Ukiachia marehemu Christopher Mtikila, hakuna mwanasiasa aliye hai kwa sasa anayeweza kuwa amekumbwa na msukosuko ya kisiasa kama mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu ambaye pia ni rais wa Chama cha wanasheria nchini (TLS) na mwanasheria mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA). Lissu amejizolea umaarufu kwa kutokuwa mwoga na mweledi wa masuala mengi ambaye amezua mijadala mingi bungeni na nchini kwa ujumla. Naandika makala hii si kwa lengo la kumtetea bali kueleza ukweli ninaoona.
Hivi karibuni Lissu alikamatwa kwa kudai kuwa ndege ya Tanzania iliyonunuliwa Kanada Bombardier Q-400 imekamatwa tokana na serikali kudaiwa fedha na mkandarasi aliyevunjiwa mkataba. Hili nililijadili kwa utuo wiki jana. Leo nitajielekeza kwenye kwanini serikali haina haja ya kupoteza muda wake na kumpotezea muda Lissu ukiachia mbali kuingilia uhuru wake wa kutoa maoni na kumtesa kwa kumweka ndani bila makosa yanayoingia akilini.
Kwanza, serikali inatumia visivyo polisi wetu ambao wanafanya kazi na kulipwa kodi zetu ukiachia mbali kuajiliwa kuwalinda watanzania bila ubaguzi wala upendeleo tokana na itikadi ya mhusika. Kuendelea kuwatumia kutaka kuwatisha au kuwanyamazisha wakosoaji ni matumizi mabaya ya kodi za wananchi.
Pili, litendo hiki kinawajengea uhasama na wananchi hasa wanapoona wawakilishi wao wakidhalilishwa na kunyanyaswa ukiachia mbali kuteswa. Kimsingi, unapomtesa au kumdhalilisha mbunge, unawadhalilisha waliomtuma. Kwani, kila anachofanya, anakifanya tokana na wadhifa huu. Wahenga wanasema: Mjumbe auwawi. Kwani anachosema si maneno yake bali ya wale waliomtuma.
Tatu, mbali na hili, kutumika polisi vibaya kunawaondolea imani toka kwa wananchi kiasi cha kuwanyima usaidizi wanapouhitaji kwenye kutimiza majukumu yao. Kwani, wanaowaona kama maadui zaidi ya marafiki na wenzao katika kusukuma gurudumu la maendeleo. Hili tulilishuhudia sikun zilizopita wakati jeshi la polisi likisifika kuwaua wananchi. Baadhi ya vituo vya polisi vilichomwa sehemu mbali mbali nchini.
Nne, licha ya kulitumia jeshi la polisi vibaya kutaka kuwatisha na kuwanyamazisha wapinzani, serikali imekuwa ikilidhalilisha. Kwani, kikatiba, jeshi la polisi halipaswi kutumikia au kutumiwa na wanasiasa wala kulalia upande moja. Linapaswa kuwatumikia watanzania bila upendeleo kama ilivyo sasa.
Tano, jeshi la polisi limeonyesha udhaifu mkubwa kwa kushindwa kuwashughulikia wahalifu kama vile wala rushwa na wengine wanaohatarisha usalama wa taifa kama vile wauza unga. Unashindwa kuelewa; inakuwaje watuhumiwa kama vile wale wa wizi wa Kagoda, Lugumi, EPA, SUKITA na ufisadi mwingine wa kutisha kuendelea kutanua huku jeshi likiwagwaya na kuwaandamana wapinzani kwa vile wanakosoa serikali iliyoingiza taifa kwenye migogoro mingi kama vile ufisadi wa kutisha na majanga mengine kama kughushi ambako siku hizi kumekuwa kukishughulikiwa kwa upendeleo.
Sasa nini kifanyike? Nadhani kuna haja ya kuwapa elimu ya haki za binadamu polisi wetu ili wajue mipaka na umuhimu wa madaraka yao. Tokana na mbinu ya mkoloni ya kutaka kuwaonea watawaliwa, alizoea kuajiri watu wasio na elimu ya kutosha kama polisi ili awatumie kuwadhalilisha wenzao bila kumuasi. Ni bahati mbaya kuwa kwa sasa tuna wasomi wengi kwenye jeshi la polisi wasioonyesha usomi wao kwa kusimamia haki za binadamu na sheria bila kuogopa kuwahoji wakubwa zao hasa wanapowapa amri zilizo kinyume. Msomi siku zote ni muasi; na hawezi kuburuzwa kirahisi hata kama yuko chini ya yule anayefanya hivyo.
Unaweza kuona upungufu katika elimu ya baadhi ya watu wetu pale, kwa mfano, mkuu wa wilaya au mkoa anapowaamuru polisi wamkamate mbunge bila hata kuwasiliana na bunge kama inavyotakiwa na sheria. Hawa wanaofanya hivi, wangekuwa wamepata elimu ya haki za binadamu ya kutosha hata sheria, wangeweza kugoma na kuwakumbusha wakubwa zao kuwa sheria haisemi wanavyotaka wafanye.
Nitatoa kisa kimoja kilichotokea hapa Kanada kwenye jimbo la Newfoundland and Labrador. Waziri mkuu (mwanasheria na tajiri) wa zamani wa jimbo hili akiwa anaendesha gari lake la bei mbaya, aliamua kupokea simu akijua ilikuwa kinyume cha sheria jimboni humo. Akiwa hana hili wala lile, alistukia polisi tena mdogo akimsimamisha na kumtaka aweke gari kando. Huyu bwana alijua amevunja sheria. Hakufanya fujo wala kutoa vitisho. Alimuuliza polisi “ofisa, mbona umenisimamisha?” Polisi alimjibu “bwana waziri mkuu unajua kosa ulilofanya.”
Kwa vile kwenye nchi za wenzetu viongozi ni watumishi wa watu na wanaowajibika vilivyo kisheria, waziri mkuu alimuomba yule askari mdogo amsamehe. Askari alimpa sharti moja kuwa aende kwenye televisheni ya mkoa aombe msamaha na kueleza kosa alilotenda. Waziri mkuu alifanya hivyo na akasamehewa. Yule askari jasiri wala hakufanywa kitu zaidi ya kuwa maarufu na wa kupigiwa mfano. Je ingekuwa kwenye nchi ambapo jeshi la polisi linadhalilishwa kwa kutumiwa na wakubwa wa kisiasa, unadhani waziri mkuu angekubali kusimama wala kuomba msamaha? Kwanza, angekamatwaje wakati kila aendako ana ving’ora na misururu ambavyo huongeza mzigo kwa mlipa kodi maskini tena kwenye nchi zinaishi kwa kuombaomba na kukopakopa? Hapa Kanada, mawaziri huendesha magari yao na hawana walinzi isipokuwa waziri mkuu pekee ambaye ni mkuu wa serikali.
Tuhitimishe kwa kurejea tulikoanzia. Kuendelea kumsakama na kumakamata Lissu ni kumpa umaarufu na ujasiri wa kuhoji zaidi. Kama alivyowahi kusema mbunge wa Arusha Godbless Lema kuwa kadri unavyowekwa ndani unakomazwa, kuondolewa woga na kupambana zaidi.
Chanzo: Tanzania Daima J'tano leo.
No comments:
Post a Comment