How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Tuesday, 15 August 2017

Misaada ya Bill Gates: Ushauri kwa Magufuli

            Kwa wanaofuatilia kiasi cha misaada iliyokwishakutolewa na tajiri mkubwa kuliko wote ulimwenguni, Bill Henry Gates III, watakubaliana nami kuwa anaipenda Tanzania kupita kiasi. Kwani hivi karibuni alitoa msaada wa shilingi bilioni 777 takribani dola milioni 300 na ushei za kimarekani. Hii si pesa ndogo hasa kwa nchi maskini na ombaomba ambayo inapoteza fedha nyingi kwenye ufisadi. Na hili Gates analilfahamu fika; japo amevutiwa na kuridhishwa na juhudi za makusudi za rais Magufuli ambaye bila shaka watakuwa marafiki. Magufuli na Tanzania wasipoteze fursa hii ambayo ni bahati ya mtende. Nasema hivi nikizingatia ukweli kuwa msaada aliotoa Gates ni mkubwa kuliko misaada ya baadhi ya nchi tena kubwa na zenye kufungamanisha masharti kwenye misaada yao. Nadhani hapa niseme wazi. Anachotaka Gate ni kuona ule msaada unawafikia walengwa. Hapa lazima nionye. Mambo ya ufisadi na business as usual lazima yaepukwe ili kutomkatisha tamaa mfadhili huyu anayetoa misaada kwa kuzingatia ubinadamu kuliko kutafuta faida na sifa au kutaka kuwalazimisha walengwa kufuata mambo fulani hata kama hawakubaliana nayo.
            Pia fedha aliyotoa Gates ni ushahidi kuwa wanaobeza juhudi za Magufuli wafikirie upya. Kwani, licha ya kusafisha nchi na kupambana na ufisadi vilivyo, amekuwa kivutio cha aina yake si kwa wawekezaji tu bali hata wafadhili.
            Kawaida ya waafrika, mikono mitupu huwa hairambwi. Hivyo, hivyo, unapopokea mgeni aliyebeba chochote, licha ya kumchinjia kuku, mbuzi au ng’ombe kulingana na uwezo wako, huwezi kumwacha arudi nyumbani mikono mitupu. Ukifanya hivyo utaonekana bahiri na mwizi wa fadhira. Hivyo basi, napendekeza rais Magufuli arejeshe mkono kwa Gates angalau kwa kumpa nishani ya juu kama heshima ya kutambua mchango wake kwa Tanzania. Kwa nchi shapu, hata vyuo vyetu vikuu vingemuarika kutoa mihadhara hata kumshawishi vimpe shahada za heshima ili avisaidie. Kwanini walishindwa hata kumuita na kulipa jengo au mtaa mojawapo jina lake kama motisha? Huku si kujipendekeza wala kujidhalilisha. Ndiyo sayansi ya jamii ya kisasa ya kuvutia wenye nazo. Bahati nzuri, Gates hatafuti kuilazimisha Tanzania kufanya lolote kinyume na ilivyojipangia kama ilivyotokea kwa mfuko wa Milennium ambao uliinyima Tanzania misaada kutokana na kadhia ya uchaguzi wa Zanzibar. Wala Gates si kuwadi wa serikali ya kwao kusema kuwa anatoa misaada hii ili kutafuta leverage kwa taifa lake.
            Kwanini tunasema kuwa Gates anapaswa kuenziwa na kuengwaengwa. Wenzetu wanathamini sana heshima kuliko kitu chochote. Isitoshe, Gates si maskini wa kuhitaji pesa zaidi ya kuengwaengwa na kuenziwa. Kama ni utajiri unaohangaisha wengi duniani alishaupata miaka mingi iliyopita kiasi cha kutosheka na kugawana na maskini lau nao waonje raha ya maisha. Huyu si mtu wa kuacha hivi hivi hasa ikizingatiwa kuwa kuna wengi wanaomsaka usiku na mchana wasimpate; n ahata wengine wakimpata wasiambulie chochote.
            Tokana na mapenzi aliyoonyeshakwa Tanzania, namshauri rais amuarike rasmi kutembelea Tanzania kama mgeni rasmi na si mfadhili; na akifika, ampe tuzo ya juu ya taifa ili kumpa motisha wa kuendelea kusaidia Tanzania. Kumpa nishani, licha ya kummotisha, kunampa faraja kuwa juhudi na misaada yake vinatambulika. Hivyo, si ajabu, baada ya kuonyeshwa anavyothaminiwa na kuenziwa, Gates akaongeza kasi ya kusaidia taifa. Kwani wakati akileta msaada huu mkubwa, kuna nchi zinazomeza mate hata kutafuta namna ya kumvutia kwao hata kama ni kwa kumfitinisha na Tanzania. Hivyo, urafiki huu ulioanzishwa unapaswa kulindwa kama mboni ya jicho.
            Sina haja wala sina sababu ya kumkosoa rais Magufuli. Hata lugha aliyotumia kusema kuwa Gates alileta fedha Tanzania kwa vile hakuwa na pa kuzipeleka si sahihi. Gates anako kwa kupeleka fedha zake hasa ikizingatiwa kuwa dunia imejaa maskini wanaohitaji msaada wake. Pia, ukiachia mbali na kutoa misaada, Gates ana biashara nyingi anakoweza kutumbukiza fedha zake ukiachia mbali benki. Hivyo, atakaporejea mara nyingine, tuchunge lugha ya kutumia. Najua rais hakuwa na nia mbaya kusema aliyosema. Hata hivyo, binadamu tumejaliwa ujuzi na utaalamu tofauti. Kwa mtu anayejua hawa jamaa wanavyofikiria, rais alipaswa kumpongeza kwa kuipenda na kuipendelea Tanzania lakini si kusema hakuwa na pa kupeleka fedha. Waswahili wanasema mwenye matunda hakosi wajukuu. Nishauri tu kuwa tunanapaswa kufanya vitu kisasa kwa kuzingatia kile kinachoweza kuitwa a two way traffic. Unanipa hiki; nami nakupa kile. Nasema hivi kutokana na ukweli kuwa Gates hatafuti faida yoyote Tanzania zaidi ya kuona kuwa mchango wake unaleta mabadiliko na kuthaminiwa.
            Nimalizie kwa kumshukuru na kumpongeza Gates pamoja na rais Magufuli kwa kuwa na mazingira wezeshi yaliyowafanya kuaminiana na kusaidiana. La muhimu ni kuwahimiza wale watakaosimamia miradi inayolengwa kutekelezwa na fedha husika waachane na upogo na ubinafsi wa kujihusisha na ufisadi ili wasimkatishe tamaa mfadhili huyu. Hatujui analenga kufanya mambo mengine mangapi kwa taifa kama miradi husika itakamilishwa kwa ufanisi na wakati.
Chanzo: Tanzania Daima J'tano leo.

No comments: