiulize–kwa mfano–leo utaona waswahili waliooa au kuolewa na wazungu lakini si kwa wahindi. Kwanini tena kwa jamii ambayo tumeishi nayo kwa miaka mingi kama hakuna harufu ya ubaguzi ingawa suala la nani amuoe au kuolewa na nani ni haki ya mtu binafsi? Hata hivyo, haiwezekani kwa jamii nzima yenye watu wengi wasitokee wachache wakavunja mwiko huu wa kibaguzi kama hakuna namna ya kuzuia hili kutokea.  Kimsingi, ujinga wetu umelea huu ubaguzi. Wengine wana hata mashule yao binafsi kwa kisingizio cha dini na mambo mengine ya kijinga na kibaguzi. Wanaishi kwenye maeneo yao maalumu hasa katika kati ya miji kwenye nyumba za Msajili ambazo marehemu baba wa taifa alitaifisha baada ya kugundua zilivyokuwa zimejengwa kwa fedha iliyotokana na kuwanyonya na kuwaibia waswahili.
            Waswahili ni watu wakarimu lakini si wajinga na wapumbavu kiasi cha kubaguliwa wazi wazi hivi. Sijui kama kuna mbunge Mswahili huko India ikilinganishwa na hapa. Sijui kama kuna waswahili wanapewa hata huo uraia wa India ingawa hauna faida wala thamani kwao. Rejea Waswahili wajulikanao kama Jarawa kwenye kisiwa cha Andaman huko India ambao–pamoja na kuishi karne ya ishirini na moja–bado wametengwa na kuishi kama wanyama huku wenyeji wao wakiwatumia kama kivutio cha utalii. Je wao wangefanyiwa hivyo hapa wangefurahi?
            Hata hivyo, binadamu ana nini hadi ambague mwenzie wakati akijisaidia bila kutawaza au kuishi bila kupiga mswaki ananuka kuliko hata nguruwe? Heri mbuzi na ng’ombe wangetubagua na ingeleta maana hasa ikizingatiwa kuwa huwa hawatawazi wanapojisaidia wala kupiga miswaki kila uchao lakini bado hawanuki. Kwanini serikali ya India haiwaambii ukweli watu wao kuwa nchi nyingi za kiafrika –baada ya kuua huduma zao za jamii –zinatunisha hazina yake kwa kupeleka wagonjwa na wanafunzi kule ukichia mbali kununua bidhaa feki toka kule mbali na kuwahifadhi watu wao walioletwa na wakoloni? Najua ukweli huu unauma. Ila ndiyo ukweli ambao tunapaswa kuambiana ili tuthaminiane na kuheshimiana. Nani hajui kuwa baadhi ya wabaguzi hawa huwanyonya wafanyakazi wengi wa Kiswahili huku mamlaka zetu za hovyo zisifanye kitu kana kwamba hazijui uwepo wa jinai hii ya ubaguzi?
            Tumalizie kwa kuuliza. Nani atamshughukia nani ilhali wengi wao ni wawezeshaji wa kashfa za wizi wa mabilioni wakishirikiana na wezi wazawa wenye mamlaka. Rejea kashfa za escrow na Singasinga nyuma yake, mashamba, Chavda na rada, Vithlani ukiachia mbali kashfa ya ndege ya Valambia.
Chanzo: Tanzania Daima, Feb., 14, 2016.

No comments: