Juzi nilitaka kuzimia baada ya kujua kuwa kumbe pamoja na tanzanite kuchimbwa Bongo aka Danganyika pekee, inauzwa kwa sana India na Kenya kiasi cha kuwa kaya zinazosifika kuzalisha tanzanite. Nikiwa zangu jijini New York nilikokwenda kujuana na Katibu Mkuu mpya wa baraza kuu la walevi la umoja wa mataifa; si bi nkubwa akanipiga bomu akitaka nimnunulie kidani cha tanzanite. Kwa vile nilikuwa na uchache wa kubwaga tena dola siyo madafu, niliamua kutia timu kwenye duka moja liitwalo Mickey Mouse’s na kukuta tanzanite bwerere. Baada ya kuchagua kitu nilichotaka na kulipa, nilimuuliza mhudumu mmowapo walikopata vitu hivi vizito na vya bei ya kuua mtu. Bila kujua mie natokea Bongo si akanijibu kuwa inatoka Afrika!
Je unaweza kuamini kuwa na watasha ni mambumbumbu kama waswahili kudhani kila mweupe ni kutoka Ulaya sawa na watasha kudhani Afrika ni kaya moja? Basi mwenzangu baada ya kujibu hivyo, niliamua kumuuliza: Mbona Afrika ni kubwa na ni kaya zaidi ya 50 je alimaanisha Afrika ipi. Alizubaa kidogo. Kwa vile mtasha si mtu wa kukubali kuzidiwa maarifa na mswahili, aliniomba nimpe dakika tano tu. Sikumkatalia. Aliondoka na kuingia kwenye chumba; na kufungua kompyuta yake. Mara kalinasa jibu asijue hola!
Akiwa anatabasamu alirejea haraka; akiwa anajiamini kana kwamba atakachoniambia kingetoa jibu kwa swali langu. Bila kufikiri mara mbili wala kusita alisema “tunaagiza hii kitu toka ima Kenya, au India.” Nilijibu kwa mshangao “Kenya au India!” Mwenzangu alionekana kupigwa na mashangao akidhani kuna kitu si sawa kichwani mwangu. Maana, yeye ameaminishwa kuwa tanzanite inatoka ima Kenya au India lakini si Bongo.
Kwa vile visimu vya kisasa ni kama kompyuta, nilifungua ki-Samsung 10 ambacho ni toleo lililotoka juzi na wenye simu hizi hawafikii hata kumi Afrika. Nili-google na kumuonyesha kuwa tanzanite inatokea Danganyika na ndiyo maana ikaitwa hivyo. Alishanga na kutia shaka nilichokuwa nikimuonyesha.
Kufupisha hadithi ndefu ni kwamba niligundua kuwa kumbe tunapigwa kiasi cha kukosa hata credit kwa kitu kinachopatikana kayani kwetu pekee. Hivyo, tokana na hali hii niliamua niandike ujumbe huu lau wanene wetu wajue wanavyotuhujumu na kutudhalilisha tokana na kutumia makinikia ya akili badala ya akili. Hivyo, leo nitatoa mapendekezo yafuatayo:
Mosi, kwa vile wanene wetu wameridhia na huduma na ujuha huu, basi tanzanite ima iitwe gabacholinite au cholinite au kenyanite ili tujue hatuna chetu kuliko kuendelea kudanganyana kuwa haya mawe yanapatikana kwetu pekee wakati hatufaidiki nayo. Kupatikana kwetu bila faida kunatusaidia nini?
Pili, kama wanene wetu wanataka kuepuka aibu ya mwaka kiasi cha kuchekwa na ndege wakati wao wakijiona wajanja basi tuamua kuziba mianya yote inayosababisha mawe yetu yaibiwe na majizi tuliyoyadekeza na kuyajaza kayani lau nasi tufaidike na kuheshimika kutokana na mawe yetu. Nashauri, kama walivyofanya kwenye dhahabu, wafanye hivyo haraka kwa tanzanite.
Tatu, ufanyike uchunguzi tangu jiwe hili ligunduliwe kujua limekuwa likitoroshwa vipi na nani wanafanya hivyo na wanatumia mbinu gani; na walevi tumeishapata hasara kiasi gani ili tuzidai kaya zinazojidai ndizo wazalishaji wakubwa wa tanzanite wakati ni majizi watupu.
Nne, tuwaite mabalozi wa kaya husika na kuwapa madai yetu na onyo kuwa kama hawataacha mchezo wanaofanya ima tutasitisha uhusiano nao au kuwafanyia kitu mbaya. Hata hivyo, wakati tukifanya hivi, tujisute; na kubadili mfumo wa kibunga wa kufanya mambo. Haiwezekani sisi tuwe shamba la bibi maisha. Haiwezekani kuhujumu uchumi liwe kosa la jinai kayani kwetu; bado kaya nyingine liendelee kulitenda dhidi yetu; nasi tunyamaze.
Tano, nawashauri wanene wawasiliane nami niwafundishe namna ya kuwa na hati milki ya tanzanite kama ilivyo kwa dhahabu na du Bears. Hakuna kitu kinaniuma kama kuona kaya za kiafrika zikizalisha madude ya bei mbaya lakini siku zote zinaishia kuwa kama kaya za manyani. Manyani hukaa porini na kuishi na kufa maskini wakati waja wakichuma kila kitu kwenye misitu mali ya manyani. Hatuwezi kuendelea na ukuku, umbwa, ukijiko, usindano na usufuria. Nitaeleza. Kuku huzalisha mayai yenye protini na kuishia kulishwa nafaka hafifu na kavu na anayemwibia mayai yake. Mbwa hulinda mali nyingi lakini siku zote yu maskini. Sufuria huungua kila siku kupika lisile. Na sindano hushona nguo nyingi lakini siku zote iko uchi. Haya si maisha yanayowafaa walevi wa kaya hii tajiri kuliko nyingi hata zile zinazoifadhili. Tukutane wiki ijayo nikotoka kupata kanywaji.
Chanzo: Nipashe J'mosi leo.
No comments:
Post a Comment