Uchaguzi mkuu ulioisha nchini Kenya umeacha mafunzo mengi kwa Kenya na Afrika kuhusiana na demokrasia, haki, uwazi na ukweli katika uchaguzi. Katika makala hii, tutadurusu baadhi ya mafunzo na mapungufu ya uchaguzi husika.
Ukabila
Hakuna shaka. Uchaguzi wa mkuu uliopita nchini Kenya, ulitia mhuri kwenye dhana kuwa taifa hili ni la kikabila. Hili halina mjadala wala kuomba radhi; lilijitokeza Dhahiri. Kwani, wakenya walio wengi walichagua kwa kuzingatia ukabila zaidi ya masuala. Hili liko dhahiri. Ukiangalia namna wagombea wawili walioogoza yaani rais Uhuru Kenya na mpinzani wake Raila Odinga, unagundua kuwa kila mmoja alishinda, ima kwenye eneo la kabila lake, au wanakotoka washirika wake. Mfano, Kenyatta alipata kura nyingi kwenye majimbo ya Kati na Bonde la Ufa na makamu wake Wiliam Ruto mtawalia huku Odinga akishinda kwenye majimbo ya Nyanza, Magharibi na Pwani wanakotoka na washirika wake mtawalia.
Mikwara
Kwenye kampeni zake, upinzani na baadaye baadhi ya mashirika yasiyokuwa ya kiserikali walitangaza kuwa walikuwa na vituo vya kukusanya, kuhesabu na kutangaza matokeo sambamba na Tume Huru ya Uchaguzi ya Kenya (IEBC) sawa na walivyofanya wenzao wa Ghana hadi upinzani ukamshinda rais aliyekuwako madarakani. Ajabu, baada ya kura kumalizika kupigwa na matokeo kuanza kutangazwa, si upinzani wala mashirika ya kiraia waliotimiza ahadi yao ya kukusanya, kuhesabu na kutangaza sambamba na tume ya uchaguzi kama walivyoahidiwa ukiachia mbali kuruhusiwa kisheria. Kwanini? Huenda kusema walikuwa na vituo ilikuwa ni mikwara na tishatisha kwa tume ya uchaguzi. Vinginevyo Kenya na dunia kwa ujumla wanapaswa kujua nini kilifanyika. Maana, walikuwa na haki kisheria kufanya hivyo.
Uhuni
Pamoja na kwamba hii inaweza kuonekana kama kudharau waafrika au waswahili, ukweli ni kwamba hatuko makini hasa kufanya mambo tofauti na wenzetu. Ndiyo maana tunaendelea kuwa nyuma tukilalamikalalamika hasa kwenye masuala yademokrasia, haki, ukweli, uwajibikaji na uwazi. Mfano, unashangaa namna ambavyo nchi iliyojisifia kutumia mfumo wa kielectroniki kuchezewa kama upinzani ulivyodai kwa ushahidi wa kutosha. Unajiuliza nini mantiki ya kuunguza fedha ya umma kuweka mfumo huu wa kiteknolojia kuishia kutoa matokeo yenye shaka na utata?
Hata hivyo, kuonyesha uhuni na uzembe, dalili kuwa mambo yangekwenda ndivyo sivyo zilikuwa wazi hasa baada ya kuuawa mkuu wa kitengo cha kompyuta (ICT) cha IEBC Chris Chege Msando siku chache kabla ya uchaguzi. Kwa upinzani na serikali makini, kifo hiki kingewafungua macho na kutaka kujua waliokuwa nyuma yake. Ni bahati mbaya; pande zote zilifuja fursa hii ambayo ingeepusha utata uliofuatia baada ya kutangazwa matokeo. Hata pale Marekani na Uingereza zilipojitolea kusaidia kuchunguza kifo hiki, serikali ilivutavuta miguu. Kwanini? Na upinzani nao uliridhika. Kwanini? Inashangaza uchaguzi ulioendesha kielektroniki kutoa matokeo tata na ya mdo mdo kana kwamba yalifanyika kizamni. Kwanini kuunguza mabilioni ya fedha za walipa kodi maskini kuweka vitu visivyoleta matokeo tarajiwa kama hakukuwa na namna hasa ikizingatiwa kuwa hata uchaguzi wa 2013 mchezo ulikuwa ule ule. Hapa ndipo uhuni na uswahili au uafrika vilipo.
Wanasiasa dhidi ya wananchi
Wakenya walipiga kura kwa amani na utulivu wakaishia kungojea hadi kuchoka tokana na ubovu wa mfumo na wanasiasa. Kimsingi, wananchi walicheleweshwa bila sababu ya msingi zaidi ya uhuni wa wanasiasa. Hata hivyo, koo mbili maarufu zikiwa zinatunishiana misuli, wakenya walijikuta wakitekwa kama malipo yao ya kuziendekeza koo hizi chini ya siasa za kikabila. Je tunaweza kulaumu koo husika au wakenya wenyewe walioziendekeza na kuzivumilia kwa muda mrefu? Hata palipotokea kutoridhishwa na matokeo yaliyokuwa yakizidi kuingia, waliokufa ni walalahoi na si wanasiasa.
Vyanzo fichi vya fedha za kampeni
Waliofuatilia kampeni za uchaguzi wa Kenya watakubaliana nami kuwa ulikuwa aghali kutokana na matumizi ya helkopta kwa wagombea wengi hata wadogo. Je hii fedha waliipata vipi na wapi? Si asasi za kiraia, magazeti wala wananchi wanauliza swali hili? Kwanini? Ni kwamba wanasiasa wetu ni kielelezo cha picha ya jamii yetu. Jamii fisadi huzalisha viongozi na wananchi mafisadi. Maana, kwa taifa linalojidai kuwa mbele ya yote kwenye Jumuia ya Afrika Mashariki kufanya madudu liliyofanya ni kielelezo halisi cha uoza huu wa kimfumo na kijamii. Pia ni ushahidi kuwa kenya na wakenya walikuwa wagumu wa kujifunza tokana na kadhia ya mauaji ya kikabila yaliyotokana na kadhia kama hii hapo mwaka 2007.
Pongezi
Pamoja na mapungufu tajwa, bado uchaguzi wa Kenya una mafunzo mengi. Wakenya walipiga kura kwa amani na utulivu wakaja kuvurugwa na wanasiasa. Kama wanasiasa waneonyesha busara walizoonyesha wananchi, huenda mtafaruko na sintofahamu tulivyoshuhudia visingetokea.
Kwa ufupi ni kwamba ili Afrika iwe na uchaguzi uhuru na wa haki na wenye kuleta maana, kunahitajika mabadiliko mengi. Badala ya kutegemea nyuso za watu au koo zao na vyama vyao, Afrika inahitaji kujenga taasisi madhubuti na zenye kuaminika ili kuondokana na kufanya mambo kijima na kitwahuti kama ilivyojitokeza kwenye uchaguzi tajwa.
Chanzo: Tanzania Daima Jpili leo.
No comments:
Post a Comment